Mchungaji Peter Msigwa. |
Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa pamoja na watuhumiwa wengine zaidi ya 70 jana walipandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Iringa wakituhumiwa kufanya makosa matatu.
Wamefikishwa mahakamani hapo, ikiwa ni siku moja baada ya wafanyabiashara ndogo 'Wamachinga’ wanaodaiwa kutii amri ya mbunge huyo, kukaidi amri halali ya serikali iliyowataka wasiendelee kufanya biashara ya gulio la kila Jumapili katika eneo la Mashinetatu la mjini Iringa.
Hatahivyo, Mchungaji Msigwa aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Katika vurugu hizo, Jeshi la Polisi lililazimika kutumia nguvu kwa kupiga mabomu ya machozi na kumwaga maji ya kuwasha ili kuwatanya wamachinga hao, waliokuwa wakiendelea kukusanyika katika eneo hilo kinyume cha sheria. Baadaye walishambulia polisi kwa mawe muda mfupi baada ya mbunge huyo kuwasili eneo hilo na kusisitiza kauli yake ya kuwataka waendelee na biashara katika eneo hilo.
Jana, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo majira ya saa nane mchana,
Mchungaji Msigwa akiwa katika gari dogo la wazi la polisi, huku watuhumiwa wengine zaidi ya 70 walifikishwa kwa karandinga la polisi.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, wakili wa serikali, Adolph Maganda alisema watuhumiwa hao kwa pamoja wanatuhumiwa kutenda makosa hayo matatu kinyume na sheria, huku mbunge huyo akisomewa mashitaka mawili likiwemo kushawishi na kufanya mkutano bila kibali.
Watuhumiwa wote walikana mashitaka dhidi yao huku wakili wa serikali akidai
kuwa hana pingamizi na dhamana kwa watuhumiwa. Akiahirisha kesi hiyo hadi Juni 3, mwaka huu, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo alisema dhamana kwa washitakiwa hao ipo wazi kwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni moja. Msigwa alikuwa wa kwanza kudhaminiwa, ingawa wengine 26 walikosa dhamana.
No comments:
Post a Comment