HOTUBA YA WAZIRI WA
ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA MHESHIMIWA SHAMSI VUAI
NAHODHA (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA
2013/2014
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa
iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili
na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
2. Mheshimiwa Spika, kwanza napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba
yangu ya bajeti kwa mwaka 2013/2014 mbele ya Bunge lako Tukufu. Pili, nawashukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi
Mkuu na Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais kwa kuendelea
kuniamini kuiongoza Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa. Namshukuru pia
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa
maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.
Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla kwamba
nitaendelea kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa uadilifu na uaminifu
mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kuchukua nafasi hii
kuwapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Anna Margareth Abdallah (Mb.) na Makamu
Mwenyekiti, Mhe. Mohammed Seif Khatib (Mb.) kwa kuchaguliwa kuiongoza Kamati
hiyo. Halikadhalika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuwa
wajumbe wa Kamati hiyo. Ninawaomba
wajumbe hao wapokee shukurani zangu kwa maoni waliyotupatia wakati wa kuchambua
mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2013/2014.
Maoni na mapendekezo yao yametusaidia sana katika kuiandaa hotuba hii.
4. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 28
Machi, 2013 Mbunge mwenzetu Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Jimbo la
Chambani alifariki dunia katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu
kutoa pole kwako Mheshimiwa Spika, familia, ndugu na marafiki kwa msiba
huo. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho
ya Marehemu Peponi. Amina.
DIRA NA DHIMA YA WIZARA YA ULINZI NA JKT
5. Mheshimiwa Spika, Dira ya
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwa Taasisi iliyotukuka ya
kudumisha amani na usalama nchini. Kwa kuzingatia kwamba ulinzi wa Taifa ndilo
jukumu la kwanza kwa Serikali, dhima
ya Wizara hii ni kuilinda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya
maadui kutoka nje au ndani ya nchi na kuhakikisha kuwa uhuru na maslahi ya
Taifa letu (national interests) yanakuwa salama wakati wote. Nafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu inaendelea kutekeleza jukumu hili
kwa ufanisi. Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 Sura 192 na
Sheria ya JKT ya mwaka 1963 Sura 193, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa imekabidhiwa jukumu la kusimamia Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la
Kujenga Taifa katika kutekeleza majukumu yake. Vile vile Wizara yangu ina
wajibu wa kuvipatia vyombo hivi mahitaji yake ya kimsingi ili kuviwezesha
kutekeleza majukumu hayo.
MAJUKUMU YA WIZARA YA ULINZI NA JKT
6. Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966, Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ina
majukumu saba. Kwanza, Wizara ina jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu. Pili,
Wizara ya Ulinzi inasaidiana na Mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga
ili kuwapatia wananchi waliofikwa na majanga misaada ya kibinadamu. Tatu, Wizara
inashiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi zenye migogoro
duniani. Nne, Wizara hii inaandaa umma wa Watanzania
kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Taifa. Tano, Wizara inawajengea vijana
wa Kitanzania moyo wa uzalendo na mshikamano wa kitaifa ili kuwaandaa
kikamilifu katika kutekeleza shughuli za kujitegemea. Sita, Wizara ya Ulinzi
inafanya utafiti ili kuendeleza teknolojia kuhusu matumizi ya kijeshi na
kiraia. Saba, Wizara hii inaimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani
katika masuala ya Kijeshi.
MALENGO YA WIZARA YA ULINZI NA JKT
7. Mheshimiwa
Spika, katika kutekeleza majukumu niliyoyataja hapo awali, Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imejiwekea malengo makuu manane kwa mwaka
2013/2014. Kwanza, kuandikisha wanajeshi
wapya kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Pili, kuwaendeleza kielimu maafisa na
askari wa JWTZ na JKT. Tatu, kununua na
kulipatia Jeshi zana bora kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa. Nne, kutunza na
kuhifadhi vizuri zana za kijeshi na kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi na
makazi kwa wanajeshi. Tano, kuimarisha mahusiano mema na nchi nyingine duniani
katika masuala ya kijeshi. Sita, kutoa mafunzo ya ulinzi wa mgambo kwa
Watanzania ili kuimarisha Jeshi la Akiba. Saba, kuwapatia vijana wa Kitanzania
mafunzo ya kuwajengea nidhamu, ukakamavu na moyo wa uzalendo. Nane, kuyajengea
mashirika ya Mzinga, Nyumbu na SUMAJKT mazingira bora ya kukuza teknolojia ili
yaweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa ruzuku ya Serikali.
UTEKELEZAJI WA MAONI NA USHAURI WA KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA
8. Mheshimiwa Spika,
wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa
mwaka 2012/2013, tulipokea maoni, ushauri na maelekezo kutoka kwa iliyokuwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Napenda
kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa
yamefanyiwa kazi na majibu yake yameainishwa katika Kiambatisho Na.1. Halikadhalika, hoja mbalimbali zilizotolewa na
Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huo pia zimezingatiwa katika mpango na
bajeti ya mwaka 2013/2014 ninayowasilisha leo hapa Bungeni.
HALI YA USALAMA WA MIPAKA KATIKA MWAKA 2012/2013
9. Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa jukumu kubwa la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kulinda
uhuru na usalama wa nchi yetu naomba nieleze hali ya usalama wa mipaka yetu na
nchi nyingine ilivyokuwa katika mwaka 2012/2013. Hali ya usalama wa mipaka yetu
na nchi jirani, nchi kavu na baharini ni shwari kwa ujumla. Hata hivyo katika baadhi ya mipaka yetu na
nchi za Uganda, Kenya na Zambia kuna tatizo la muda mrefu la kung’olewa kwa
alama za mipakani yaani “beacons”. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa zinaendelea kulifanyia kazi suala hili ili kuzirudisha alama hizo
kwenye eneo la mpaka.
(i) Mpaka katika Bahari ya Hindi
10. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama
katika eneo la mpaka wa Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilomita 1,424 ambako
nchi yetu inapakana na Kenya, Visiwa vya Ushelisheli, Komoro na Msumbiji
inaendelea kuwa shwari. Hivi sasa matukio ya uharamia yaliyokuwa yakitokea
miaka mitatu iliyopita yamepungua kwa kiasi kikubwa. Katika kipindi cha kuanzia
mwezi Julai 2012 hadi sasa hakujatokea tukio lolote la uharamia katika eneo
hili. Mafanikio haya yanatokana na doria zinazofanywa na Jeshi la Wananchi
kupitia Kamandi yake ya Wanamaji pamoja na ulinzi unaofanywa na majeshi ya
Ulaya, Asia na Marekani katika eneo la Ghuba ya Aden.
(ii) Mpaka wa Kaskazini
11. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika mpaka huu wenye urefu
wa kilometa 1,190 ambako Tanzania inapakana na Kenya na Uganda inaendelea kuwa
shwari. Hata hivyo kumejitokeza tatizo la wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na
Somalia wanaoingia nchini kwa kupitia kwenye mpaka wetu na nchi jirani. Wizara
yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zimekuwa zikiwasaka
wahamiaji haramu pamoja na kuwatafuta mawakala wa biashara hiyo ili
kuwachukulia hatua za kisheria.
(iii) Mpaka wa Magharibi
12. Mheshimiwa Spika, hali ya
usalama katika mpaka huu wenye urefu wa kilomita 1,220 ambako Tanzania
inapakana na Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni shwari.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kudumisha ulinzi katika Ukanda wa
Ziwa Tanganyika. Ili kuimarisha ulinzi wa eneo hilo Jeshi la Wananchi wa
Tanzania linatarajia kupata boti 2 za kisasa mwishoni mwa mwaka huu ambazo
zitatumika kufanyia doria katika Ziwa Tanganyika.
(iv) Mpaka wa Kusini
13. Mheshimiwa Spika, katika mpaka wa
Kusini Tanzania inapakana na Msumbiji, Malawi na Zambia. Hali ya usalama katika
mpaka wetu wa kusini wenye urefu wa kilomita 759 zikiwemo kilomita 248 za maji kwenye Ziwa Nyasa ni
shwari. Kuhusu mgogoro wa mpaka katika
Ziwa Nyasa kati ya Malawi na Tanzania mazungumzo bado yanaendelea. Mazungumzo haya yanaratibiwa na Wizara yetu
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
14. Mheshimiwa Spika, pamoja na
changamoto mbalimbali nilizozieleza, napenda kuwahakikishia wananchi wote wa
Tanzania kwa ujumla kwamba ulinzi wa mipaka yetu ni imara. Jeshi letu liko
makini na linaendelea kuchukua tahadhari kwa kuimarisha vikosi vyake ili
kudumisha ulinzi na usalama wa nchi yetu.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2012/2013
15. Mheshimiwa
Spika, naomba sasa nitoe taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka
2012/2013. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikadiria kukusanya
mapato ya jumla ya Shilingi
57,650,000.00 kutoka katika Mafungu yake matatu (yaani Fungu 38 – NGOME,
Fungu 39 – JKT na Fungu 57 – Wizara ya Ulinzi). Hadi kufikia mwezi Machi, 2013
Mafungu hayo matatu yalikusanya mapato ya jumla ya Shilingi 27,584,536.00 sawa na asilimia 47.8 ya makadirio (Angalia Kiambatisho Na.2).
16. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu bajeti ya shilingi 1,086,550,058,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na
Maendeleo katika Mafungu yake matatu. Kati ya fedha hizo, shilingi 678,363,492,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 408,186,566,000.00 ni kwa
ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi 2013, Wizara ilikuwa
imepokea jumla ya shilingi
718,855,852,627.00 sawa na asilimia
66 ya bajeti yake. Kati ya fedha hizo shilingi
583,155,852,627.00 zilikuwa ni kwa Matumizi ya Kawaida. Kwa upande wa
Matumizi ya Maendeleo, fedha zilizopokelewa ni Shilingi 135,700,000,000.00 sawa na asilimia 33 ya fedha
zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Mchanganuo wa Matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa Mafungu yote
matatu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi mwezi Machi, 2013 umeonyeshwa katika Kiambatisho Na. 3.
17. Mheshimiwa Spika, tathmini ya fedha zilizopokelewa inaonesha
kwamba mwenendo wa upatikanaji wa
fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida hadi mwezi Machi 2013 kwa ujumla ulikuwa
ni wa kuridhisha. Fedha kwa ajili ya
mishahara na marupurupu zilipokelewa kulingana na makisio ya bajeti. Hata
hivyo, fedha zilizotolewa kwa ajili ya shughuli
za Maendeleo zilikuwa kidogo ukilinganisha na mahitaji. Hadi kufikia
mwezi Machi 2013 Wizara ilipata wastani wa asilimia 33 tu ya fedha
zilizoidhinishwa kwa Matumizi ya Maendeleo. Hali hii imeathiri utekelezaji wa
miradi mbali mbali ya maendeleo.
18. Mheshimiwa
Spika, ili kufikia malengo yake, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa ilipanga kutekeleza shughuli mbalimbali. Kwa upande wa Matumizi ya
Kawaida, shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kulipa stahili mbalimbali za
wanajeshi, vijana walioko katika mafunzo ya JKT na watumishi wa umma,
kusafirisha wastaafu, kutoa huduma muhimu za chakula, tiba, sare na usafiri kwa
wanajeshi na vijana walioko katika mafunzo ya JKT. Wizara pia ilipanga kulipia huduma za
umeme, maji, simu na mafuta kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu ya ulinzi,
kuimarisha mafunzo ya kijeshi, kuendesha mafunzo ya ulinzi wa mgambo na
kutengeneza magari na zana za kijeshi.
19. Mheshimiwa
Spika, kwa kutumia bajeti ya Maendeleo, Wizara ya Ulinzi iliweza
kulipia mikataba ya ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi, kujenga maghala ya
kuhifadhia silaha na ujenzi wa mahanga ya kuhifadhia zana. Shughuli nyingine ni
pamoja na kumalizia ujenzi wa majengo mbalimbali, kukarabati miundombinu katika
makambi, kurejesha mikopo ya mikataba ukiwemo wa NSSF, kulipia sehemu ya malipo
ya awali ya mkopo kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za
wanajeshi, kuboresha kiwanda cha Shirika la Mzinga, kukarabati mitambo na
miundombinu kwa ajili ya kuboresha shughuli za utafiti katika Shirika la
Nyumbu, kupima na kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa
ajili ya shughuli za Jeshi.
(i) Mafunzo na Mazoezi ya Kijeshi
20. Mheshimiwa Spika, suala la
kuwajengea weledi maafisa na askari wetu limeendelea kupewa uzito mkubwa. Katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2012/2013 maafisa na askari wetu
walishiriki katika mazoezi mbalimbali ya medani katika ngazi ya brigedi
likiwemo zoezi kubwa la Ongeza Nguvu lililofanyika katika brigedi ya
kusini mwezi Novemba, 2012. Wanajeshi wetu pia wameshiriki katika mazoezi ya
pamoja chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Malengo ya mafunzo hayo ni
kuwajengea wanajeshi uwezo wa kukabiliana na matishio mapya yakiwemo ugaidi,
uharamia baharini, uhamiaji haramu na maafa. Vilevile maafisa na askari
wamehudhuria kozi mbalimbali katika shule na vyuo ndani na nje ya nchi kikiwemo
Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National
Defence College) ambacho kimeanza kozi yake ya kwanza inayowahusisha
Maafisa Wakuu kutoka Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Maafisa Waandamizi
Serikalini. Kozi hiyo inayowashirikisha wanafunzi 20 ilianza rasmi tarehe 3
Septemba, 2012 na inatarajiwa kumalizika tarehe 20 Julai, 2013. Halikadhalika,
wanajeshi wetu wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya zana mpya.
(ii) Mafunzo ya Ulinzi wa Mgambo
21. Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutoa mafunzo ya ulinzi wa mgambo
kama sehemu muhimu ya Jeshi la akiba.
Katika mwaka 2012 wanamgambo 11,482 walihitimu mafunzo hayo katika
sehemu mbalimbali nchini. Aidha, mafunzo
ya Uongozi mdogo wa mgambo yaliendeshwa huko “Kunduchi Training Camp” (KTC),
Dar es Salaam na wanafunzi 39 walihitimu mafunzo hayo. Jeshi la Ulinzi pia limeendelea kutoa mafunzo
ya ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili
kukabiliana na uhalifu nchini.
(iii) Huduma za Tiba na Madawa
22. Mheshimiwa Spika, huduma za tiba na upatikanaji wa dawa kwa
maafisa, askari, watumishi wa umma na wanajeshi wastaafu zimeendelea kutolewa
katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za Jeshi 70 zilizoko katika vikosi
mbalimbali nchini. Huduma hizo ambazo
pia hutolewa kwa wananchi hususan wanaoishi katika maeneo jirani na vituo hivyo
vya afya zimetolewa kwa kiwango cha kuridhisha.
(iv) Uendeshaji wa Majukumu ya Ulinzi
23. Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Ulinzi imekuwa ikilipia gharama za shughuli mbalimbali
zikiwemo doria za mipakani, operesheni za kijeshi na kufungua ‘detachment’.
Vile vile Wizara yangu imelipia huduma muhimu zikiwemo mafuta, umeme, maji na
simu. Wizara pia imepata zana na vifaa
vipya vya kijeshi yakiwemo magari ya huduma kwa wanajeshi. Hata hivyo, ununuzi
wa zana na magari mapya umeongeza kiwango cha mahitaji ya mafuta ikilinganishwa
na bajeti iliyotolewa. Kutokana na hali hiyo Wizara yangu imelazimika
kulimbikiza madeni yenye thamani ya shilingi 35,496,809,000.00.
(v) Ushirikiano wa Jeshi na Mamlaka za Kiraia
24. Mheshimiwa Spika, moja
ya jukumu la Jeshi la Wananchi wakati wa amani ni kushirikiana na Mamlaka za
Kiraia kukabiliana na majanga au maafa pale yanapotokea. Katika kutekeleza
jukumu hilo, Jeshi la Wananchi lilishiriki katika kutoa misaada katika maafa
makubwa matatu: Ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skargate tarehe 18 Julai, 2012;
ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 iliyotokea katika Jiji la Dar es
Salaam tarehe 29 Machi, 2013. Vile vile
tarehe 1 Aprili, 2013 Jeshi lilishiriki katika kutoa msaada katika eneo la
Moshono huko Arusha kufuatia maporomoko ya udongo katika machimbo ya moramu
yaliyosababisha watu 13 kupoteza maisha yao. Katika kutekeleza jukumu hilo
Jeshi letu lilishirikiana na mamlaka za kiraia katika shughuli za uokoaji wa
majeruhi na uopoaji wa miili ya marehemu. Mbali na kushiriki katika kukabiliana
na maafa, Jeshi pia limeshiriki katika zoezi la kusomba mahindi kutoka Laela
kwenda Vwawa (Mbozi) tani 4,772, kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda tani 20,000 na
kutoka Makambako kwenda Shinyanga tani 3,600. Napenda kuchukua fursa hii
kuwapongeza maafisa, askari na watumishi wa umma wote walioshiriki katika kutoa
msaada wakati wa maafa na kwenye operesheni ya kusomba mahindi.
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Jeshi la Wananchi,
Jeshi la Kujenga Taifa na Mashirika yake yameshiriki katika shughuli mbalimbali
za Kitaifa. Shughuli hizo ni pamoja na Maonesho ya Sabasaba, Nane nane, na
Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, majeshi hayo yalitoa timu ambazo zilishiriki
mashindano katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
(vi) Ujenzi wa Nyumba za Makazi na Maghala ya Kuhifadhia Zana na Silaha
26. Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu Jeshi la Wananchi limekuwa likikabiliwa na uhaba mkubwa wa nyumba
kwa ajili ya maafisa na askari. Hivi
karibuni Serikali imepata mkopo wa ujenzi wa nyumba kutoka benki ya Exim ya
China. Hivi sasa taratibu za kutekeleza mradi wa ujenzi zimekamilika. Katika mradi huo tutaanza na ujenzi wa nyumba
6,064 katika awamu ya kwanza kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 300,
ambapo Dola za Kimarekani milioni 285 ni mkopo kutoka Exim Bank ya China na
Dola za Kimarekani milioni 15 zimetolewa na Serikali ya Tanzania. Wizara ya
Ulinzi tayari imelipa Dola za Kimarekani milioni 5 za malipo ya awali
zinazotakiwa kulipwa kwa mujibu wa mkataba. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa
kuanza mwezi Mei, 2013. Mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya “Shanghai
Construction (Group) General Company” kutoka China. Nyumba hizo zitajengwa
katika vikosi 37 vilivyopo katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma,
Kagera, Kigoma, Morogoro, Pemba, Pwani na Tanga. Ujenzi huu unatarajiwa kuchukua muda wa miezi
50 hadi kumalizika kwake. Mazungumzo ya kupata fedha za ujenzi wa nyumba
takribani 4,000 katika awamu ya pili yanaendelea. Vile vile awamu ya kwanza ya
mradi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha umeanza kutekelezwa. Ninatarajia
kuwa Awamu ya pili ya ujenzi wa maghala hayo itaanza katika mwaka 2013/2014.
(vii) Ununuzi wa Zana na Vifaa vya Kijeshi
27. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kutekeleza mkakati
wa kuimarisha Jeshi la Wananchi kwa kulinunulia zana na vifaa vya kisasa. Nafurahi
kuarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limeanza kupokea baadhi ya zana na vifaa
hivyo. Tayari vifaa hivyo vimeshaanza kutumika katika shughuli za ulinzi na
mafunzo. Hapana shaka hatua hii pia inatarajiwa kuongeza gharama za uendeshaji,
utunzaji na matengenezo ya zana. Jeshi la Wananchi litajitahidi kuvitunza na
kuvifanyia matengenezo vifaa na zana kwa wakati ili kupunguza gharama za
uendeshaji na matengenezo yake.
(viii) Ushirikiano wa Kiulinzi na Kijeshi na Nchi nyingine Duniani
28. Mheshimiwa Spika,
nchi yetu inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi na nchi
mbalimbali duniani zikiwemo China, Ujerumani, India, Marekani, Umoja wa Falme
za Kiarabu na Canada. Kwa ujumla ushirikiano
huo umekuwa wa manufaa makubwa kwa nchi yetu. Kupitia ushirikiano huo, nchi
hizi zimeendelea kutoa misaada mbalimbali kwa nchi yetu kama vile zana,
mafunzo, wataalamu na vifaa vya hospitali.
29. Mheshimiwa Spika, licha ya
ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi baina ya nchi na nchi umekuwepo pia
ushirikiano wa kikanda katika nyanja hizo. Tanzania imeshirikiana na nchi nyingine katika
Jumuiya za EAC na SADC. Majeshi ya nchi
hizi yamefanya mazoezi ya pamoja ambapo mwaka 2012 lilifanyika zoezi la Medani
(Field Training Exercise – FTX 2012)
lililoitwa “ZOEZI USHIRIKIANO IMARA 2012” huko Nyakinama, Rwanda. Vile vile
majeshi hayo yanatarajia kushiriki katika zoezi la ‘Command Post Exercise – CPX’ litakalofanyika nchini Burundi mwaka
huu 2013.
30. Mheshimiwa Spika, Tanzania
imekuwa ikiimarisha ushirikiano wake na nchi za SADC. Kwa kipindi kirefu nchi
yetu inatoa nafasi za mafunzo katika chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Arusha kwa
nchi za Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe. Aidha, katika kukabiliana na tishio la
uharamia kwenye Bahari ya Hindi, Tanzania imesaini makubaliano ya kupambana na
uharamia na nchi za Afrika Kusini na Msumbiji.
Tanzania pia ilikuwa ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya
Wanamaji wa SADC (Standing Maritime
Committee) ambapo kikao cha mwaka cha Kamati hiyo kilifanyika Tanzania kati
ya tarehe 18 hadi 22 Februari, 2013. Katika kipindi hiki
kumefanyika mikutano na vikao mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa
kikanda katika Jumuiya za SADC. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
imeshiriki katika mikutano na vikao hivyo ili kujadili masuala ya ulinzi.
31. Mheshimiwa Spika,
kuhusu ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kimataifa, Jeshi la Wananchi
limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na
Umoja wa Mataifa katika nchi zenye migogoro. Hadi sasa kuna jumla ya maafisa na
askari 1,081 wa Jeshi la Wananchi wanaoshiriki operesheni hizo katika nchi za
Lebanon na Darfur.
(ix) Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Vijana
32. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga
Taifa lina uzoefu mkubwa katika kuwalea
vijana. Mafunzo ya JKT yana
manufaa makubwa kwa Taifa letu kwa sababu yanawaandaa vijana kuwa wazalendo,
wenye maadili mema na moyo wa ujasiri.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Jeshi la Kujenga Taifa litafikisha miaka 50
ifikapo Julai mwaka huu tangu kuanzishwa kwake.
Tuna Viongozi wengi waliopata mafunzo haya ya JKT. Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano ni mmoja wa Viongozi hao. Hapana
shaka mafunzo ya JKT yanamfanya kijana ajiamini, awe mvumilivu, mzalendo na
jasiri katika kukabiliana na matatizo ya maisha.
33. Mheshimiwa Spika, kutokana na
umuhimu huu wa JKT, uamuzi wa kusitisha mafunzo haya uliwanyima vijana fursa ya
kupata malezi mema ya kuwajengea uzalendo na umoja. Ndio maana hivi sasa
tunashuhudia mmong’onyoko wa maadili miongoni mwa vijana. Kwa kutambua ukweli huu Serikali yenu imeamua
kurudisha mafunzo haya. Naupongeza
uamuzi wa Serikali wa kurudisha mafunzo ya vijana wa JKT kwa Mujibu wa Sheria.
34. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013 Jeshi la Kujenga Taifa lilichukua idadi ya vijana wa kujitolea
12,620 katika makundi mawili. Kundi la kwanza la Operesheni Sensa lenye idadi ya vijana 5,898 (wavulana 4,576 na
wasichana 1,322) liliandikishwa mwezi Agosti 2012. Vijana hao wamehitimu
mafunzo yao ya awali na kwa sasa wapo katika makambi ya Burombola na Kanembwa
(Kigoma), Chita (Morogoro), Mafinga (Iringa), Makutupora (Dodoma), Maramba na
Mgambo (Tanga), Mgulani (Dar es Salaam), Mlale (Ruvuma), Msange (Tabora),
Nachingwea (Lindi), Oljoro (Arusha) na Rwamkoma (Mara) wakiendelea na mafunzo
ya stadi za kazi. Kundi la pili la Operesheni Miaka 50 ya JKT lenye idadi
ya vijana 6,722 (kati yao wavulana 5,227 na wasichana 1,495) limeanza mafunzo
yake tarehe 04 Machi, 2013. Mafunzo hayo yanaendeshwa katika makambi ya
Bulombora, Kanembwa, Maramba, Mgambo, Mlale, Msange, Ruvu na Rwamkoma.
Mchanganuo wa vijana wa kujitolea walioandikishwa kwa mwaka 2012/2013
umeonyeshwa katika Kiambatisho Na. 4.
35. Mheshimiwa Spika, katika
Hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2012/2013 niliahidi kwamba Wizara yangu
itarejesha mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria kuanzia mwaka 2013. Nafurahi
kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa ahadi hiyo imetekelezwa ambapo awamu ya
kwanza ya mafunzo hayo ya miezi mitatu ilianza tarehe 04 Machi, 2013 kwa
kuchukua vijana 4,710. Mafunzo hayo yalizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete tarehe
26 Machi, 2013 katika Kambi ya Ruvu. Vijana waliochukuliwa ni miongoni mwa
vijana 41,348 waliohitimu mafunzo ya Kidato cha Sita katika mwaka 2013. Aidha, vijana 36,638 waliobaki watachukuliwa
katika mwaka 2013/2014 kwa awamu tatu (Angalia
Kiambatisho Na. 5). Mafunzo hayo
yatafanyika kwa muda wa miezi mitatu katika makambi ya Bulombora, Kanembwa,
Maramba, Mgambo, Mlale, Msange, Ruvu na Rwamkoma. Utaratibu huu wa kuchukua
vijana kwa Mujibu wa Sheria hautaathiri mafunzo ya vijana wanaotaka kujiunga na
Jeshi la Kujenga Taifa kwa utaratibu wa kujitolea. Jeshi la Kujenga Taifa
litaendelea kuwachukua vijana wa kujitolea kutoka maeneo mbalimbali ya nchi
yetu.
36. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imepokea maoni kutoka kwa wadau
mbalimbali wanaoeleza kwamba muda wa miezi mitatu uliopangwa kwa Vijana wa
Mujibu wa Sheria ni mfupi sana na kwa hiyo wanapendekeza muda huo uwe angalau
miezi sita. Napenda kuliarifu bunge lako
Tukufu kwamba Serikali haina kipingamizi katika kutekeleza jambo hili ila
tatizo kubwa linalotukabili katika kutekeleza dhamira hiyo ni ufinyu wa bajeti
inayotolewa ukilinganisha na idadi ya wahitimu wa kidato cha sita. Iwapo bajeti ya mafunzo haya itaongezeka basi
taratibu za kuongeza muda zitafanywa ikizingatiwa kuwa JKT imeandaa Makambi
yenye uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa mara moja.
37. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara
yangu mwaka jana tulipokea ombi la Waheshimiwa Wabunge kuandaliwa mafunzo
maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi
ombi hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalum ya wiki tatu kwa Waheshimiwa
Wabunge. Mafunzo hayo yalianza rasmi
tarehe 04 Machi, 2013 na kufungwa tarehe 26 Machi, 2013 na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Ufungaji huo wa mafunzo ya Waheshimiwa
Wabunge ulikwenda sambamba na kuzinduliwa kwa mafunzo ya vijana kwa Mujibu wa
Sheria. Wabunge 24 kati ya 47 waliojiandikisha kwa hiari yao walihudhuria
mafunzo hayo.
38. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu
kuwa kati ya Waheshimiwa Wabunge 24 walioanza mafunzo yao ni Waheshimiwa
Wabunge 22 ndiyo waliomaliza mafunzo yao. Waheshimiwa
Wabunge wawili walipatwa na maradhi. Kwa hiyo hawakumaliza mafunzo yao.
(x) Shirika la Uzalishaji Mali la SUMAJKT
39. Mheshimiwa Spika, mwaka
1982 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa amri ya kuundwa kwa Shirika
la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) chini ya Sheria ya “The Corporation Sole
Establishment Act” No. 23 of 1974. Amri
hiyo ilitolewa katika Tangazo la Serikali Namba 116 la mwaka 1982. Lengo la
kuanzishwa kwa SUMAJKT ni kuwa na Shirika linalojiendesha kibiashara ili
kupunguza utegemezi kwa Serikali katika kuendesha shughuli za JKT na hatimaye
liweze kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla. Katika kutekeleza
majukumu yake SUMAJKT linaendesha miradi mbali mbali ya shughuli za kilimo na
ujenzi.
40. Mheshimiwa Spika, hivi
sasa shirika la SUMAJKT lina kampuni tanzu ya ujenzi ya “National Service Construction Department” inayofanya kazi kupitia
kanda zake tano za ujenzi (Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza).
Kanda hizi zinatekeleza majukumu yake baada ya kusajiliwa na Bodi ya Usajili ya
Makandarasi.
41. Mheshimiwa Spika, katika
kuendeleza shughuli za kilimo SUMAJKT imepewa maagizo makuu mawili ambayo ni
uzalishaji wa mbegu bora na mpango wa kujitosheleza kwa chakula katika Jeshi la
Kujenga Taifa.
a. Uzalishaji wa mbegu bora
42. Mheshimiwa Spika, hivi
sasa SUMAJKT inazalisha mbegu bora kwa kushirikiana na Makampuni ya
Agricultural Seeds Agency, Tanseeds, Southern Highland Seed Growers na Sub Agro
Ltd. Ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kuzalisha mbegu bora katika kiwango
kinachotakiwa na kuweza kutekeleza agizo la Serikali kikamilifu linahitaji
mtaji mkubwa kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa pembejeo, zana za kilimo
(combine harvesters na tractors) na mtambo wa kusindika mbegu bora.
b. Mpango wa kujitosheleza kwa chakula
43. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga
Taifa linategemea kuchukua vijana wasiopungua 41,000 kwa mujibu wa sheria na
10,000 wa kujitolea kwa kila mwaka. Ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kuwalisha
vijana hawa kwa mwaka linahitaji unga wa mahindi tani 4480, mchele tani
5,039.82, maharage tani 1,119.96, ngano tani 5,000, mafuta ya kula tani
3,957.192, nyama tani 389,225, mboga mboga na viungo tani 320.13 na matunda tani
2,799.9. Jeshi la Kujenga Taifa limekusudia kutekeleza miradi mbalimbali kwa
lengo la kukidhi mahitaji ya chakula kwa vijana na biashara. Miradi hiyo ni kama ifuatavyo:-
(a)
Vikosi vya 842 KJ (Mlale), 835 (Mgambo) na 844 KJ (Itende)
vimepewa jukumu la kuzalisha mahindi.
(b)
Kikosi cha 837 KJ (Chita) kimepewa jukumua la kuzalisha mpunga.
(c)
Vikosi vya 824 KJ (Kanembwa), 833 KJ (Oljoro) na Kambi ya Mtabila
vimepewa jukumu la kuzalisha maharage.
(d)
Vikosi vya 823 KJ (Msange), 821 KJ (Bulombora), na 834 KJ
(Makutupora) vimepewa jukumu la kuzalisha mawese, karanga na alizeti za kutosha
ili kusindika mafuta.
(e)
JKT lina mpango wa kuboresha ufugaji ng’ombe wa nyama katika
vikosi vya 833 KJ (Oljoro) na 841 KJ (Mafinga) na ufugaji kuku wa nyama na
mayai huko 832 KJ (Ruvu) ili kuzalisha nyama na mayai ya kutosha.
(f)
Kikosi cha 832 KJ (Ruvu) na 834 KJ (Makutupora) vimepewa jukumu la
kuzalisha aina mbalimbali za mboga na viungo.
(g)
Kikosi cha 835 KJ (Mgambo), Mtabila na 824 KJ (Kanembwa) vimepewa
jukumu la kuzalisha matunda.
44. Mheshimiwa Spika, hapana shaka
utekelezaji wa miradi hii ya kilimo na ufugaji inahitaji mtaji mkubwa. Jeshi la
Kujenga Taifa linahitaji shilingi 13,867,656,392 kwa ajili ya ununuzi wa
mbegu, madawa ya magugu na zana za kilimo ambapo uzalishaji wa mahindi utahitaji
shilingi 2,630,550,000.00, mchele shilingi 1,989,500,000.00, maharage shilingi 863,190,000.00, mafuta ya
kula shilingi 385,050,000.00, mboga
na viungo shilingi 398,417,500.00 na
ufugaji shilingi 7,600,948,892.00. Kwa
kuwa SUMAJKT haiwezi kupata fedha hizi kwa kupitia bajeti, Wizara yangu
imeagiza itafute wawekezaji kutoka ndani au nje watakaoweza kushirikiana nao
katika shughuli za kilimo na ufugaji wa kisasa.
Hivi sasa tayari tumeshapata wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika
kilimo cha kisasa.
45. Mheshimiwa
Spika, ili SUMAJKT iweze kuendesha shughuli zake kitaalamu inahitaji
kuimarisha utendaji wake. Nimeuagiza Uongozi wa SUMAJKT kutafuta wataalamu wa
masuala ya biashara, kilimo, ufugaji na ujenzi. Vile vile nimeliagiza Shirika
hilo litafute mikopo
yenye riba nafuu kutoka mabenki ili kuendesha miradi yake kwa uhakika.
c. Mradi wa Matrekta
46. Mheshimiwa Spika, wakati wa Hotuba
yangu ya Bajeti ya mwaka 2012/2013 nililiarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika
kutekeleza kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, Serikali kupitia Shirika la Uzalishaji
Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) lilipata mkopo kutoka Serikali ya
India wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 40. Kupitia mkopo huo, SUMAJKT waliingiza
matrekta, zana na vifaa vya kilimo vyenye thamani ya shilingi 69,146,318,781.00. Nafurahi kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa,
kufikia mwezi Septemba 2012 matrekta 1,833 yalikuwa yameuzwa, ambapo kati yake
matrekta 275 yameuzwa kwa fedha taslimu shilingi
8,270,481,780.00.
Aidha, matrekta 1,558 na zana za kilimo zenye thamani ya shilingi 53,675,837,001.00 ziliuzwa kwa
mkopo kwa wadau mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya, vikundi vya
uzalishaji mali, SACCOs, na watu binafsi wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa
Wabunge.
47. Mheshimiwa Spika, urejeshwaji wa
mkopo unakwenda sambamba na mikataba iliyosainiwa. Mpaka sasa jumla ya shilingi 14,575,490,929.00 zimerejeshwa. Hata hivyo, Shirika bado lina zana za kilimo
na vipuri vyenye thamani ya shilingi
7,200,000,000.00. Miongoni mwa zana
hizo ni pamoja na power tillers na pampu za umwagiliaji. Kufuatia mafanikio ya mradi huo, tumepokea
maombi mbalimbali kutoka kwa wananchi yanayofikia 4,000 ya kuuziwa
matrekta. Kati ya maombi hayo waombaji
73 wamekwisha toa fedha za utangulizi (deposit) kiasi cha shilingi 273,603,599.00. Kwa ujumla mradi wa matrekta umetekelezwa
vizuri na mahitaji yameonekana kuwa makubwa.
Kutokana na mahitaji yaliyopo mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na
Serikali ya India kuhusu Awamu ya Pili ya mkopo wa matrekta wenye thamani ya
Dola za Kimarekani milioni 92 yanaendelea.
(xi) Shughuli za Shirika la Mzinga
48. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013 Wizara ya Ulinzi na JKT imeendelea kuimarisha shirika la
Mzinga. Shirika hili linaendelea na uzalishaji kufuatia kukamilika kwa awamu ya
kwanza ya ukarabati wa kiwanda cha uzalishaji wa mazao ya kijeshi. Shirika
linaendelea kufanya jitihada za kupata malighafi pamoja na kukuza ujuzi wa
wafanyakazi wake ili kuongeza tija na ufanisi. Hata hivyo, utekelezaji wa
malengo haya utategemea sana upatikanaji wa fedha.
49. Mheshimiwa
Spika, chini ya sheria ya Makampuni Sura 212 Shirika la Mzinga limeweza
kuanzisha kampuni tanzu ya Mzinga Holdings ili kulipatia Shirika hilo mapato na
kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini. Hivi sasa Mzinga Holdings
imefanikiwa kupata miradi midogo ya ujenzi wa majengo. Aidha, Wizara imeipa
Mzinga Holdings jukumu la kuendesha maduka yasiyolipiwa kodi (Duty Free Shops)
kwa ajili ya kuwahudumia wanajeshi na familia zao vikosini. Mpaka sasa kampuni hiyo imeshafanya ukarabati
wa majengo katika vikosi vya 24 KJ Kigoma na 23 KJ Biharamulo. Duka la Kigoma tayari limeanza kutoa huduma
kwa wanajeshi na lile la Biharamulo linatarajiwa kuanza kazi ifikapo mwezi
Juni, 2013.
50. Mheshimiwa
Spika, Shirika la Mzinga Holdings pia lina mpango wa kuanzisha maduka
yasiyolipiwa kodi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kagera, Mwanza na
Shinyanga. Hivi sasa Shirika hilo linaendelea
na taratibu za kupata hati miliki za viwanja katika Mikoa hiyo. Ili kutekeleza azma hii Shirika linahitaji shilingi bilioni 6.5. Kwa kuwa Shirika
hili haliwezi kupata fedha zote kwa mara moja litatekeleza miradi hii kwa awamu
kutokana na makusanyo ya fedha zitakazopatikana katika miradi mingine.
(xii) Shughuli za Shirika la Nyumbu
51. Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Shirika la Nyumbu, Shirika hili limekusudia
kuimarisha shughuli za utafiti katika teknolojia ya mambo ya kijeshi. Shirika
la Nyumbu limeweza kufanya utafiti katika teknolojia za magari, uhandisi na
miundombinu ya majengo. Katika tafiti zake Shirika limekamilisha matengenezo ya
gari la deraya (Personnel Armoured Vehicle) kwa ajili ya kutumika katika sekta
ya ulinzi. Aidha, utafiti wa gari la nyumbu kwa ajili ya matumizi ya kijeshi
umeendelea kuimarishwa. Vile vile Shirika la Nyumbu linaendelea na utafiti wa
kuzalisha mtambo wa kuchuna mkonge ili kupata nyuzi na pampu za umwagiliaji.
Aidha, utafiti kuhusiana na “engine” na “gearbox” kwa ajili ya matumizi kwenye
matrekta madogo unaendelea vizuri. Shughuli
za uzalishaji wa vipuri vya mashine zinazotumika kwenye viwanda na mitambo pia
unaendelea.
(xiii) Mtandao wa Mawasiliano
Jeshini
52. Mheshimiwa Spika,
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kuboresha Mtandao wa
Mawasiliano Jeshini ili uweze kutoa huduma za mawasiliano bila ya kutegemea
mitandao ya kibiashara ya simu. Kazi hii imegawika katika awamu mbili. Katika
awamu ya kwanza mradi umekusudia kuboresha mawasiliano ya ndani ya vikosi.
Katika awamu ya pili mradi una lengo la kuimarisha mawasiliano kati ya kikosi
na kikosi kwa kutumia mfumo wa “satellite”. Sambamba na jitihada hizo, Wizara
inatekeleza mradi wa mawasiliano salama utakaowezesha kuwepo mawasiliano ya
kisasa baina ya vikosi vya Jeshi nchi nzima.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Novemba, 2012 hadi sasa umefikia asilimia
30. Mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2013.
(xiv) Upimaji na Ulipaji fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi
53. Mheshimiwa Spika, Jeshi la
Wananchi wa Tanzania lina mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa
makambi, makazi ya wanajeshi na maghala
ya kuhifadhia silaha. Vile vile Jeshi
linahitaji ardhi kwa ajili ya kuendeshea mafunzo na mazoezi ya kijeshi.
Kutokana na mgongano kati ya mahitaji ya ardhi kwa Jeshi na Wananchi, Wizara
yangu imekuwa ikikabiliwa na migogoro mingi.
Kwa kuwa maeneo mengi ya Jeshi hayajapimwa, wananchi hutumia fursa hiyo
kuyavamia. Hivi sasa kuna maeneo
yapatayo 80 yenye migogoro katika mikoa mbalimbali. Kwa bahati mbaya upimaji wa
maeneo ya Jeshi haufanyiki kwa kasi inayotakiwa kutokana na ufinyu wa
bajeti. Wizara yangu ina mpango wa
kununua vifaa vya kisasa vya kupimia ardhi kwa matarajio kwamba kazi ya upimaji
itafanywa kwa haraka zaidi na hatimaye kuepusha uvamizi wa maeneno ya Jeshi
unaofanywa na wananchi.
54. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa
ikichukua hatua kadhaa kutatua migogoro hiyo ikiwemo upimaji na ulipaji wa
fidia ya ardhi zilizochukuliwa na Jeshi. Wizara imekamilisha kulipa fidia
katika eneo la Kiharaka (Mapinga) mkoani Pwani. Aidha, katika mwaka huu wa
fedha Wizara ina mpango wa kulipa fidia ya maeneo ya Mwakidila –Tanga, Cheyo
– Tabora na Mwantini – Shinyanga. Wizara yangu itaendelea kulipa fidia
ya ardhi kwa wananchi mbalimbali kadri hali ya upatikanaji wa fedha
itakavyoruhusu.
(xv) Mkakati wa Kupambana na UKIMWI
55. Mheshimiwa Spika,
Wizara ya ulinzi imeendelea kutekeleza mkakati wa kupambana na maambukizi ya Virusi
vya UKIMWI kwa kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga ili kuzuia maambukizi
mapya. Wizara imekuwa ikihimiza upimaji
wa hiari kwa maafisa, askari na watumishi wa umma na vijana wa JKT kwa kutumia
waelimishaji rika. Aidha, kwa wale ambao tayari wameshathibitika kuwa
wameambukizwa virusi vya UKIMWI wamekuwa wakipatiwa dawa za kupunguza makali ya
virusi (ARVs) bure katika vituo vya huduma na matibabu (care and treatment centres)
vilivyoko katika hospitali kuu za kanda na huduma ya lishe katika maeneo ya
kambi.
(xvi) Hifadhi ya Mazingira
CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2012/2013
57. Mheshimiwa Spika, changamoto
kubwa zinazoikabili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni mbili. Kwanza ni kutokukidhi kwa ukamilifu mahitaji
ya kutekeleza mipango yake ya kila mwaka ya kuendeleza Jeshi la Wananchi wa
Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa. Mahitaji ya mipango ya jeshi letu ni
makubwa kama ilivyo kwa majeshi mengine duniani ikilinganishwa na uwezo mdogo
wa Serikali. Athari za hali hiyo ni kuwepo kwa upungufu wa mahitaji muhimu ya
kiulinzi, yakiwemo ya ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi, utoaji wa huduma
kwa wanajeshi na ulipaji duni wa huduma muhimu za maji, umeme, mafuta na
vilainisho. Changamoto hii pia
imesababisha Jeshi la Kujenga Taifa kufupisha muda wa uendeshaji wa mafunzo ya
Mujibu wa Sheria kwa vijana waliomaliza kidato cha sita kutoka miezi sita iliyokusudiwa awali na kuwa miezi
mitatu.
58. Mheshimiwa Spika, changamoto
ya pili ni upatikanaji wa fedha za
maendeleo. Katika kipindi hiki fedha za maendeleo zilitolewa kwa kuchelewa na
kwa kiwango pungufu. Kielelezo cha hali
hii ni, upokeaji wa fedha hizi kwa mwaka 2012/2013 ambapo hadi sasa mafungu yote matatu ya
Wizara yamepokea jumla ya shilingi
135,700,000,000.00 sawa na asilimia 33.2
ya shilingi 408,189,566,000.00 zilizoidhinishwa.
Hali hii imesababisha kulimbikiza madeni ya kimikataba na kuathiri miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo upimaji wa ardhi ya maeneo ya jeshi na
kutokamilika kwa zoezi la kulipa fidia ya maeneo yaliyochukuliwa na jeshi. Kwa
ujumla changamoto hizi ambazo zimeendelea kwa muda mrefu sasa zimekuwa kikwazo
cha utekelezaji wa majukumu ya Ulinzi na JKT.
MPANGO WA MWAKA 2013/2014
59. Mheshimiwa Spika, mpango wa Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2013/2014 unakusudia kuimarisha
utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa Jeshi katika kutekeleza majukumu yake
kulingana na Dira na Dhima ya Wizara. Vile vile Wizara inakusudia kukamilisha miradi ambayo
haijamalizika pamoja na kulipa madeni ya ununuzi wa vifaa. Kwa hivyo, Wizara
yangu itakuwa na jukumu la kutekeleza shughuli zifuatazo:-
(i)
Kupunguza tatizo la wanajeshi kuishi uraiani kwa kuanza awamu ya
kwanza ya ujenzi wa nyumba 6064, kukarabati na kuimarisha miradi ya ujenzi
inayoendelea.
(ii)
Kulipatia Jeshi zana na vifaa vya kijeshi ikiwemo vifaa vya
uhandisi wa medani, ndege vita na magari.
(iii)
Kukarabati mitambo na miundombinu katika Mashirika ya Mzinga na
Nyumbu ili kuimarisha shughuli za viwanda na kuendeleza teknolojia ya masuala
ya kijeshi.
(iv)
Kuboresha mawasiliano ya simu ndani ya Jeshi baina ya vikosi na
kwenye makambi ya jeshi.
(v)
Kulipa mikopo ya Mfuko wa NSSF.
(vi)
Kupima na kulipa fidia ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya
wananchi yaliyochukuliwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi.
(vii)
Kujenga maghala ya kuhifadhia silaha na zana za kijeshi.
(viii)
Kulipia gharama za matumizi ya huduma za umeme, maji na simu kwa
ajili ya uendeshaji wa majukumu ya kimsingi zikiwemo operesheni za kiulinzi na
mafunzo.
(ix)
Kulipia stahili mbalimbali za Maafisa, Askari, vijana wa Jeshi la
Kujenga Taifa na Watumishi wa Umma ikiwemo mishahara, posho za chakula kwa
ajili ya wanajeshi, matibabu, likizo, maziko na mafunzo.
(x)
Kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za
kijeshi na kiulinzi.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
i. Makadirio ya Mapato
60. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
2013/2014 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekadiria kukusanya
mapato kiasi cha Shilingi 68,206,000.00
katika mchanganuo ufuatao:-
a.
Fungu 38 NGOME
Shilingi 1,501,000.00
b.
Fungu 39 JKT
Shilingi
46,703,000.00
c.
Fungu 57 WIZARAYA ULINZI Shilingi 20,002,000.00
Jumla Shilingi 68,206,000.00
ii. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo
61. Mheshimwa Spika, ili
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iweze kutekeleza majukumu yake
katika Mwaka 2013/2014 inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,102,999,529,000.00 ambazo kati yake Shilingi 857,417,502,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Shilingi 245,582,027,000.00 ni
kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Mchanganuo wa bajeti hiyo kwa
kuzingatia mafungu ya Wizara ni kama ufuatao:-
FUNGU 38 NGOME
Matumizi ya Kawaida
Sh.651,015,373,000.00
Matumizi ya Maendeleo
Sh. 10,000,000,000.00
Jumla ya Makadirio kwa Fungu 38
Sh. 661,015,373,000.00
FUNGU 39 JKT
Matumizi ya Kawaida
Sh 187,301,634,000.00
Matumizi ya Maendeleo
Sh. 6,000,000,000.00
Jumla ya makadirio kwa Fungu 39
Sh. 193,301,634,000.00
FUNGU 57 WIZARA YA ULINZI
Matumizi ya Kawaida
Sh. 19,100,495,000.00
Matumizi ya Maendeleo
Sh. 229,582,027,000.00
Jumla ya Makadirio kwa Fungu 57
Sh.
248,682,522,000.00
3 comments:
Hey there! Do you know iif they make any plugins to safeguard agaist hackers?
I'm kinda paranoid about losing everything I've worked hard on.
Anny suggestions?
Hi, I log on to your blog like every week. Your writing styoe iis awesome, keep it
up!
Thank you, I've just been looking for info approximately
this subject for a while and yours is the best I've
discovered so far. But, what concerning the conclusion? Are you positive about thee source?
Post a Comment