WANAJESHI WASAKWA KWA MAUAJI YA DEREVA WA BAJAJI KAWE...

Barabara hii iligeuka uwanja wa mapambano kwa muda.
Polisi mkoani Kinondoni inashikilia watu 12 kwa kuvamia kituo cha Polisi Kawe na kuleta vurugu, huku likiwatafuta watu wanaodhaniwa kuwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kambi la Lugalo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian (20).

Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe, alisema wanasubiri uchunguzi unaoendelea ili kubaini kama kweli waliohusika na tukio hilo ni wanajeshi ili waweze kuwachukulia hatua.
Alisema kutokana na taratibu za jeshi zilivyo, hawana pingamizi lolote kwa polisi kama watataka kuingia kambini na kufanya uchunguzi wa askari wake kutokana na ukweli kuwa vyombo hivyo vya ulinzi vina utaratibu maalumu  unaowezesha mambo kufanyika.
 Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Charles Kenyela, alisema wanaoshikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, wanadaiwa kufanya fujo hiyo juzi katika kituo cha Kawe  wakishinikiza kukabidhiwa mtu aliyetambulika kwa jina la Revenary Anatory(40) anayedaiwa kuwa askari Mgambo katika Kampuni ya Bakhresa ili wakamdhuru.
Akieleza chanzo cha watu hao  kumtafuta mtu huyo, Kenyela alisema mgambo huyo  inadaiwa kuwa ndiye aliyekwenda kuwaita watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wanajeshi ili kuwaadhibu vijana waliokuwa wamekaa katika moja ya eneo la  Kawe ambalo ni maarufu kwa watu wanaokaa na kuvuta bangi.
Alisema baada ya wanajeshi hao kufika katika eneo hilo, waliwakurupusha vijana hao na kuanza kukimbia huku na kule kabla ya kumkuta kijana huyo anayedaiwa kuwa hakuwepo katika eneo hilo isipokuwa kutokana na purukushani hizo ndipo wanajeshi hao wakamvamia na kumpiga.
“Baada ya kumshambulia huku akiwa hajiwezi, walimchukua hadi kando kando ya mto Mbezi na kumtupa hapo wakati huo akiwa tayari ameshakufa kisha wao kutoweka,” alisema Kenyela.
Aidha Kenyela alisema kutokana na kitendo hicho cha kuuawa kwa kijana Yohana ambaye ni mtoto wa Mchungaji wa Kanisa la ‘Yerusalem Mitomingi Ministry’ lilolopo Kagera jijini Dar es Salaam, wananchi hao waliamua kuungana na kumtafuta mgambo huyo ambaye alikimbilia katika moja ya nyumba zilizopo Kawe na kujificha ili kujinusuru hadi polisi walipofika na kumpeleka katika kituo cha Kawe.

No comments: