MAJAMBAZI WAKURUPUSHWA NA KUTUPA MAKABURINI SADAKA WALIYOIBA...

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, usiku wa kuamkia jana majambazi waliangusha mfuko wa mamilioni ya fedha na simu mbili makaburini wakati wakiwakimbia polisi baada ya kuvamia, kuvunja na kuiba fedha hizo katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Parokia ya Mkuza, Kibaha, mkoani Pwani.

Katika tukio hilo lililotokea saa tisa usiku, Polisi walipiga risasi juu baada ya kupewa taarifa na majirani, na kuwafanya majambazi hao waliokuwa tisa, kutimua mbio kwa kuruka ukuta upande wa makaburini na kuangusha mfuko wenye fedha zaidi ya Sh milioni tatu, fedha za kigeni na simu mbili.
Paroko wa kanisa hilo, Padri Mathew Chavely alimwambia mwandishi jana kuwa, majambazi hao walivunja mlango wa ofisi baada ya kuwafunga kamba walinzi na kuwawekea plasta midomoni kisha kufanikiwa kuiba fedha hizo.
“Tulijua wakitoka ofisini, wanatujia sisi nyumbani, ila kabla, watu wema walitoa taarifa polisi na mara polisi wakaja hapa, walipiga risasi wale wezi wakakimbia na fedha zote, asubuhi wakati wa uchunguzi, kumbe waliangusha fedha makaburini, karibu na kanisa,” alisema Padri Chavely.
Alipoulizwa kwa nini wakae na fedha nyingi ofisini, Padri Chavely alisema kanisani hapo hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa kanisa jipya kubwa, hivyo Jumapili ya juzi, mbali ya  kukusanya sadaka za kawaida, kulikuwa na harambee ya ujenzi wa kanisa hilo.
Padri Chavely aliwashukuru waumini na majirani kwa sala na kutoa taarifa polisi na aliwaombea majambazi hao wabadilike, wamrudie Mungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, asubuhi walimshikilia Karani wa Ofisi, Deus Cosmas kwa mahojiano, lakini walimuachia baada ya kupata simu mbili za majambazi hao zilizodondoshwa makaburini pamoja na fedha zote.
“Ni kweli saa tisa usiku leo (jana) walivamia kanisa hilo, wezi waliokuwa tisa, wakiwa na silaha za jadi kama marungu, mapanga, nyundo na nyinginezo, tulipopata taarifa tulifika mara moja na kwa kuwa hatukujua walioko ndani wana silaha gani zaidi, tuliamua kupiga risasi juu, ndipo walipokimbia kwa kuruka ukuta nyuma, eneo la makaburini,” alisema Kamanda Matei.
Akielezea zaidi tukio hilo, Kamanda Matei alisema wezi hao waliwafunga kamba na plasta walinzi kabla ya kuvunja ofisi ya kanisa na kuiba Sh 3,172,450, Dola za Marekani 13, fedha za Uganda Sh 18,700, fedha za Kenya Sh 200 na Rupia 328.
Kwa mujibu wa Polisi, kutokana na ukubwa wa eneo hilo, majambazi walitumia ukuta wa nyuma kuruka na kukimbia na wakati wakikimbia, katika eneo hilo lenye makaburi, walikuta damu kwenye misalaba kadhaa iliyoharibiwa kwa kupindishwa na kutokana na purukushani hiyo, waliangusha mfuko wenye fedha zote walizoiba na simu hizo mbili.
Kamanda Matei alisema usalama umeimarishwa eneo hilo, na kupitia simu hizo, kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), wamebaini mtandao na mambo mengi ambayo yatawawezesha kuwakamata wote wanaohusika na tukio hilo na matukio mengine mkoani humo.

No comments: