WAJAWAZITO WANG'ATISHWA NGE ILI WAPATE UCHUNGU RUKWA...

Mdudu aina ya Nge.
Wakunga wa jadi mkoani Rukwa, wamekuwa wakitumia nge kusaidia wajawazito waliopitiliza muda wa kujifungua, kupata uchungu na kujifungua salama.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi, umebaini kuwa  wajawazito wanaokwenda kwa wakunga wa jadi wakiwa na tatizo la kupitiliza muda wa kujifungua, hung’atishwa nge mwilini ili wapate uchungu.

Wakunga waliozungumza na mwandishi kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisifu sumu ya mdudu huyo inayodaiwa kuwa kali, kwa kusababisha mjamzito aliyepitiliza muda, kupata uchungu na kujifungua salama.
“Ni sawa  na hospitalini, mjamzito unapofika muda wa kujifungua, inaweza kutokea siku zake za kujifungua zimepitiliza na madaktari humpa dawa ya kuongeza uchungu  na  hatimaye hujifungua.
“Vivyo hivyo nasi tunawang’atisha nge wajawazito, tena hatuwaarifu kuwafanyia hivyo, tunashitukiza na wengi tunaowafanyia hivyo,  hujifungua salama,“ alisema  mmoja  wa wakunga hao wa jadi.
Mmoja wa waliopata kung’atishwa nge, akijitambulisha kwa jina moja la Maria, alikiri kuongezwa uchungu  kwa  kung’atishwa mdudu huyo mwilini bila kujiandaa kuwa atafanyiwa  hivyo, ambapo  alidai hatimaye  alijifungua mtoto wake wa kiume salama.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado ni jambo la busara  na  salama kwa wajawazito  kujifungulia  katika  vituo vya  kutolea  huduma  ya afya, kuliko kujifungulia kwa wakunga wa jadi, ambao wengi wao hawana ujuzi
wa kutosha  pale  mama  anapopata  matatizo  makubwa  ya  uzazi wakati wa kujifungua.
Maria alidai kuwa wanalazimika kujifungulia kwa wakunga wa jadi hususan vijijini, kutokana  na  uhaba  wa watumishi katika  vituo  vingi  vya kutolea  huduma ya afya hususani vijijini, na wakunga wa jadi huwatoza kati ya Sh 10,000  na Sh 15,000.
Diwani wa Kata ya Kipili, wilayani Nkasi, Basilio Mbwilo,  alikiri wakunga  wa jadi kutumia  nge  kwa wajawazito ili kuwaongeza  uchungu wajifungue haraka.
“Hiyo ni kweli  kabisa, wala si siri,  unajua sumu ya  nge  ni kali  sana, kama ilivyo hospitalini wajawazito wanaopitiliza  siku  za kujifungua,  hupewa  dawa  ya kuwaongeza uchungu, sasa  hiyo ni  kitaalamu zaidi.
“Basi ni hivyo pia vijijini  kwa wakunga wa jadi,  ni  kweli  wanatumia  nge kung’atisha wajawazito mwilini.  Sumu ya nge wanaamini kuwa  inasaidia  kumwongeza mama  uchungu wa uzazi kwa kasi ya
ajabu, lakini wanawashitukiza hawawataarifu kwanza,  si unajua uchungu  mtu anaoupata akiumwa na nge?” Alihoji Mbwilo.
Mratibu  wa Mradi  wa Uhamasishaji wa Afya ya Uzazi Rukwa (TMEP), Dk John Komba, alidai hawezi kusema moja kwa moja kuwa sumu ya  nge  inaweza kumwongeza  mjamzito  uchungu wa  uzazi, kwani  inatakiwa  sumu  hiyo ifanyiwe utafiti wa kitabibu,  ili  kubaini  kama  ni  salama kwa matumizi ya  binadamu.
“Mimi ningeshauri akina mama wanapobaini  kuwa  na ujauzito, waanze kuhudhuria na kujifungulia  katika  vituo  vya huduma ya afya kwa ajili  ya usalama wao na mtoto atakayezaliwa na si vinginevyo,” alisisitiza Dk Komba.
Muuguzi  wa Manispaa  ya Sumbawanga, Tizowere Munkondia,  alisema haamini  kama  sumu  ya nge,  ni  njia sahihi  kwa  sasa,  wakati  kuna huduma bora  inayotolewa kwa wajawazito  katika  vituo  vya kutolea  huduma  ya afya mkoani humo.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni na hali ya kujifungua katika  wilaya ya Sumbawanga,  kati  ya  wajawazito  16,581 wilayani  humo, 12,483 walijifungulia katika  vituo  vya huduma ya afya sawa na asilimia 76.3.
Pia takwimu  hizo zinaonesha kuwa wajawazito 3,729,  walizalishwa  na wakunga  wa jadi  wilayani  humo, ambapo 372 walijifungulia njiani.
Nge hupendelea kuishi maeneo yenye joto ingawa wapo pia wanaopendelea kuishi katika maeneo yenye ubaridi milimani na katika maeneo ya kawaida. Pia huweza kuonekana majumbani.
Nge wa njano mwenye mikia bapa - Androctonus australis- miili yao ina pingili 18 na kwa kawaida huwa na urefu wa kati ya sentimeta tano na 10, lakini aina nyingine hususan   Pandinus imperator huweza kufikia urefu wa kati ya sentimeta 20 na 30.
‘Sindano’ yake anayotumia kung’ata iko mwishoni mwa mkia. Ana vifuko viwili ambavyo hutengeneza na kutunza aina mbalimbali za sumu. Hutumia sindano kwa kazi mbalimbali: kukamata mawindo, kujilinda na hata wakati wa kujamiiana. 
Nge hufanya kazi zake usiku. Na hula viumbe hai: buibui, wadudu, viluwiluwi na wakati mwingine mijusi na panya wadogo.
Aina zote za nge wana sumu zinazoweza kudhuru hasa wadudu na kuwaua, lakini ni idadi ndogo tu ya nge katika aina zaidi ya 1,050 duniani ndio hatari kwa binadamu.
Sumu ya nge ina kemikali nyingi, ambazo hazijachunguzwa. Sumu kutoka nge mmoja inaweza kuwa na kemikali ambazo ni maalumu kudhuru aina fulani ya viumbe.
Nge anapong’ata maumivu yake hudumu kwa saa moja na huweza kusababisha ganzi, mwili kukakamaa na mwasho katika eneo lililong’atwa.
Baadaye uchungu unaweza kuenea na kusisimua mwili, kupandisha joto la mwili; uso, ulimi, na kifua huvimba sambamba na maumivu makali kifuani au mgongoni.
Baadhi ya aina za nge (Pandinum imperator, Leiurus quinquestriatus, Buthus occitanus, Androctonus australis, n.k.) wana uwezo wa kudunga kiasi kikubwa cha sumu.
Katika matukio kama hayo, mwathirika hupata homa, hujawa mate kinywani, ngozi humkauka, hupatwa kichefuchefu au kutapika, huchanganyikiwa, huzimia, huku pia mapigo ya moyo yakipungua au kuongezeka, joto la mwili kubadilikabadilika na mapafu kujaa maji na wakati mwingine hutokea moyo au mapafu kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, uwezekano wa mwathirika kupoteza maisha kutokana na sumu ya nge huwa mdogo kwani hutegemea kiwango cha sumu iliyodungwa na umbile la aliyeng’atwa kwa maana ya ukubwa au udogo wa mwili, lakini pia hali ya kiafya ya aliyeng’atwa; watoto wako hatarini zaidi kuliko watu wazima kutokana na maumbo yao.

No comments: