WAZAZI 'WASUSIA' MISA NA MAZISHI YA BILIONEA WA ARUSHA...

Marehemu Nyaga Mawalla.
Wazazi wa Wakili Nyaga Mawalla, jana hawakuonekana katika misa, wala maziko ya mtoto wao, yaliyofanyika jijini hapa.

Misa ya kumuaga Nyaga, anayetajwa kuwa bilionea kijana, ilianza saa 5.10 asubuhi, katika Kanisa la Kilutheri la Kenya, Usharika wa Uhuru Highway.
Baada ya misa hiyo, iliyoongozwa na Mchungaji Izare Obare na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Tanzania, maziko yalifuata katika makaburi ya Lang’ata.
Baba wa wakili huyo, Wakili Juma Mawalla na mama mzazi, Margareth Sawaya, hawakuhudhuria misa wala maziko ya kijana wao kama walivyotangaza awali.
Kabla ya maziko hayo, kwa wiki nzima tangu afariki dunia, mama huyo alisisitiza, kwamba angependa mwanawe kipenzi azikwe nyumbani kwao Marangu Moshi, na si kwingine.
Pia baba yake, Juma, ambaye ni wakili wa siku nyingi, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hatahudhuria maziko hayo, iwapo atazikwa eneo tofauti na Marangu. 
Pamoja na kutokuwapo wazazi hao, baadhi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa waliohudhuria, na kutoa kauli za kuiwakilisha familia hiyo.
Mmoja wa viongozi aliyetoa kauli kwa niaba ya familia, ni Jaji mstaafu Mark Bomani, ambaye alisema alimfahamu Nyaga tangu utoto na ndiye aliyependekeza kupewa jina la Nyaga.
Jaji Bomani alisema yeye alisoma na kufanya kazi na Juma na alipozaliwa na kukua alipendekeza apewe jina hilo, kutokana na kipaji alichokiona kwa kijana huyo.
Nyaga kwa mujibu wa Jaji Bomani, ni neno la Kisukuma lenye maana ya mtu mwenye kipaji maalumu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema ni mwanafamilia ya Nyaga na kifo hicho kimeacha pengo si tu katika familia, bali kwa Taifa hasa sekta ya utalii katika uhifadhi wa wanyamapori.
Alisema Nyaga alikuwa mdau wa uhifadhi wa wanyamapori na alianzisha ranchi za kuhifadhi wanyama Serengeti na Lindi.
Katika ranchi hizo kwa mujibu wa Nyalandu, alipenda kuona jamii inayozunguka inanufaika na kupata maendeleo na kutimiza malengo hayo.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher  ole Sendeka, alisema kifo hicho kimemsikitisha na kuiomba familia kuwa na utulivu wakati huu wa majonzi.
Waziri wa zamani katika awamu mbalimbali, Sir George Kahama, alisema maneno mengi yatazungumzwa katika msiba huo na kuiomba familia kuwa na utulivu.
Kabla ya maziko, msiba huo ulitawaliwa na sintofahamu  kuhusu wapi azikwe Nyaga,  lakini ilifikia tamati baada ya wakili wake, Fatuma Karume, kutoa wosia ambao ulielekeza azikwe alikofia (Kenya).
Nyaga alielekeza katika wosia huo maeneo mawili ya kuzikwa, kulingana na mazingira ya kifo chake.
Kwanza alielekeza akifia Tanzania, azikwe katika shamba la Momela wilayani Arumeru, Arusha.
Pili kwa mujibu wa wosia uliotolewa na Wakili Karume, ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Nyaga alielekeza akifia nje ya nchi,  maziko yake yafanyike katika nchi alimofia.
Kutokana na mgogoro huo, kulikuwa na taarifa  kuwa viongozi wa dini na mila, walitumwa kwa wazazi hao, ili walegeze kamba na kukubali maziko ya mtoto wao yazingatie wosia wake.
Vyanzo vya habari kutoka karibu na familia hiyo, vilieleza kuwa mdogo wa marehemu, Wilfred, alituma viongozi wa dini wakiwamo wachungaji, mapadri na wazee wa mila ya Kichaga, kwenda kwa wazazi hao.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao walitakiwa  kwenda Marangu kuomba wazazi wakubaliane na wosia wa mtoto wao alioacha akiwa hai. 
Mama yake alishasisitiza, kwamba angependa mwanawe kipenzi azikwe nyumbani kwao Marangu Moshi na si mahali pengine popote.

No comments: