FREEMAN MBOWE ABEBA AHADI ALIYOTOA BILIONEA WA ARUSHA...

Baadhi ya mawakili kutoka Dar es Salaam, Arusha na Moshi wakijiandaa kushusha kaburini jeneza lenye mwili wa marehemu Nyaga Mawalla 'Bilionea wa Arusha' jijini Nairobi, nchini Kenya juzi.
Kiwanja cha ekari tano kilicho eneo la Burka jijini Arusha kilichotolewa na Nyaga Mawalla kwa lengo la ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, kitatumika kama ilivyokusudiwa. 

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwenye maziko ya mwanasheria huyo jijini hapa.
Mbowe alisema na kusisitiza kuwa kati ya vitu ambavyo vitafanya chama hicho kimkumbuke marehemu, ni kutoa kiwanja hicho chenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 500 bure, kitu ambacho ni adimu kwa baadhi ya watu nchini.
 ‘’Mimi nikiwa Mwenyekiti na chama, kwa ujumla tumeamua kumuenzi marehemu Mawalla kwa kujenga hospitali hiyo eneo hilo na itaitwa jina la Nyaga,’’ alisema Mbowe.
Akimzungumzia marehemu, Mbowe alisikitishwa kutomfahamu mapema wakati wa uhai wake kwani alikuwa Wakili mwenye kipaji cha aina yake na alitaka maendeleo kwa kila mtu bila kuangalia itikadi.
Mbowe alisema Nyaga hakuwa mwanasiasa, lakini alikuwa mwanachama wa CCM na “nilijitahidi kumshawishi kuhama chama chake hicho lakini aligoma katakata.
‘’Aliniambia kuwa mimi nina roho ngumu kuwa kiongozi wa upinzani nchini, kauli ambayo niliifikiria sana hadi leo hii,’’ alisema.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania,  Francis Stolla, alisema chama hicho kimeondokewa na mtu muhimu katika fani, kwani alikuwa msaada mkubwa kwa chama na wanasheria chipukizi Tanzania, kwa kuwapa miongozo mizuri ya kazi za sheria.
Stolla alisema Nyaga alihakikisha wanasheria vijana wanasoma vyuo mbalimbali na wengine walisomeshwa naye kwa gharama yoyote ndani na nje ya nchi na alifanikisha chama hicho kupata ofisi ya uhakika.
Wakati huo huo,   Wizara ya Maliasili na Utalii imekanusha habari zilizoandikwa na gazeti la Mwananchi juzi zikidai kuwa Waziri Balozi Khamis Kagasheki ataongoza maziko ya Wakili Mawalla.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari jana iliyotolewa na Msemaji wa Wizara hiyo, George Matiko, habari hizo si za kweli na gazeti hilo linatakiwa kuzikanusha na kumtaka radhi Waziri Kagasheki.
“Waziri hakualikwa… hakuwa na mpango wowote wa kwenda Nairobi kuhudhuria mazishi hayo.
Katika kipindi kinachodaiwa na gazeti hilo, Waziri Kagasheki alikuwa Dar es Salaam akiendelea na shughuli zake za kikazi kama kawaida.
“Kwa mfano, Aprili 2 alihudhuria kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira …Aprili  3 alikuwa Dar es Salaam akihudhuria kikao cha Wizara cha Kamati ya Kusimamia, Kudhibiti na Kuratibu Mapato na Matumizi ya Serikali ambacho kilifanyika siku nzima katika ukumbi wa makao makuu ya wizara,” ilisema taarifa.

No comments: