Jerry Muro. |
Uamuzi wa hoja katika kesi ya kutaka kuomba na kupokea rushwa, iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC), Jerry Murro, unatolewa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Fauz Twaib anatarajiwa kutoa uamuzi huo, kutokana na hoja iliyowasilishwa na mawakili wa Serikali katika rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa Murro na wenzake wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo.
Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilikosea kisheria kuweka kumbukumbu ya mwenendo wa kesi hiyo.
Katika hoja zao, mawakili hao walidai kuwa Mahakama haikuandika vizuri kumbukumbu za ushahidi na vielelezo katika mwenendo wa kesi.
Walidai kuwa kuna baadhi ya ushahidi, haueleweki unamaanisha nini, jambo lililosababisha Hakimu kufikia uamuzi usio wa haki.
Akifafanua, Awamu Mbagwa alidai kuna baadhi ya vielelezo na ushahidi haupo kwenye mwenendo wa kesi, ikiwemo maelezo ya onyo yaliyotolewa na Muro katika kituo cha Polisi na kitabu cha wageni waliofika katika Hoteli ya Sea Cliff, ambavyo ni vielelezo dhidi ya mshitakiwa anayedaiwa kuomba rushwa.
Aliieleza Mahakama kuwa kitabu cha wageni kilikataliwa kupokewa mahakamani kama kielelezo, lakini katika mwenendo wa kesi haijaandikwa.
Kutokana na hali hiyo kutoandikwa katika taarifa ya mwenendo wa kesi, Mbagwa alidai hata uamuzi wa pingamizi la kielelezo hicho, haukutolewa na kudai kuwa kukosekana kwa uamuzi huo, kumesababisha Hakimu kutofikia uamuzi wa haki.
Mbali na kitabu cha wageni kukataliwa, wakili huyo alidai pia katika mwenendo wa kesi, hakuna kumbukumbu za wao kuwasilisha mkanda wa kamera inayonasa matukio (CCTV).
Aliongeza kuwa kesi hiyo awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Gabriel Mirunde, lakini Hakimu Frank Moshi ndiye aliyetoa hukumu hivyo.
Akijibu hoja, Wakili wa Muro, Richard Rweyongeza aliiomba Mahakama kutupilia mbali hoja hiyo, kwa kuwa haina misingi kisheria. Alidai Wakili wa Serikali hajaeleza ni vipi kukosewa kwa mwenendo wa kesi hiyo, kumesababisha kufikia uamuzi usio sahihi.
Washitakiwa wanadaiwa kuwa waliomba rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage kwa lengo la kuzuia kutangazwa kwenye televisheni, habari za tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma akiwa Mhasibu wa halmashauri hiyo.
Endapo Mahakama itakubaliana na hoja hiyo, kesi itarudishwa katika Mahakama ya Kisutu kusikilizwa upya.
Kama itakataliwa, rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa na mawakili wa Serikali wataendelea kutoa hoja za kupinga hukumu hiyo.
No comments:
Post a Comment