JAJI MSTAAFU MWIPOPO KUZIKWA KESHO MUFINDI...

Marehemu Jaji Ernest Mwipopo.
Jaji mstaafu Ernest Mwipopo (63) aliyefariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro anatarajiwa kuzikwa kesho katika kitongoji cha King’ola, kijiji cha Ibatu, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Mtoto wa  marehemu, Angaza Mwipopo alisema hayo jana  mjini hapa kabla ya mwili wa baba yake  kusafirishwa kwenda Dar es Salaam ukitoka  chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
“ Tumeondokewa na mzazi wetu , rafiki  na kwa kiasi kikubwa ametufanya ndugu , watoto wake kuwajengea uwezo wa kujitegemea kimaisha na alikuwa ni mtu wa watu...na alikuwa awapitie ndugu zake wa Morogoro kuwasalimu,” alisema Angaza.
Kwa mujibu wa Angaza ambaye ni  Mwanasheria , mwili wa marehemu ulifikishwa kwenye Hospitali ya Jeshi la Lugalo  jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaliwa vyema  na kupelekwa nyumbani kwake Oysterbay kuangwa rasmi  leo kabla ya kusafirishwa kwenda Mufindi kwa maziko.
Dada wa Marehemu,  Grace Mnyanyi, alisema pia aliwasiliana na Jaji huyo mstaafu, akiwa njiani kutokea Iringa akimtaarifu kuwa angepitia nyumbani kwake kupata chakula , hivyo aandae ugali mkubwa.
Alisema , aliwasiliana naye tena akiwa Mikumi, dakika chache kabla ya ajali kutokea , lakini alipigiwa simu na mmoja wa aliyenusurika kwenye ajali hiyo akimwarifu kuwa wamepata matatizo kidogo eneo la Mkata na kuhitajika kufika eneo hilo pasipo kukosa.
“Nilifika Mkata , lakini nikaona magari yanawabeba watu walioumia  na mmoja wao , alinifahamisha kwamba Jaji alikuwa akipatiwa tiba eneo la ajali, nilipofika hapo nilikuta amefunikwa nguo mwili mzima , amefariki dunia,” alisema Mnyanyi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera , aliyekuwepo kwenye shughuli za kumuaga marehemu, alimtaja  Jaji mstaafu huyo kuwa alikuwa ni tegemeo kubwa kwa taifa na kuaminiwa  na Serikali pamoja na wananchi. Alisema kutokana na uaminifu huo, aliteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini.

No comments: