TANZANIA KUTOA MSIMAMO WAKE LEO KUHUSU ZIWA NYASA...

Wananchi wakiendelea na shughuli zao za uvuvi kwenye Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
Serikali leo inatarajia kutoa tamko kuhusu msimamo wa Tanzania, baada ya Malawi kujitoa kwenye mazungumzo ya usuluhishi na kuamua kupeleka mgogoro  kwenye Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipohojiwa na waandishi wa habari wakitaka msimamo wa Tanzania kuhusu uamuzi wa Malawi.
Alisema kwa jana asingeweza kuzungumza lolote, lakini Tanzania ina uamuzi wake ambao atautoa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari, ofisini kwake. 
“Kuhusu suala hili, kuweni na subira kesho (leo) nitatoa tamko litakalobainisha wazi msimamo wetu kuhusu mgogoro huu na hatua hiyo ya Malawi,” alisema Membe.
Juzi Rais wa Malawi, Joyce Banda, alibainisha wazi kuwa nchi yake haijaridhishwa na hatua za usuluhishi wa mgogoro huo na inatarajia kupeleka suala hilo ICJ.
Hivi karibuni, vyombo vya habari vya Malawi, viliripoti kuwa Rais huyo alisema nchi yake haitopoteza muda na usuluhishi uliokuwa ukifanywa na marais na viongozi wastaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) chini ya Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chisano.
“Maoni yetu ni kuwa baadaye itabidi tupeleke suala hili mahakamani. Hatutaendelea kupoteza muda na usuluhishi,” alisema Rais Banda wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini humo akitoka Marekani na Uingereza.
Katika hoja yake kuu ya kujitoa kwenye mazungumzo ya usuluhishi, alibainisha kuwa usuluhishi huo umeingia dosari kutokana na taarifa zilizotolewa na Malawi kuvujishwa kwa Tanzania.
Mgogoro huo, uliodumu kwa muda mrefu sasa ni mpaka katika Ziwa Nyasa, ambapo Malawi imekuwa ikidai kuwa Ziwa hilo lote ni mali yake wakati Tanzania ikisisitiza  kuwa nusu ya Ziwa iko Tanzania.
Wakati Membe akitarajiwa kutoa msimamo leo, Ofisa wa Maji wa Bonde la Ziwa Nyasa, Witgal Nkondola, alisema maji ya Ziwa hilo asilimia 59 hutoka kwenye mito ya Tanzania, kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na maji yatokayo Malawi na Msumbiji.
Nkondola alisema Malawi inachangia asilimia 33, huku asilimia nane zikichangiwa na mito iliyo Msumbiji.
Hata hivyo ofisa huyo alisema ni Watanzania wachache wanaotambua kuwa mito yao inachangia kwa kiasi kikubwa maji ya Ziwa hilo, hivyo wanapaswa kujisikia fahari kuwa sehemu ya wamiliki wa Ziwa hilo.
Aliitaja mito ya Songwe, Kiwira na Lufilyo mkoani Mbeya, kuwa miongoni mwa inayoingiza maji kwa wingi ziwani humo.
Hata hivyo alikiri kutofahamika vizuri kwa taarifa za Ziwa hilo kwa Watanzania, kutokana na kutotangazwa kwa mambo yake mengi na kuongeza kuwa ni wakati sasa mamlaka zinazofanya shughuli zao ndani ya ziwa hilo kuweka wazi taarifa zao.

No comments: