BODI YA MAKANDARASI YASHIKWA KIGUGUMIZI JENGO LILILOPOROMOKA DAR...

Jengo lililoanguka katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) hadi jana ilishindwa kuzungumzia kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 katikati ya Jiji la Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.

Aidha, imeshindwa kukutana na waandishi wa habari kila walipofika kuulizia tamko lake kuhusu ajali hiyo na badala yake, mfanyakazi wa Mapokezi amekuwa akitoa majibu ya kutokuwa na taarifa za kuwapo mpango wa kutoa tamko la aina hiyo.
"Hata jana kuna waandishi walifika hapa kutafuta wakubwa wangu wakisema wamepata taarifa kuwa CRB inataka kutoa tamko la kuporomoka kwa jengo hilo, lakini kwa kweli hatujajulishwa kuhusu suala hilo kiofisi wala kibinafsi.
"Hata Katibu Muhtasi wa bosi nimewasiliana naye anasema hana taarifa kama kutakuwa na tamko kwa waandishi wa habari sasa pengine uulize kwa hao wengine," alisema na kumhakikishia mwandishi kuwa taarifa zikiwapo au viongozi wake watakapokuwa tayari kusema lolote watasema.
Wakati hayo yakiendelea, wananchi wameendelea kujiuliza maswali, ikiwa ni pamoja na endapo mkandarasi aliyekuwa akishughulika na ujenzi huo alisajiliwa kwa kufuata vigezo au la, na kama kulikuwa na usimamizi unaostahili au ulipuaji na uzembe.
Hata hivyo, wakati Watanzania wakitarajia kusikia lolote kutoka kwa bodi hiyo kwa ushirikiano na Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), iliunda  Kamati ya uchunguzi inayoendelea na kazi kimya kimya.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, Kamati hiyo  iliongezwa wataalamu watano kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa, Polisi na Mhandisi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Katika ajali hiyo, watu 36 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa huku mali kama vile magari vikiharibiwa. 

No comments: