Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu. |
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, watumishi wa Serikali nchini wataanza kunufaika na mikopo nafuu ya ujenzi wa nyumba za kuishi chini ya utaratibu mpya ulioandaliwa na Serikali na unaojulikana kama Mpango Maalumu wa Nyumba za Kuishi za Watumishi wa Umma – Public Servant Housing Scheme.
Kwa mujibu wa mikopo hiyo ya nyumba inayotarajiwa kuanza Septemba mwaka huu, watumishi watapaswa kulipa deni taratibu katika kipindi cha miaka 25.
Mpango huo ulitangazwa mwishoni mwa wiki na Rais Jakaya Kikwete wakati wa hotuba yake ya kufunga Wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye bustani ya Nyerere Square mjini Dodoma.
Hata kabla ya kuutangaza mradi huo hadharani mjini Dodoma, Rais Kikwete alikwishaambiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Beno Ndullu kuwa chini ya Mpango huo utakaoanza na nyumba 5,000 kote nchini, watumishi wa Serikali wataweza kukopa nyumba za bei nafuu au kuchukua mikopo nafuu ambayo italipwa katika kipindi cha miaka 25.
Gavana Ndullu alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu iliyoteuliwa na Rais Kikwete kuangalia jinsi ya kuwasaidia watumishi wa Serikali katika Tanzania kuweza kupata mikopo nafuu ama kukopa nyumba za bei nafuu ambayo iliwasilisha ripoti yake kwake katika mkutano uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam katikati ya wiki iliyopita.
Chini ya mpango huo, ambao utaendeshwa na kampuni iitwayo Watumishi Housing Company Limited iliyoandikishwa na kupewa usajili Februari mwaka huu, kiasi cha nyumba 5,000 zitajengwa katika miaka ya kwanza mitano, mwaka wa kwanza zitajengwa nyumba 2,500.
Mpaka sasa kiasi cha Sh bilioni 68 zimekwishapatikana kati ya kiasi cha Sh bilioni 358 zinazotarajiwa kuwekezwa katika Mradi huo katika miaka hiyo mitano ya mwanzo na itakuwa ni kampuni hiyo ambayo itajenga nyumba za gharama nafuu na kuwezesha kupatikana kwa mikopo nafuu kwa watumishi ambao watapendelea kukopa fedha ili kujenga wenyewe nyumba za kuishi.
Taasisi zitakazoshiriki katika kampuni hiyo ni pamoja na mifuko ya Hifadhi ya jamii ya NSSF, PPF, PSPF, LAPF, GEPF, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mbali na taasisi hizo, pia benki 10 zimekubali kushiriki katika mradi huo. Mabenki hayo ambayo yatakuwa yanatoza riba ya kati ya asilimia 10 na 13 kwa miaka yote 25 ya mkopo ni NMB, CRDB, NBC, Bank of Africa, Azania Bank, EXIM Bank, Banc ABC, NIC Bank, DCB Bank na KCB.
Mpango huo wa Serikali ni nje ya ule wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo pia limejikita katika kuondoa uhaba wa nyumba bora za makazi na biashara katika sehemu mbalimbali nchini, huku shirika hilo likilenga kujenga nyumba 15,000 katika kipindi cha miaka mitano.
No comments:
Post a Comment