SERIKALI YARIDHIA SHERIA YA KUSIMAMIA VYOMBO VYA HABARI...

Dk Fenella Mukangara.
Kutokana na kushamiri kwa vitendo vya vyombo vya habari kukiuka na kutozingatia maadili ya taaluma ya habari, serikali imesema sasa imeridhia kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari nchini.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alisema bungeni mjini hapa jana kwamba Muswada wa kutunga sheria hiyo utawasilishwa bungeni baadaye mwaka huu.
Akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, Dk Mukangara alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge, Wizara hiyo itaanza kuandaa waraka wa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari na kwamba sasa Serikali inaendelea kupata uzoefu kutoka nchi mbalimbali zenye sheria hiyo.
Alisema Serikali kupitia Sekta ya Habari ilikabiliana na changamoto mbalimbali katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 miongoni mwao zikiwa ni zile za baadhi ya vyombo vya habari kukiuka na kutozingatia maadili ya taaluma ya habari, kurusha matangazo ambayo yanakwenda kinyume cha sera, sheria na kanuni za utangazaji.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni ufinyu wa fursa za masomo ya juu ya taaluma ya habari nchini na mazingira duni ya kazi kwa baadhi ya wafanyakazi katika tasnia ya habari, lakini akasema pamoja na changamoto hizo wizara hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
“Mheshimiwa Spika, mwaka jana nililiambia Bunge lako tukufu kwamba wizara yangu imewasilisha kwenye Baraza la Mawaziri mapendekezo ya kutunga Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari nchini, nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba serikali tayari imeridhia kutungwa kwa sheria hiyo,” alisema.
Alisema kutungwa kwa sheria hiyo kutasaidia sana katika kuimarisha tasnia ya habari nchini na kupunguza kwa kiasi kikubwa baadhi ya changamoto, ikiwemo suala la mafunzo kwa waandishi wa habari na mazingira duni ya kazi na aliliomba Bunge kuunga mkono muswada huo utakapowasilishwa.
Kuhusu uratibu wa shughuli za Vitengo vya Habari, Wizara hiyo iliandaa kikao kazi cha mwaka cha Maofisa Mawasiliano wa Serikali kilichofanyika Dodoma Februari 4 hadi 9  mwaka huu ambacho kilihudhuriwa na Maofisa Mawasiliano 139 wa serikali kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji.
Kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu vituo vya utangazaji kuchochea udini, Dk Mukangara alisema katika mwaka wa fedha uliopita Wizara hiyo kupitia Kamati ya Maudhui imeendelea kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kuhusu vituo vya utangazaji kukiuka kanuni za utangazaji.
“Napenda kulialifu Bunge lako tukufu kuwa Februari 26, 2013, Kamati ya Maudhui ilivifungia kurusha matangazo kwa kipindi cha miezi sita kwa kosa la kutangaza habari za uchochezi vituo vya redio vya Kwa Neema Fm cha Mwanza na Imaan Fm cha Morogoro.
“Vituo hivyo vilitakiwa pia kuithibitishia Kamati ya Maudhui kwa maandishi kuwa havitarudia tena kutenda kosa la aina hiyo na kama vitarudia adhabu kali ya kuvifutia leseni za utangazaji itatolewa.”
Alisema katika tarehe hiyo hiyo pia Kamati hiyo ilitoa onyo kali kwa Kituo cha Redio cha Clouds Fm cha jijini Dar es Salaam na kukitoza faini ya Sh milioni tano kwa kukiuka kanuni za utangazaji.
Alizungumzia pia mikakati mbalimbali ya kuwakomboa vijana ikiwemo uratibu wa uanzishwaji wa Benki ya Vijana aliyosema mchakato wake unaendelea, kuwajengea vijana utaalamu wa kijasiriamali ambapo alisema kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), wizara ipo katika mchakato wa kutayarisha awamu ya pili ya Programu ya Kazi Nje Nje.
Alisema katika mwaka wa fedha uliopita, Wizara ilikumbana na changamoto mbalimbali miongoni mwake zikiwa ni upungufu wa Maofisa Vijana katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri za Wilaya, upungufu wa vyombo vya usafiri, upungufu wa maeneo ya vijana ya kufanyia kazi na kukosa maarifa ya biashara na ujasiriamali.
“Katika hili Wizara imeendelea kufanya kazi kwa karibu kwa kushirikiana na TAMISEMI. Mikoa yote imeagizwa kuajiri Maafisa Vijana. Ili kuhakikisha vijana nchini wanapata maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi, Wizara yangu imewasiliana na wakuu wa mikoa yote kwa ajili ya kutenga maeneo hayo,” alisema.
Lakini kabla mjadala rasmi wa bajeti ya wizara haujaanza, Bunge lilisitisha shughuli zake kabla ya muda wa kawaida ili kuichunguza Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kwa Wizara ya Habari,  Vijana, Utamaduni na Michezo kutokana na hotuba hiyo kubainika kuwa na maneno ya uchochezi.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alililazimika kuchukua hatua hiyo baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) kuomba Mwongozo wa Spika akitaka kuondolewa kwa kurasa 14 za ndani ya hotuba hiyo akisema zilikuwa na lugha ya uchochezi.
“Waheshimiwa wabunge ni hivi juzi tu sisi wenyewe tulipitisha Azimio la Bunge la kudhibiti lugha za uchochezi.
“Kwa hiyo nasitisha shughuli za Bunge hadi saa 11 jioni ili hotuba hii ikapitiwe na Kamati ya Kanuni ya Bunge ili kuangalia kama kuna lugha ya uchochezi,” alisema Spika
Makinda alipokuwa akisitisha kikao hicho cha Bunge kabla ya saa sita mchana jana. Kwa kawaida kikao cha Bunge cha asubuhi huahirishwa saa saba mchana.
Sokomoko lilianza mara tu baada ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini – Chadema), kuanza kuwasilisha hotuba ya kambi hiyo akiwafuatia Waziri, Dk Fenella Mukangara aliyewasilisha hotuba ya wizara hiyo na Said Mohamed Mtanda (Mchinga – CCM), aliyewasilisha maoni ya Kamati ya Bunge.
Katika kurasa 14 za mwanzo za hotuba yake, Mbilinyi maarufu kama Sugu, alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hatari inayowakabili waandishi wa habari nchini akisema Tanzania imegeuka kuwa si eneo salama kwao.
“Mheshimiwa Spika kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya fedheha ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni taaluma  ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao kwa Taifa na kama ajira yao.
“Kwa mujibu wa wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari Ulimwenguni (CPJ) iliyotolewa mwaka huu wa 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Tanzania ilishika nafasi ya 7 ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi wa habari,” alisema Mbilinyi.
Mbali ya maelezo hayo Mbilinyi alisema kwa mujibu wa CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa habari duniani ni kuuawa kwa kutekwa na kutishiwa maisha.
“Mheshimiwa Spika Aidha, Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa mauaji ya waandishi wa habari.
“Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya waandishi waliouawa mwaka 2012, karibu asilimia 20 waliuawa ama na maafisa wa serikali au na majeshi yake,” alisema Mbunge huyo.
Baadaye Mbilinyi alihamia upande wa kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi ambapo alisema Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na kuongozwa na Jaji Stephen Ihema imethibitisha kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya Mwangosi.
“Mheshimiwa Spika kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM na Jeshi la Polisi wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika habari zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi,” alisema Mbilinyi kabla ya kukatizwa na Zambi akiendelea kusoma hotuba hiyo yenye kurasa 54 akiwa amefikia ukurasa wa tisa.
Baada ya kusimama, Zambi alitumia kanuni namba 64 A ya Bunge ambayo inasema bila kuathiri masharti ya Ibara ya Katiba, Mbunge atawajibika kutosema maneno ya uongo na uchochezi, akisema Mbilinyi alikuwa amesema maneno ya uongo na uchochezi bungeni.
“Mheshimiwa Spika maneno aliyoyasema Mbunge (Mbilinyi) ni ya uongo. Kauli kwamba serikali ya CCM ndiyo inayowateka waandishi wa habari, kuwatoboa macho, kuwakata kucha na kuwaua ni kauli ya uongo.
“Na si maneno hayo tu, ukisoma kitabu cha hotuba hii kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa 14 imejaa maneno ya uongo na uchochezi kwamba jamii na wananchi waamini kwamba Serikali ya CCM ndiyo inayofanya matendo hayo ya kuwatoboa macho, kuwakata kucha na kuwaua waandishi,” alisema Zambi katika mwongozo wake huo.
Hali hiyo ilitosha kabisa kumfanya Spika Makinda kusimama katika kiti chake na kuahirisha kikao hicho cha Bunge hadi saa 11 jioni ili kuifanya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanuni kuipitia hotuba hiyo ili kujiridhisha.
Muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho cha Bunge, Katibu wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Neville Meena alisema jukwaa hilo lilikuwa limesikitishwa na hatua hiyo ya kukatizwa kwa hotuba iliyokuwa inaelezea hatari inayowakabili waandishi wa habari nchini.
Alisema ingawa TEF haijaipitia hotuba yote ya upinzani kuona ni maneno gani yametumika, lakini mazingira ya usalama kwa waandishi wa habari nchini ni ya hatari na kwamba Waziri Dk Mukangara alipaswa kuzungumzia mazingira hayo kupitia hotuba yake.
“Ni kweli kwamba waandishi wa habari wanauawa na kujeruhiwa vibaya. Leo hii Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya New Habari (2006), Absalom Kibanda yupo hospitali anatibiwa kwa kuumizwa vibaya, tulitegemea hotuba ya Waziri itoe hata salamu za pole kwa tukio hilo,” alisema Meena.

No comments: