UOKOAJI WAKAMILIKA KWA VICHWA KUOPOLEWA JENGO LILILOPOROMOKA DAR...

Wafanyakazi wakihitimisha zoezi la uokoaji jana.
Vichwa viwili vya binadamu, ni miongoni mwa miili ya watu 36 waliopatikana wakati wa uopoaji katika jengo la ghorofa 16 lililoporomoka siku ya Ijumaa Kuu, Dar es Salaam.

Akizungumza katika hitimisho la kazi ya uopoaji jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema hadi kukamilika, miili ya watu 34 ndiyo iliyokuwa imepatikana.
Kati yao, watu wazima walikuwa 30, mwanamke na watoto wanne waliokuwa wakicheza nje ya jengo hilo.
“Kuna vichwa viwili ambavyo viwiliwili vyao havionekani, kama tukikubaliana kwa dhana hiyo, waliopoteza maisha ni 36 ila miili kamili ni 34 na wengi wametambuliwa na ndugu zao na wameanza kuchukuliwa kwa ajili ya  maziko.
“Uchunguzi wa kitaalam utakapokamilika kuhusu vichwa hivi, tutawatangazia rasmi kwamba ni watu 36 ila kwa sasa nasisitiza ni watu 34,” alisema.
Alisema mpaka wanakamilisha uopoaji, majeruhi waliokuwa wamepatikana ni 18 na hadi jana wanne walikuwa bado wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kati yao, watoto ni wawili. Majeruhi wengine walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na hali zao kuimarika.
Sadiki alishukuru vikosi vilivyoshiriki uopoaji, vikiwamo vikosi vya manispaa, taasisi na mashirika mbalimbali yaliyojitolea vyakula, mitambo, magari ya kubebea wagonjwa na maiti, pamoja na mitambo ya ufukuaji wa kifusi na magari ya kubeba.
Katika hatua nyingine, Sadiki alisema wameongeza timu ya wataalam watano waliobobea katika mambo mbalimbali kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa, Polisi na Mhandisi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili kuongeza nguvu katika Kamati ya Uchunguzi, iliyoudwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB).
Alisisitiza, kwamba jengo lililo jirani na eneo hilo, bado wana shaka nalo kwa kuwa mmiliki wake ni huyo huyo mwenye jengo la ajali.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza ujenzi wake usitishwe na walio jirani na jengo hilo, wahame kwa muda kwa usalama wao hadi uchunguzi utakapokamilika.
 “Naomba tusihukumu, tusubiri vyombo husika vifanye kazi na utaratibu wa kisheria ufanyike, ninaomba wananchi waendelee kuwa na utulivu tunapolishughulikia suala hili, na tunawahakikishia kwamba hatutamwacha mtu aliyehusika na tukio hili,” alisema Sadiki.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Suleiman Kova, alisema idadi ya waliokamatwa kwa uchunguzi wa tukio hilo, imefika tisa baada ya Polisi kumshikilia mtuhumiwa mwingine ambaye ni Vedasto Ferdnand (39), mkazi wa Kimara ambaye ni Mchambuzi wa Ubora na Gharama za Ujenzi wa jengo hilo.
“Upelelezi unaendelea, ila tunawashikilia hawa kwa mahojiano zaidi, ili tuangalie kama wana makosa, ili  tuzuie mambo kama haya kutokea na watafikishwa mahakamani wakati wowote… mashauri ya watuhumiwa hawa yatapitishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema.
Alisema Polisi kazi yake ni kulinda amani na kuhakikisha sheria zinafuatwa, hivyo yuko tayari wakati wowote kutoa timu kwa ajili ya kushiriki ubomoaji wa jengo lolote, ambalo litabainika kukosa viwango.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete, alishukuru walioshiriki kusaidia uokoaji na uopoaji kwa siku nne bila kupumzika, wakiwamo askari wa vikosi, mashirika na taasisi.
“Rais alikuwa aje kuwashukuru hapa, ila amepata dharura ambayo pia ina manufaa kwetu sote, hivyo amenituma niseme kwamba Aprili 8 atakutana Ikulu kwa chakula cha mchana na walioshiriki katika shughuli hii,” alisema.
Akizungumza juzi katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Jakaya Kikwete alizilaumu mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi akisema hazikutimiza ipasavyo wajibu wao ndiyo sababu ajali hiyo ikatokea. 
“Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalumu kwenye ujenzi katika maeneo yao.  Watimize wajibu wao.  Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote,” alisema Rais. 
Hata hivyo, alisisitiza matumaini yake kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi kukamilisha mapema uchunguzi ili ukweli ujulikane.  
Pia alitoa mwito kama huo kwa Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi akitaka washirikishwe kwa ukamilifu kwa lengo hilo hilo na  hatua stahiki zichukuliwe na kuomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni.
“Wa kushitakiwa mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi,” alisisitiza.
Alitoa shukurani maalumu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na maofisa na askari wa JWTZ, na wote walioshiriki katika juhudi za uokoaji. 
“Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyingine kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa,” alisema.
Pia alitoa pole kwa waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo akiwaomba wawe na moyo wa subira huku marehemu wakiombewa wapate mapumziko mema peponi.  “Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi,” alisema Rais. 
Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Taifa, George Nangale, alisema zaidi ya vijana 50 wa kujitolea walikuwa wakifanya kazi katika eneo hilo, ambapo pia walitoa gari la kubeba wagonjwa na maiti kwa ajili ya kupelekwa Muhimbili.
Alisema chama hicho kilishiriki kutoa huduma ya kwanza na kutafuta ndugu wa waathirika wa tukio hilo, na kuwafariji na kuwataka vijana zaidi kujitolea.
Jengo hilo lilikuwa likiendelea kujengwa katika mtaa wa Indira Ghandhi na Morogoro  lilianguka Machi 29, saa 2 asubuhi ambapo kuanzia siku hiyo vikosi, mashirika na taasisi zimekuwa zikijitolea kufanya uokoaji na uopoaji na jana kazi hiyo kukamilika.

No comments: