KUSHOTO: Mchungaji Peter Msigwa. KULIA: Machinga wakilisukuma gari la mbunge huyo eneo la tukio jana. |
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amekamatwa na Polisi, na leo atafikishwa mahakamani, akihusishwa na vurugu kati ya wafanyabiashara ndogo (machinga) na Polisi.
Pamoja na mbunge huyo, wafanyabiashara zaidi ya 60 waliokuwa wakifanya biashara katika eneo la Mashinetatu, lililopigwa marufuku kwa biashara na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa, pia walikamatwa na wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo.
Vurugu hizo zilianza katikati ya mji wa Iringa, kati ya Polisi na machinga na zilidumu kwa zaidi ya saa sita.
Machinga hao waliodai kuruhusiwa na Mbunge huyo kuendelea na biashara, walirusha mawe kupinga kuondolewa katika eneo hilo, huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Abiria waendao mikoani walishindwa kuitumia stendi kuu ya mabasi ya mjini Iringa iliyoko karibu na eneo hilo kutokana na vurugu hizo.
Baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria, walilazimika kuondoa mabasi yao na kuyapeleka karibu na uwanja wa Mwembetogwa, unaotumiwa kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo mikutano ya hadhara kusubiri abiria wao.
Katika vurugu hizo zilizoanza saa tatu asubuhi na kuendelea hadi saa nane mchana, machinga hao walirusha ovyo mawe yaliyowajeruhi baadhi ya watu, na kuharibu mali mbalimbali katika eneo hilo kama njia ya kuwazuia askari hao, wakiwemo wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kuendelea na azma yao kuwatimua.
Pamoja na kuharibu mali ambazo aina yake na thamani yake haijajulikana, machinga hao waliharibu gari la Zimamoto kwa kuvunja vioo vyake na kulirushia matairi machakavu yaliyokuwa yamewashwa moto.
Vurugu hizo zinadaiwa kuwa matokeo ya kauli za Msigwa, alizonukuliwa akizitoa katika mikutano mbalimbali ya siasa, aliyofanya mjini hapa hivi karibuni.
Katika mikutano hiyo, ukiwemo ule uliohutubiwa na baadhi ya wabunge waliosimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano, Mchungaji Msigwa inadaiwa alisema haiwezekani machinga wa Iringa wakapelekwa katika eneo lisilo na biashara.
“Mbona Arusha na Mwanza, halmashauri zao kwa kushirikiana na vyombo vya dola walijaribu kuwaondoa lakini wakashindwa? Niko pamoja na masikini, kamwe sitawakumbatia matajiri kwa hiyo natangaza rasmi mrudi eneo la Mashinetatu na niko nyuma yenu,” alisema.
Baada ya kutoa kauli hiyo katika mkutano huo, machinga hao walirejea na kufanya biashara katika eneo hilo Jumapili ya kwanza, lakini wakadhibitiwa.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya machinga na ambazo zimethibitishwa na baadhi ya viongozi wa Chadema wa mjini hapa, zinaonesha kwamba Mchungaji Msigwa aliyerejea mjini hapa hivi karibuni akitokea mjini Dodoma, alitoa taarifa ya kuwataka machinga hao kuondoa woga na kurudi katika eneo hilo.
Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo za jana, machinga hao walioonekana kuogopa nguvu ya Polisi, lakini walihamasika kupambana na polisi ili waendelee na biashara zao, baada ya Mchungaji Msigwa kuwasili katika eneo hilo saa tatu asubuhi.
Baada ya kufika katika eneo hilo, Mchungaji Msigwa akiwa na gari lake la ubunge, alisikika akiwataka wafanyabiashara hao kuendelea na biashara zao katika eneo hilo, na baada ya muda alitoweka eneo hilo kabla ya Polisi kuanza kuwatawanya machinga hao kwa mabomu ya machozi walipoanza kupanga biashara zao.
Wakitoa maoni yao kuhusu vurugu hizo, ambazo ni za kwanza kutokea mjini Iringa, baadhi ya wananchi ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walitofautina huku baadhi yao wakiunga mkono na wengine wakilaumu kauli za kisiasa zinazotolewa na baadhi ya viongozi na kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.
“Kwa upande mmoja, machinga wana haki ya kufanya biashara katika eneo lenye wateja, lakini kwa upande mwingine ni lazima wazingatie sheria,” alisema mmoja wao.
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Samson Mwangoka, alisema Serikali imetumia nguvu kubwa inayozidisha umaarufu kwa Mchungaji Msigwa na chama chake.
“Lakini kwa upande mwingine kauli za Msigwa zinakinzana na uamuzi alioshiriki kuutoa ndani ya vikao vya baraza la madiwani,” alisema.
Alisema kukamatwa kwa Msigwa na wafuasi hao, kutaziwezesha mamlaka zinazohusika kutumia njia za kisheria na kistaarabu kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo.
Kabla ya kukamatwa kwake, Msigwa alizungumza na baadhi ya wanahabari na kusema yupo tayari kukamatwa kwa sababu anachofanya ni kutetea haki za wapiga kura wake.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Polisi zimesema Mchungaji Msigwa, baadhi ya viongozi wa chama hicho na machinga waliokamatwa, watafikishwa mahakamani leo.
No comments:
Post a Comment