PROFESA WAMBARI WA UDSM AFARIKI DUNIA...

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wakili maarufu, Profesa Michael Wambari, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, Profesa Wambari alikumbwa na mauti jana mchana.
Akizungumzia msiba huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Profesa Mwesiga Baregu, alisema chuo hicho pamoja na tasnia ya sheria, imepoteza mtu muhimu ambaye pengo lake halitozibika.
“Kwa kweli nimepokea taarifa za msiba huu kwa mshituko kwa kuwa Profesa Wambari nilimfahamu kwa muda mrefu, ni mmoja wa wahadhiri wa upande wa sheria aliyejijengea nafasi yake vyema katika tasnia hiyo,” alisema Profesa Baregu.
Alisema Profesa huyo alikuwa na uwezo wa kuchanganua mambo mbalimbali, lakini kubwa zaidi alikuwa akishirikiana vyema na mawakili wenzake.
“Bado hata kwa umri wake alikuwa anahitajika, kwa kweli tumempoteza mtu muhimu sana,” alisema Profesa Baregu kwa masikitiko.
Mhadhiri mwingine aliyewahi kufanya kazi na Profesa Wambari, Dk Azaveli Lwaitama, alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa UDSM na fani ya sheria.
Alisema Profesa Wambari ni kati ya wasomi waliobobea katika tasnia ya sheria na alikuwa mtu muhimu katika Shule Kuu  ya Sheria.
“Tangu niingie chuo 1982 kama mhadhiri, alikuwepo na mambo mengi amefanya katika taaluma hiyo.
“Amewafundisha watu wengi sana. Nilikuwa nafundisha stadi za mawasiliano katika Shule Kuu ya Sheria, nimeendelea kumuona kama mtu ambaye wenzake walimwendea kwa ushauri na alishakuwa mlezi wa wanazuoni wa baadaye wa sheria,” alisema Dk Lwaitama.

No comments: