BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA MWAKA 2013/2014...


HOTUBA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA MHESHIMIWA SHAMSI VUAI NAHODHA (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA  MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/2014

UTANGULIZI


1.         Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

2.         Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2013/2014 mbele ya Bunge lako Tukufu.  Pili, nawashukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu na Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais kwa kuendelea kuniamini kuiongoza Wizara ya  Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.  Namshukuru pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu. Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla kwamba nitaendelea kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

3.         Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama, Mhe.  Anna Margareth Abdallah (Mb.) na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Mohammed Seif Khatib (Mb.) kwa kuchaguliwa kuiongoza Kamati hiyo. Halikadhalika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati hiyo.  Ninawaomba wajumbe hao wapokee shukurani zangu kwa maoni waliyotupatia wakati wa kuchambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2013/2014. Maoni na mapendekezo yao yametusaidia sana katika kuiandaa hotuba hii.

4.         Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 28 Machi, 2013 Mbunge mwenzetu Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Jimbo la Chambani  alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwako Mheshimiwa Spika, familia, ndugu na marafiki kwa msiba huo.  Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Peponi. Amina.


DIRA NA DHIMA YA WIZARA YA ULINZI NA JKT


5.         Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwa Taasisi iliyotukuka ya kudumisha amani na usalama nchini. Kwa kuzingatia kwamba ulinzi wa Taifa ndilo jukumu la kwanza kwa Serikali, dhima ya Wizara hii ni kuilinda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya maadui kutoka nje au ndani ya nchi na kuhakikisha kuwa uhuru na maslahi ya Taifa letu (national interests) yanakuwa salama wakati wote. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu inaendelea kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi. Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 Sura 192 na Sheria ya JKT ya mwaka 1963 Sura 193, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekabidhiwa jukumu la kusimamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa katika kutekeleza majukumu yake. Vile vile Wizara yangu ina wajibu wa kuvipatia vyombo hivi mahitaji yake ya kimsingi ili kuviwezesha kutekeleza majukumu hayo.

MAJUKUMU YA WIZARA YA ULINZI NA JKT


6.         Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  ina majukumu saba. Kwanza, Wizara ina jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu. Pili, Wizara ya Ulinzi inasaidiana na Mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga ili kuwapatia wananchi waliofikwa na majanga misaada ya kibinadamu. Tatu, Wizara inashiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi zenye migogoro duniani. Nne, Wizara hii inaandaa umma wa Watanzania kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Taifa. Tano, Wizara inawajengea vijana wa Kitanzania moyo wa uzalendo na mshikamano wa kitaifa ili kuwaandaa kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kujitegemea. Sita, Wizara ya Ulinzi inafanya utafiti ili kuendeleza teknolojia kuhusu matumizi ya kijeshi na kiraia. Saba, Wizara hii inaimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika masuala ya Kijeshi.

MALENGO YA WIZARA YA ULINZI NA JKT



7.         Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu niliyoyataja hapo awali, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imejiwekea malengo makuu manane kwa mwaka 2013/2014.  Kwanza, kuandikisha wanajeshi wapya kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Pili, kuwaendeleza kielimu maafisa na askari wa JWTZ na JKT.  Tatu, kununua na kulipatia Jeshi zana bora kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Nne, kutunza na kuhifadhi vizuri zana za kijeshi na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi na makazi kwa wanajeshi. Tano, kuimarisha mahusiano mema na nchi nyingine duniani katika masuala ya kijeshi. Sita, kutoa mafunzo ya ulinzi wa mgambo kwa Watanzania ili kuimarisha Jeshi la Akiba. Saba, kuwapatia vijana wa Kitanzania mafunzo ya kuwajengea nidhamu, ukakamavu na moyo wa uzalendo. Nane, kuyajengea mashirika ya Mzinga, Nyumbu na SUMAJKT mazingira bora ya kukuza teknolojia ili yaweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa ruzuku ya Serikali.

 

UTEKELEZAJI WA MAONI NA USHAURI WA KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA


8.         Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2012/2013, tulipokea maoni, ushauri na maelekezo kutoka kwa iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa yamefanyiwa kazi na majibu yake yameainishwa katika Kiambatisho Na.1. Halikadhalika, hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huo pia zimezingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2013/2014 ninayowasilisha leo hapa Bungeni.

HALI YA USALAMA WA MIPAKA KATIKA MWAKA 2012/2013


9.         Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jukumu kubwa la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kulinda uhuru na usalama wa nchi yetu naomba nieleze hali ya usalama wa mipaka yetu na nchi nyingine ilivyokuwa katika mwaka 2012/2013. Hali ya usalama wa mipaka yetu na nchi jirani, nchi kavu na baharini ni shwari kwa ujumla.  Hata hivyo katika baadhi ya mipaka yetu na nchi za Uganda, Kenya na Zambia kuna tatizo la muda mrefu la kung’olewa kwa alama za mipakani yaani “beacons”. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zinaendelea kulifanyia kazi suala hili ili kuzirudisha alama hizo kwenye eneo la mpaka.

(i)                 Mpaka katika Bahari ya Hindi


10.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika eneo la mpaka wa Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilomita 1,424 ambako nchi yetu inapakana na Kenya, Visiwa vya Ushelisheli, Komoro na Msumbiji inaendelea kuwa shwari. Hivi sasa matukio ya uharamia yaliyokuwa yakitokea miaka mitatu iliyopita yamepungua kwa kiasi kikubwa. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2012 hadi sasa hakujatokea tukio lolote la uharamia katika eneo hili. Mafanikio haya yanatokana na doria zinazofanywa na Jeshi la Wananchi kupitia Kamandi yake ya Wanamaji pamoja na ulinzi unaofanywa na majeshi ya Ulaya, Asia na Marekani katika eneo la Ghuba ya Aden.

(ii)               Mpaka wa Kaskazini


11.       Mheshimiwa Spika,  hali ya usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilometa 1,190 ambako Tanzania inapakana na Kenya na Uganda inaendelea kuwa shwari. Hata hivyo kumejitokeza tatizo la wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wanaoingia nchini kwa kupitia kwenye mpaka wetu na nchi jirani. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zimekuwa zikiwasaka wahamiaji haramu pamoja na kuwatafuta mawakala wa biashara hiyo ili kuwachukulia hatua za kisheria.

(iii)             Mpaka wa Magharibi


12.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilomita 1,220 ambako Tanzania inapakana na Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni shwari. Jeshi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kudumisha ulinzi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Ili kuimarisha ulinzi wa eneo hilo Jeshi la Wananchi wa Tanzania linatarajia kupata boti 2 za kisasa mwishoni mwa mwaka huu ambazo zitatumika kufanyia doria katika Ziwa Tanganyika.

(iv)             Mpaka wa Kusini


13.       Mheshimiwa Spika, katika mpaka wa Kusini Tanzania inapakana na Msumbiji, Malawi na Zambia. Hali ya usalama katika mpaka wetu wa kusini wenye urefu wa kilomita 759 zikiwemo  kilomita 248 za maji kwenye Ziwa Nyasa ni shwari.  Kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Malawi na Tanzania mazungumzo bado yanaendelea.  Mazungumzo haya yanaratibiwa na Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

14.       Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto mbalimbali nilizozieleza, napenda kuwahakikishia wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla kwamba ulinzi wa mipaka yetu ni imara. Jeshi letu liko makini na linaendelea kuchukua tahadhari kwa kuimarisha vikosi vyake ili kudumisha ulinzi  na usalama wa nchi yetu.


MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2012/2013


15.       Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitoe taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikadiria kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 57,650,000.00 kutoka katika Mafungu yake matatu (yaani Fungu 38 – NGOME, Fungu 39 – JKT na Fungu 57 – Wizara ya Ulinzi). Hadi kufikia mwezi Machi, 2013 Mafungu hayo matatu yalikusanya mapato ya jumla ya Shilingi 27,584,536.00 sawa na asilimia 47.8 ya makadirio (Angalia Kiambatisho Na.2).

16.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu bajeti ya shilingi 1,086,550,058,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo katika Mafungu yake matatu. Kati ya fedha hizo, shilingi 678,363,492,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 408,186,566,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2013, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi 718,855,852,627.00 sawa na asilimia 66 ya bajeti yake. Kati ya fedha hizo shilingi 583,155,852,627.00 zilikuwa ni kwa Matumizi ya Kawaida. Kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo, fedha zilizopokelewa ni Shilingi 135,700,000,000.00 sawa na asilimia 33 ya fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Mchanganuo wa Matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa Mafungu yote matatu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi mwezi Machi, 2013 umeonyeshwa katika Kiambatisho Na. 3.

17.       Mheshimiwa Spika, tathmini ya fedha zilizopokelewa inaonesha kwamba mwenendo wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida hadi mwezi Machi 2013 kwa ujumla ulikuwa ni wa kuridhisha.  Fedha kwa ajili ya mishahara na marupurupu zilipokelewa kulingana na makisio ya bajeti. Hata hivyo, fedha zilizotolewa kwa ajili ya shughuli  za Maendeleo zilikuwa kidogo ukilinganisha na mahitaji. Hadi kufikia mwezi Machi 2013 Wizara ilipata wastani wa asilimia 33 tu ya fedha zilizoidhinishwa kwa Matumizi ya Maendeleo. Hali hii imeathiri utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo. 

18.       Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo yake, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilipanga kutekeleza shughuli mbalimbali. Kwa upande wa Matumizi ya Kawaida, shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kulipa stahili mbalimbali za wanajeshi, vijana walioko katika mafunzo ya JKT na watumishi wa umma, kusafirisha wastaafu, kutoa huduma muhimu za chakula, tiba, sare na usafiri kwa wanajeshi na vijana  walioko  katika mafunzo  ya JKT. Wizara pia ilipanga kulipia huduma za umeme, maji, simu na mafuta kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu ya ulinzi, kuimarisha mafunzo ya kijeshi, kuendesha mafunzo ya ulinzi wa mgambo na kutengeneza magari na zana za kijeshi.

19.       Mheshimiwa Spika, kwa kutumia bajeti ya Maendeleo, Wizara ya Ulinzi iliweza kulipia mikataba ya ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi, kujenga maghala ya kuhifadhia silaha na ujenzi wa mahanga ya kuhifadhia zana. Shughuli nyingine ni pamoja na kumalizia ujenzi wa majengo mbalimbali, kukarabati miundombinu katika makambi, kurejesha mikopo ya mikataba ukiwemo wa NSSF, kulipia sehemu ya malipo ya awali ya mkopo kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za wanajeshi, kuboresha kiwanda cha Shirika la Mzinga, kukarabati mitambo na miundombinu kwa ajili ya kuboresha shughuli za utafiti katika Shirika la Nyumbu, kupima na kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya shughuli za Jeshi.

(i)                   Mafunzo na Mazoezi ya Kijeshi


20.           Mheshimiwa Spika, suala la kuwajengea weledi maafisa na askari wetu limeendelea kupewa uzito mkubwa. Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2012/2013 maafisa na askari wetu walishiriki katika mazoezi mbalimbali ya medani katika ngazi ya brigedi likiwemo zoezi kubwa la Ongeza Nguvu lililofanyika katika brigedi ya kusini mwezi Novemba, 2012. Wanajeshi wetu pia wameshiriki katika mazoezi ya pamoja chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Malengo ya mafunzo hayo ni kuwajengea wanajeshi uwezo wa kukabiliana na matishio mapya yakiwemo ugaidi, uharamia baharini, uhamiaji haramu na maafa. Vilevile maafisa na askari wamehudhuria kozi mbalimbali katika shule na vyuo ndani na nje ya nchi kikiwemo Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College) ambacho kimeanza kozi yake ya kwanza inayowahusisha Maafisa Wakuu kutoka Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Maafisa Waandamizi Serikalini. Kozi hiyo inayowashirikisha wanafunzi 20 ilianza rasmi tarehe 3 Septemba, 2012 na inatarajiwa kumalizika tarehe 20 Julai, 2013. Halikadhalika, wanajeshi wetu wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya zana mpya.

(ii)        Mafunzo ya Ulinzi wa Mgambo


21.       Mheshimiwa Spika, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutoa mafunzo ya ulinzi wa mgambo kama sehemu muhimu ya Jeshi la akiba.  Katika mwaka 2012 wanamgambo 11,482 walihitimu mafunzo hayo katika sehemu mbalimbali nchini.  Aidha, mafunzo ya Uongozi mdogo wa mgambo yaliendeshwa huko “Kunduchi Training Camp” (KTC), Dar es Salaam na wanafunzi 39 walihitimu mafunzo hayo.  Jeshi la Ulinzi pia limeendelea kutoa mafunzo ya ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kukabiliana na uhalifu nchini.

(iii) Huduma za Tiba na Madawa


22.       Mheshimiwa Spika, huduma za tiba na upatikanaji wa dawa kwa maafisa, askari, watumishi wa umma na wanajeshi wastaafu zimeendelea kutolewa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za Jeshi 70 zilizoko katika vikosi mbalimbali nchini.  Huduma hizo ambazo pia hutolewa kwa wananchi hususan wanaoishi katika maeneo jirani na vituo hivyo vya afya zimetolewa kwa kiwango cha kuridhisha.

(iv)       Uendeshaji wa Majukumu ya Ulinzi


23.       Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi imekuwa ikilipia gharama za shughuli mbalimbali zikiwemo doria za mipakani, operesheni za kijeshi na kufungua ‘detachment’. Vile vile Wizara yangu imelipia huduma muhimu zikiwemo mafuta, umeme, maji na simu.  Wizara pia imepata zana na vifaa vipya vya kijeshi yakiwemo magari ya huduma kwa wanajeshi. Hata hivyo, ununuzi wa zana na magari mapya umeongeza kiwango cha mahitaji ya mafuta ikilinganishwa na bajeti iliyotolewa. Kutokana na hali hiyo Wizara yangu imelazimika kulimbikiza madeni yenye thamani ya shilingi 35,496,809,000.00.

(v)        Ushirikiano wa Jeshi na Mamlaka za Kiraia


24.       Mheshimiwa Spika, moja ya jukumu la Jeshi la Wananchi wakati wa amani ni kushirikiana na Mamlaka za Kiraia kukabiliana na majanga au maafa pale yanapotokea. Katika kutekeleza jukumu hilo, Jeshi la Wananchi lilishiriki katika kutoa misaada katika maafa makubwa matatu: Ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skargate tarehe 18 Julai, 2012; ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 iliyotokea katika Jiji la Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2013.  Vile vile tarehe 1 Aprili, 2013 Jeshi lilishiriki katika kutoa msaada katika eneo la Moshono huko Arusha kufuatia maporomoko ya udongo katika machimbo ya moramu yaliyosababisha watu 13 kupoteza maisha yao. Katika kutekeleza jukumu hilo Jeshi letu lilishirikiana na mamlaka za kiraia katika shughuli za uokoaji wa majeruhi na uopoaji wa miili ya marehemu. Mbali na kushiriki katika kukabiliana na maafa, Jeshi pia limeshiriki katika zoezi la kusomba mahindi kutoka Laela kwenda Vwawa (Mbozi) tani 4,772, kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda tani 20,000 na kutoka Makambako kwenda Shinyanga tani 3,600. Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza maafisa, askari na watumishi wa umma wote walioshiriki katika kutoa msaada wakati wa maafa na kwenye operesheni ya kusomba mahindi.

25.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Jeshi la Wananchi, Jeshi la Kujenga Taifa na Mashirika yake yameshiriki katika shughuli mbalimbali za Kitaifa. Shughuli hizo ni pamoja na Maonesho ya Sabasaba, Nane nane, na Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, majeshi hayo yalitoa timu ambazo zilishiriki mashindano katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.

(vi)       Ujenzi wa Nyumba za Makazi na Maghala ya Kuhifadhia Zana na Silaha


26.       Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Jeshi la Wananchi limekuwa likikabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba kwa ajili ya maafisa na askari.  Hivi karibuni Serikali imepata mkopo wa ujenzi wa nyumba kutoka benki ya Exim ya China. Hivi sasa taratibu za kutekeleza mradi wa ujenzi zimekamilika.  Katika mradi huo tutaanza na ujenzi wa nyumba 6,064 katika awamu ya kwanza kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 300, ambapo Dola za Kimarekani milioni 285 ni mkopo kutoka Exim Bank ya China na Dola za Kimarekani milioni 15 zimetolewa na Serikali ya Tanzania. Wizara ya Ulinzi tayari imelipa Dola za Kimarekani milioni 5 za malipo ya awali zinazotakiwa kulipwa kwa mujibu wa mkataba. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2013. Mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya “Shanghai Construction (Group) General Company” kutoka China. Nyumba hizo zitajengwa katika vikosi 37 vilivyopo katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Pemba, Pwani na Tanga.  Ujenzi huu unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 50 hadi kumalizika kwake. Mazungumzo ya kupata fedha za ujenzi wa nyumba takribani 4,000 katika awamu ya pili yanaendelea. Vile vile awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha umeanza kutekelezwa. Ninatarajia kuwa Awamu ya pili ya ujenzi wa maghala hayo itaanza katika mwaka 2013/2014.

(vii)      Ununuzi wa Zana na Vifaa vya Kijeshi


27.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha Jeshi la Wananchi kwa kulinunulia zana na vifaa vya kisasa.  Nafurahi kuarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limeanza kupokea baadhi ya zana na vifaa hivyo. Tayari vifaa hivyo vimeshaanza kutumika katika shughuli za ulinzi na mafunzo. Hapana shaka hatua hii pia inatarajiwa kuongeza gharama za uendeshaji, utunzaji na matengenezo ya zana. Jeshi la Wananchi litajitahidi kuvitunza na kuvifanyia matengenezo vifaa na zana kwa wakati ili kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo yake.

(viii)         Ushirikiano wa Kiulinzi na Kijeshi na Nchi nyingine Duniani


28.       Mheshimiwa Spika, nchi yetu inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi na nchi mbalimbali duniani zikiwemo China, Ujerumani, India, Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu na Canada.  Kwa ujumla ushirikiano huo umekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi yetu. Kupitia ushirikiano huo, nchi hizi zimeendelea kutoa misaada mbalimbali kwa nchi yetu kama vile zana, mafunzo, wataalamu na vifaa vya hospitali.

29.       Mheshimiwa Spika, licha ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi baina ya nchi na nchi umekuwepo pia ushirikiano wa kikanda katika nyanja hizo.  Tanzania imeshirikiana na nchi nyingine katika Jumuiya za EAC na SADC.  Majeshi ya nchi hizi yamefanya mazoezi ya pamoja ambapo mwaka 2012 lilifanyika zoezi la Medani (Field Training Exercise – FTX 2012) lililoitwa “ZOEZI USHIRIKIANO IMARA 2012” huko Nyakinama, Rwanda. Vile vile majeshi hayo yanatarajia kushiriki katika zoezi la ‘Command Post Exercise – CPX’ litakalofanyika nchini Burundi mwaka huu 2013.

30.       Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa ikiimarisha ushirikiano wake na nchi za SADC. Kwa kipindi kirefu nchi yetu inatoa nafasi za mafunzo katika chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Arusha kwa nchi za Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe.  Aidha, katika kukabiliana na tishio la uharamia kwenye Bahari ya Hindi, Tanzania imesaini makubaliano ya kupambana na uharamia na nchi za Afrika Kusini na Msumbiji.  Tanzania pia ilikuwa ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya Wanamaji wa SADC (Standing Maritime Committee) ambapo kikao cha mwaka cha Kamati hiyo kilifanyika Tanzania kati ya tarehe 18 hadi 22 Februari, 2013. Katika kipindi hiki kumefanyika mikutano na vikao mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika Jumuiya za SADC. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeshiriki katika mikutano na vikao hivyo ili kujadili masuala ya ulinzi.

31.       Mheshimiwa Spika, kuhusu ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kimataifa, Jeshi la Wananchi limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa katika nchi zenye migogoro. Hadi sasa kuna jumla ya maafisa na askari 1,081 wa Jeshi la Wananchi wanaoshiriki operesheni hizo katika nchi za Lebanon na Darfur.

(ix)              Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Vijana


32.       Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lina uzoefu mkubwa katika kuwalea  vijana.  Mafunzo ya JKT yana manufaa makubwa kwa Taifa letu kwa sababu yanawaandaa vijana kuwa wazalendo, wenye maadili mema na moyo wa ujasiri.  Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Jeshi la Kujenga Taifa litafikisha miaka 50 ifikapo Julai mwaka huu tangu kuanzishwa kwake.  Tuna Viongozi wengi waliopata mafunzo haya ya JKT.  Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano ni mmoja wa Viongozi hao.  Hapana shaka mafunzo ya JKT yanamfanya kijana ajiamini, awe mvumilivu, mzalendo na jasiri katika kukabiliana na matatizo ya maisha.

33.       Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu huu wa JKT, uamuzi wa kusitisha mafunzo haya uliwanyima vijana fursa ya kupata malezi mema ya kuwajengea uzalendo na umoja. Ndio maana hivi sasa tunashuhudia mmong’onyoko wa maadili miongoni mwa vijana.  Kwa kutambua ukweli huu Serikali yenu imeamua kurudisha mafunzo haya.  Naupongeza uamuzi wa Serikali wa kurudisha mafunzo ya vijana wa JKT kwa Mujibu wa Sheria.

34.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Jeshi la Kujenga Taifa lilichukua idadi ya vijana wa kujitolea 12,620 katika makundi mawili. Kundi la kwanza la Operesheni Sensa lenye idadi ya vijana 5,898 (wavulana 4,576 na wasichana 1,322) liliandikishwa mwezi Agosti 2012. Vijana hao wamehitimu mafunzo yao ya awali na kwa sasa wapo katika makambi ya Burombola na Kanembwa (Kigoma), Chita (Morogoro), Mafinga (Iringa), Makutupora (Dodoma), Maramba na Mgambo (Tanga), Mgulani (Dar es Salaam), Mlale (Ruvuma), Msange (Tabora), Nachingwea (Lindi), Oljoro (Arusha) na Rwamkoma (Mara) wakiendelea na mafunzo ya stadi za kazi.  Kundi la pili la Operesheni Miaka 50 ya JKT lenye idadi ya vijana 6,722 (kati yao wavulana 5,227 na wasichana 1,495) limeanza mafunzo yake tarehe 04 Machi, 2013. Mafunzo hayo yanaendeshwa katika makambi ya Bulombora, Kanembwa, Maramba, Mgambo, Mlale, Msange, Ruvu na Rwamkoma. Mchanganuo wa vijana wa kujitolea walioandikishwa kwa mwaka 2012/2013 umeonyeshwa katika Kiambatisho Na. 4.

35.       Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2012/2013 niliahidi kwamba Wizara yangu itarejesha mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria kuanzia mwaka 2013. Nafurahi kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa ahadi hiyo imetekelezwa ambapo awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ya miezi mitatu ilianza tarehe 04 Machi, 2013 kwa kuchukua vijana 4,710. Mafunzo hayo yalizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 26 Machi, 2013 katika Kambi ya Ruvu. Vijana waliochukuliwa ni miongoni mwa vijana 41,348 waliohitimu mafunzo ya Kidato cha Sita katika mwaka 2013.  Aidha, vijana 36,638 waliobaki watachukuliwa katika mwaka 2013/2014 kwa awamu tatu (Angalia Kiambatisho Na. 5).  Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa miezi mitatu katika makambi ya Bulombora, Kanembwa, Maramba, Mgambo, Mlale, Msange, Ruvu na Rwamkoma. Utaratibu huu wa kuchukua vijana kwa Mujibu wa Sheria hautaathiri mafunzo ya vijana wanaotaka kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa utaratibu wa kujitolea. Jeshi la Kujenga Taifa litaendelea kuwachukua vijana wa kujitolea kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

36.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wanaoeleza kwamba muda wa miezi mitatu uliopangwa kwa Vijana wa Mujibu wa Sheria ni mfupi sana na kwa hiyo wanapendekeza muda huo uwe angalau miezi sita.  Napenda kuliarifu bunge lako Tukufu kwamba Serikali haina kipingamizi katika kutekeleza jambo hili ila tatizo kubwa linalotukabili katika kutekeleza dhamira hiyo ni ufinyu wa bajeti inayotolewa ukilinganisha na idadi ya wahitimu wa kidato cha sita.  Iwapo bajeti ya mafunzo haya itaongezeka basi taratibu za kuongeza muda zitafanywa ikizingatiwa kuwa JKT imeandaa Makambi yenye uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa mara moja.

37.       Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara yangu mwaka jana tulipokea ombi la Waheshimiwa Wabunge kuandaliwa mafunzo maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa.  Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi ombi hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalum ya wiki tatu kwa Waheshimiwa Wabunge.  Mafunzo hayo yalianza rasmi tarehe 04 Machi, 2013 na kufungwa tarehe 26 Machi, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Ufungaji huo wa mafunzo ya Waheshimiwa Wabunge ulikwenda sambamba na kuzinduliwa kwa mafunzo ya vijana kwa Mujibu wa Sheria. Wabunge 24 kati ya 47 waliojiandikisha kwa hiari yao walihudhuria mafunzo hayo.

38.       Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kati ya Waheshimiwa Wabunge 24 walioanza mafunzo yao ni Waheshimiwa Wabunge 22 ndiyo waliomaliza mafunzo yao.  Waheshimiwa Wabunge wawili walipatwa na maradhi. Kwa hiyo hawakumaliza mafunzo yao.

(x)               Shirika la Uzalishaji Mali la SUMAJKT


39.       Mheshimiwa Spika, mwaka 1982 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa amri ya kuundwa kwa Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) chini ya Sheria ya “The Corporation Sole Establishment Act” No. 23 of 1974.  Amri hiyo ilitolewa katika Tangazo la Serikali Namba 116 la mwaka 1982. Lengo la kuanzishwa kwa SUMAJKT ni kuwa na Shirika linalojiendesha kibiashara ili kupunguza utegemezi kwa Serikali katika kuendesha shughuli za JKT na hatimaye liweze kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla. Katika kutekeleza majukumu yake SUMAJKT linaendesha miradi mbali mbali ya shughuli za kilimo na ujenzi.

40.       Mheshimiwa Spika, hivi sasa shirika la SUMAJKT lina kampuni tanzu ya ujenzi ya “National Service Construction Department” inayofanya kazi kupitia kanda zake tano za ujenzi (Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza). Kanda hizi zinatekeleza majukumu yake baada ya kusajiliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi.

41.       Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza shughuli za kilimo SUMAJKT imepewa maagizo makuu mawili ambayo ni uzalishaji wa mbegu bora na mpango wa kujitosheleza kwa chakula katika Jeshi la Kujenga Taifa.

a.         Uzalishaji wa mbegu bora


42.       Mheshimiwa Spika, hivi sasa SUMAJKT inazalisha mbegu bora kwa kushirikiana na Makampuni ya Agricultural Seeds Agency, Tanseeds, Southern Highland Seed Growers na Sub Agro Ltd. Ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kuzalisha mbegu bora katika kiwango kinachotakiwa na kuweza kutekeleza agizo la Serikali kikamilifu linahitaji mtaji mkubwa kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa pembejeo, zana za kilimo (combine harvesters na tractors) na mtambo wa kusindika mbegu bora.

b.         Mpango wa kujitosheleza kwa chakula


43.       Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Taifa linategemea kuchukua vijana wasiopungua 41,000 kwa mujibu wa sheria na 10,000 wa kujitolea kwa kila mwaka. Ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kuwalisha vijana hawa kwa mwaka linahitaji unga wa mahindi tani 4480, mchele tani 5,039.82, maharage tani 1,119.96, ngano tani 5,000, mafuta ya kula tani 3,957.192, nyama tani 389,225, mboga mboga na viungo tani 320.13 na matunda tani 2,799.9. Jeshi la Kujenga Taifa limekusudia kutekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kukidhi mahitaji ya chakula kwa vijana na biashara.  Miradi hiyo ni kama ifuatavyo:-

(a)             Vikosi vya 842 KJ (Mlale), 835 (Mgambo) na 844 KJ (Itende) vimepewa jukumu la kuzalisha mahindi.

(b)            Kikosi cha 837 KJ (Chita) kimepewa jukumua la kuzalisha mpunga.

(c)             Vikosi vya 824 KJ (Kanembwa), 833 KJ (Oljoro) na Kambi ya Mtabila vimepewa jukumu la kuzalisha maharage.

(d)            Vikosi vya 823 KJ (Msange), 821 KJ (Bulombora), na 834 KJ (Makutupora) vimepewa jukumu la kuzalisha mawese, karanga na alizeti za kutosha ili kusindika mafuta.

(e)             JKT lina mpango wa kuboresha ufugaji ng’ombe wa nyama katika vikosi vya 833 KJ (Oljoro) na 841 KJ (Mafinga) na ufugaji kuku wa nyama na mayai huko 832 KJ (Ruvu) ili kuzalisha nyama na mayai ya kutosha.

(f)             Kikosi cha 832 KJ (Ruvu) na 834 KJ (Makutupora) vimepewa jukumu la kuzalisha aina mbalimbali za mboga na viungo.

(g)            Kikosi cha 835 KJ (Mgambo), Mtabila na 824 KJ (Kanembwa) vimepewa jukumu la kuzalisha matunda.

44.       Mheshimiwa Spika, hapana shaka utekelezaji wa miradi hii ya kilimo na ufugaji inahitaji mtaji mkubwa. Jeshi la Kujenga Taifa linahitaji shilingi 13,867,656,392 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu, madawa ya magugu na zana za kilimo ambapo uzalishaji wa mahindi utahitaji shilingi 2,630,550,000.00, mchele shilingi 1,989,500,000.00, maharage shilingi 863,190,000.00, mafuta ya kula shilingi 385,050,000.00, mboga na viungo shilingi 398,417,500.00 na ufugaji  shilingi 7,600,948,892.00.  Kwa kuwa SUMAJKT haiwezi kupata fedha hizi kwa kupitia bajeti, Wizara yangu imeagiza itafute wawekezaji kutoka ndani au nje watakaoweza kushirikiana nao katika shughuli za kilimo na ufugaji wa kisasa.  Hivi sasa tayari tumeshapata wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika kilimo cha kisasa.

45.       Mheshimiwa Spika, ili SUMAJKT iweze kuendesha shughuli zake kitaalamu inahitaji kuimarisha utendaji wake. Nimeuagiza Uongozi wa SUMAJKT kutafuta wataalamu wa masuala ya biashara, kilimo, ufugaji na ujenzi. Vile vile nimeliagiza Shirika hilo litafute mikopo yenye riba nafuu kutoka mabenki ili kuendesha miradi yake kwa uhakika.

c.      Mradi wa Matrekta


46.       Mheshimiwa Spika, wakati wa Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2012/2013 nililiarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kutekeleza kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, Serikali kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) lilipata mkopo kutoka Serikali ya India wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 40.  Kupitia mkopo huo, SUMAJKT waliingiza matrekta, zana na vifaa vya kilimo vyenye thamani ya shilingi 69,146,318,781.00.  Nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa, kufikia mwezi Septemba 2012 matrekta 1,833 yalikuwa yameuzwa, ambapo kati yake matrekta 275 yameuzwa kwa fedha taslimu shilingi 8,270,481,780.00.  Aidha, matrekta 1,558 na zana za kilimo zenye thamani ya shilingi 53,675,837,001.00 ziliuzwa kwa mkopo kwa wadau mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya, vikundi vya uzalishaji mali, SACCOs, na watu binafsi wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. 

47.       Mheshimiwa Spika, urejeshwaji wa mkopo unakwenda sambamba na mikataba iliyosainiwa.  Mpaka sasa jumla ya shilingi 14,575,490,929.00 zimerejeshwa.  Hata hivyo, Shirika bado lina zana za kilimo na vipuri vyenye thamani ya shilingi 7,200,000,000.00.  Miongoni mwa zana hizo ni pamoja na power tillers na pampu za umwagiliaji.  Kufuatia mafanikio ya mradi huo, tumepokea maombi mbalimbali kutoka kwa wananchi yanayofikia 4,000 ya kuuziwa matrekta.  Kati ya maombi hayo waombaji 73 wamekwisha toa fedha za utangulizi (deposit) kiasi cha shilingi 273,603,599.00. Kwa ujumla mradi wa matrekta umetekelezwa vizuri na mahitaji yameonekana kuwa makubwa.  Kutokana na mahitaji yaliyopo mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India kuhusu Awamu ya Pili ya mkopo wa matrekta wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 92 yanaendelea.

(xi)             Shughuli za Shirika la Mzinga


48.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Wizara ya Ulinzi na JKT imeendelea kuimarisha shirika la Mzinga. Shirika hili linaendelea na uzalishaji kufuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ukarabati wa kiwanda cha uzalishaji wa mazao ya kijeshi. Shirika linaendelea kufanya jitihada za kupata malighafi pamoja na kukuza ujuzi wa wafanyakazi wake ili kuongeza tija na ufanisi. Hata hivyo, utekelezaji wa malengo haya utategemea sana upatikanaji wa fedha.

49.       Mheshimiwa Spika, chini ya sheria ya Makampuni Sura 212 Shirika la Mzinga limeweza kuanzisha kampuni tanzu ya Mzinga Holdings ili kulipatia Shirika hilo mapato na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini. Hivi sasa Mzinga Holdings imefanikiwa kupata miradi midogo ya ujenzi wa majengo. Aidha, Wizara imeipa Mzinga Holdings jukumu la kuendesha maduka yasiyolipiwa kodi (Duty Free Shops) kwa ajili ya kuwahudumia wanajeshi na familia zao vikosini.  Mpaka sasa kampuni hiyo imeshafanya ukarabati wa majengo katika vikosi vya 24 KJ Kigoma na 23 KJ Biharamulo.  Duka la Kigoma tayari limeanza kutoa huduma kwa wanajeshi na lile la Biharamulo linatarajiwa kuanza kazi ifikapo mwezi Juni, 2013.

50.       Mheshimiwa Spika, Shirika la Mzinga Holdings pia lina mpango wa kuanzisha maduka yasiyolipiwa kodi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kagera, Mwanza na Shinyanga.  Hivi sasa Shirika hilo linaendelea na taratibu za kupata hati miliki za viwanja katika Mikoa hiyo.  Ili kutekeleza azma hii Shirika linahitaji shilingi bilioni 6.5. Kwa kuwa Shirika hili haliwezi kupata fedha zote kwa mara moja litatekeleza miradi hii kwa awamu kutokana na makusanyo ya fedha zitakazopatikana katika miradi mingine.

 

(xii)      Shughuli za Shirika la Nyumbu


51.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Shirika la Nyumbu, Shirika hili limekusudia kuimarisha shughuli za utafiti katika teknolojia ya mambo ya kijeshi. Shirika la Nyumbu limeweza kufanya utafiti katika teknolojia za magari, uhandisi na miundombinu ya majengo. Katika tafiti zake Shirika limekamilisha matengenezo ya gari la deraya (Personnel Armoured Vehicle) kwa ajili ya kutumika katika sekta ya ulinzi. Aidha, utafiti wa gari la nyumbu kwa ajili ya matumizi ya kijeshi umeendelea kuimarishwa. Vile vile Shirika la Nyumbu linaendelea na utafiti wa kuzalisha mtambo wa kuchuna mkonge ili kupata nyuzi na pampu za umwagiliaji. Aidha, utafiti kuhusiana na “engine” na “gearbox” kwa ajili ya matumizi kwenye matrekta madogo unaendelea vizuri.  Shughuli za uzalishaji wa vipuri vya mashine zinazotumika kwenye viwanda na mitambo pia unaendelea. 

 

(xiii)           Mtandao wa Mawasiliano

 Jeshini


52.       Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kuboresha Mtandao wa Mawasiliano Jeshini ili uweze kutoa huduma za mawasiliano bila ya kutegemea mitandao ya kibiashara ya simu. Kazi hii imegawika katika awamu mbili. Katika awamu ya kwanza mradi umekusudia kuboresha mawasiliano ya ndani ya vikosi. Katika awamu ya pili mradi una lengo la kuimarisha mawasiliano kati ya kikosi na kikosi kwa kutumia mfumo wa “satellite”. Sambamba na jitihada hizo, Wizara inatekeleza mradi wa mawasiliano salama utakaowezesha kuwepo mawasiliano ya kisasa baina ya vikosi vya Jeshi nchi nzima.  Utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Novemba, 2012 hadi sasa umefikia asilimia 30. Mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2013.

(xiv)           Upimaji na Ulipaji fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi


53.       Mheshimiwa Spika, Jeshi la Wananchi wa Tanzania lina mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makambi, makazi ya wanajeshi  na maghala ya kuhifadhia silaha.  Vile vile Jeshi linahitaji ardhi kwa ajili ya kuendeshea mafunzo na mazoezi ya kijeshi. Kutokana na mgongano kati ya mahitaji ya ardhi kwa Jeshi na Wananchi, Wizara yangu imekuwa ikikabiliwa na migogoro mingi.  Kwa kuwa maeneo mengi ya Jeshi hayajapimwa, wananchi hutumia fursa hiyo kuyavamia.  Hivi sasa kuna maeneo yapatayo 80 yenye migogoro katika mikoa mbalimbali. Kwa bahati mbaya upimaji wa maeneo ya Jeshi haufanyiki kwa kasi inayotakiwa kutokana na ufinyu wa bajeti.  Wizara yangu ina mpango wa kununua vifaa vya kisasa vya kupimia ardhi kwa matarajio kwamba kazi ya upimaji itafanywa kwa haraka zaidi na hatimaye kuepusha uvamizi wa maeneno ya Jeshi unaofanywa na wananchi.

54.       Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikichukua hatua kadhaa kutatua migogoro hiyo ikiwemo upimaji na ulipaji wa fidia ya ardhi zilizochukuliwa na Jeshi. Wizara imekamilisha kulipa fidia katika eneo la Kiharaka (Mapinga) mkoani Pwani. Aidha, katika mwaka huu wa fedha Wizara ina mpango wa kulipa fidia ya maeneo ya Mwakidila –Tanga, Cheyo – Tabora na Mwantini – Shinyanga. Wizara yangu itaendelea kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi mbalimbali kadri hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu.

(xv)      Mkakati wa Kupambana na UKIMWI


55.       Mheshimiwa Spika, Wizara ya ulinzi imeendelea kutekeleza mkakati wa kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga ili kuzuia maambukizi mapya.  Wizara imekuwa ikihimiza upimaji wa hiari kwa maafisa, askari na watumishi wa umma na vijana wa JKT kwa kutumia waelimishaji rika. Aidha, kwa wale ambao tayari wameshathibitika kuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI wamekuwa wakipatiwa dawa za kupunguza makali ya virusi (ARVs) bure katika vituo vya huduma na matibabu (care and treatment centres) vilivyoko katika hospitali kuu za kanda na huduma ya lishe katika maeneo ya kambi.

(xvi)         Hifadhi ya Mazingira



CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2012/2013


57.       Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa zinazoikabili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni mbili.  Kwanza ni kutokukidhi kwa ukamilifu mahitaji ya kutekeleza mipango yake ya kila mwaka ya kuendeleza Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa. Mahitaji ya mipango ya jeshi letu ni makubwa kama ilivyo kwa majeshi mengine duniani ikilinganishwa na uwezo mdogo wa Serikali. Athari za hali hiyo ni kuwepo kwa upungufu wa mahitaji muhimu ya kiulinzi, yakiwemo ya ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi, utoaji wa huduma kwa wanajeshi na ulipaji duni wa huduma muhimu za maji, umeme, mafuta na vilainisho.  Changamoto hii pia imesababisha Jeshi la Kujenga Taifa kufupisha muda wa uendeshaji wa mafunzo ya Mujibu wa Sheria kwa vijana waliomaliza kidato cha sita kutoka  miezi sita iliyokusudiwa awali na kuwa miezi mitatu.

58.       Mheshimiwa Spika, changamoto ya pili ni upatikanaji wa  fedha za maendeleo. Katika kipindi hiki fedha za maendeleo zilitolewa kwa kuchelewa na kwa kiwango pungufu.  Kielelezo cha hali hii ni, upokeaji wa  fedha hizi kwa  mwaka 2012/2013  ambapo hadi sasa mafungu yote matatu ya Wizara yamepokea jumla ya shilingi 135,700,000,000.00 sawa na asilimia 33.2 ya shilingi 408,189,566,000.00 zilizoidhinishwa. Hali hii imesababisha kulimbikiza madeni ya kimikataba na kuathiri miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo upimaji wa ardhi ya maeneo ya jeshi na kutokamilika kwa zoezi la kulipa fidia ya maeneo yaliyochukuliwa na jeshi. Kwa ujumla changamoto hizi ambazo zimeendelea kwa muda mrefu sasa zimekuwa kikwazo cha utekelezaji wa majukumu ya Ulinzi na JKT.


MPANGO WA MWAKA 2013/2014


59.       Mheshimiwa Spika, mpango wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2013/2014 unakusudia kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa Jeshi katika kutekeleza majukumu yake kulingana na Dira na Dhima ya Wizara. Vile vile Wizara inakusudia kukamilisha miradi ambayo haijamalizika pamoja na kulipa madeni ya ununuzi wa vifaa. Kwa hivyo, Wizara yangu itakuwa na jukumu la kutekeleza shughuli zifuatazo:-

(i)                       Kupunguza tatizo la wanajeshi kuishi uraiani kwa kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 6064, kukarabati na kuimarisha miradi ya ujenzi inayoendelea.

(ii)                     Kulipatia Jeshi zana na vifaa vya kijeshi ikiwemo vifaa vya uhandisi wa medani, ndege vita na magari.

(iii)                   Kukarabati mitambo na miundombinu katika Mashirika ya Mzinga na Nyumbu ili kuimarisha shughuli za viwanda na kuendeleza teknolojia ya masuala ya kijeshi.
(iv)                   Kuboresha mawasiliano ya simu ndani ya Jeshi baina ya vikosi na kwenye makambi ya jeshi.

(v)                     Kulipa mikopo ya Mfuko wa NSSF.

(vi)                   Kupima na kulipa fidia ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi.

(vii)                 Kujenga maghala ya kuhifadhia silaha na zana za kijeshi.

(viii)               Kulipia gharama za matumizi ya huduma za umeme, maji na simu kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu ya kimsingi zikiwemo operesheni za kiulinzi na mafunzo.

(ix)                   Kulipia stahili mbalimbali za Maafisa, Askari, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na Watumishi wa Umma ikiwemo mishahara, posho za chakula kwa ajili ya wanajeshi, matibabu, likizo, maziko na mafunzo.

(x)               Kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.


MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014


i.                    Makadirio ya Mapato


60.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/2014 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekadiria kukusanya mapato kiasi cha Shilingi 68,206,000.00 katika mchanganuo ufuatao:- 

a.       Fungu 38 NGOME
Shilingi     1,501,000.00
b.      Fungu 39 JKT                              
Shilingi   46,703,000.00


c.       Fungu 57 WIZARAYA ULINZI                                    Shilingi 20,002,000.00

Jumla Shilingi   68,206,000.00

ii.                  Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo


61.       Mheshimwa Spika, ili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iweze kutekeleza majukumu yake katika Mwaka 2013/2014 inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,102,999,529,000.00 ambazo kati yake Shilingi 857,417,502,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida  na Shilingi 245,582,027,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Mchanganuo wa bajeti hiyo kwa kuzingatia mafungu ya Wizara ni kama ufuatao:-




FUNGU 38 NGOME

Matumizi ya Kawaida
 Sh.651,015,373,000.00 
Matumizi ya Maendeleo  
Sh.  10,000,000,000.00

Jumla ya Makadirio kwa Fungu 38           
Sh. 661,015,373,000.00

FUNGU 39 JKT

Matumizi ya Kawaida                                    
Sh 187,301,634,000.00
Matumizi ya Maendeleo
Sh.    6,000,000,000.00

Jumla ya makadirio kwa Fungu 39            
Sh. 193,301,634,000.00




FUNGU 57 WIZARA YA ULINZI

Matumizi ya Kawaida                        
Sh.    19,100,495,000.00
Matumizi ya Maendeleo                    
Sh.  229,582,027,000.00

Jumla ya Makadirio kwa Fungu 57
Sh.  248,682,522,000.00

MWISHO


62.       Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara (www.modans.go.tz).  Naomba kutoa Hoja.

3 comments:

Anonymous said...

Hey there! Do you know iif they make any plugins to safeguard agaist hackers?
I'm kinda paranoid about losing everything I've worked hard on.
Anny suggestions?

Anonymous said...

Hi, I log on to your blog like every week. Your writing styoe iis awesome, keep it
up!

Anonymous said...

Thank you, I've just been looking for info approximately
this subject for a while and yours is the best I've
discovered so far. But, what concerning the conclusion? Are you positive about thee source?