SERIKALI YASITISHA AWAMU YA PILI MATUMIZI YA DIKODA...

Dikoda ama Kisimbuzi.
Watazamaji wa televisheni katika mikoa ambayo mfumo wa dijitali haujaanza kutumika wataendelea kuangalia matangazo bila kutumia visimbuzi (decorders).

Hiyo imetokana na uamuzi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, kusitisha awamu ya pili ya kuzima mitambo ya analojia na kuwasha ya dijitali, ili kufanyia tathmini yaliyojiri katika awamu ya kwanza.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa hatua hiyo ni ya muda ili kupisha tathmini hiyo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa mabadiliko ya utangazaji kutoka analojia kwenda dijitali hayaepukiki na kutaka wadau kushirikiana katika mchakato kama ilivyokubalika kupitia vikao vilivyofanyika tangu mwaka 2005.
Profesa Mbarawa alisema Serikali haina mpango wa kusitisha kuwasha mitambo ya dijitali na kuzima ya analojia na inachofanya sasa ni kuhakikisha mchakato mzima wa dijitali unafanikiwa nchini.
“Tupo kwenye awamu ya kwanza bado na tutaendelea na mpango wetu wa kumalizia kuzima mitambo ya analojia na kuwasha ya dijitali katika Mkoa mmoja wa Mbeya uliobakia,” alisisitiza Mbarawa.
Alisema awamu ya kwanza ilihusisha mikoa saba ambayo baadhi yao ni Dar es Salaam, Tanga, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya; inayotarajiwa kuzimiwa rasmi mitambo yake ya analojia na kuwashiwa mitambo ya dijitali mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema awamu ya pili iliyotarajiwa kuanza wakati wowote na kuhusisha mikoa zaidi ya 14, wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau na Kamati ya Bunge ya Miundombinu, walikubaliana isitishwe kwa muda hadi tathmini ya kina itakapofanyika katika mikoa saba iliyoanza kutumia mfumo huo mpya wa dijitali.
“Tunachotaka kuangalia ni changamoto zilizopo baada ya kuanza kutumika kwa mfumo huu wa dijitali na namna ya kuzifanyia kazi, baada ya hapo tutaendelea na utaratibu wetu wa kuhakikisha maeneo yote ya Tanzania yanatumia dijitali na kuondokana na analojia,” alisema.
Hata hivyo, alisema katika mikoa iliyobaki, maeneo mengi yaliyofanyiwa tathmini yamebainika kuwa hayatumii sana mfumo wa analojia hivyo katika maeneo hayo, Serikali itawasha tu mitambo ya dijitali kwa kuwa hakuna mtambo wa analojia wa kuzimwa.
Alisema msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo la matumizi ya dijitali ni kuhakikisha kuwa hadi ifikapo Juni 17, 2015 dunia nzima itazima mitambo ya analojia na kuwasha ya dijitali, na hivyo Tanzania nzima itakuwa tayari inatumia mfumo huo mpya.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia na kuwasha ya dijitali katika mikoa iliyobaki ili kutoa mwanya wa kufanyia tathmini kwanza maeneo yaliyokwishaanza kutumia mfumo huo mpya.
Hatua hiyo ya Serikali inamaliza mvutano uliokuwapo baina ya Serikali na wamiliki wa vituo vya televisheni, ambao walikuwa wakitaka hatua hiyo isitishwe na analojia iende sambamba na dijitali, kwani athari za kukosa matangazo zilishaanza kuonekana dhidi yao.
Katikati ya wiki hii, Serikali iliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuchunguza kauli
zilizotolewa na baadhi ya wamiliki hao kwa kutumia muda mrefu kuzungumzia mabadiliko ya mfumo wa
utangazaji wa analojia kwenda dijitali kubaini kama hawakukiuka sheria na kanuni za utangazaji.
Waziri Mbarawa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Jumatano, alisema matamko ya
hivi karibuni yaliyotolewa na wamiliki hao wakitaka  matangazo ya dijitali yaende pamoja na ya analojia kwamba ni upotoshaji.
Baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari na hasa televisheni, walisema uamuzi wa kuhamia mfumo wa dijitali umefanyika haraka, hali ambayo imekosesha baadhi ya watu haki ya kupata habari.

No comments: