Iddi Simba. |
Kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kulisababishia Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), hasara ya Sh bilioni 2.3 inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Iddi Simba kuendelea kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jana Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta aliahirisha kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa kuwa shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi anaumwa.
Awali, Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekoma aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi leo na kuomba hati ya kumuita shahidi mwingine mahakamani kwa kuwa aliyetakiwa kutoa ushahidi anaumwa.
Mbali na Simba ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa shirika hilo, Salim Mwaking’inda na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Victor Milanzi.
Wanatuhumiwa Septemba 2, 2009 jijini Dar es Salaam, Simba na Milanzi walikula njama ya kuchepusha fedha na kughushi barua, wakionesha kuwepo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za UDA Ltd.
Aidha, wanadaiwa walichepusha Sh milioni 320 wakijifanya ni malipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo, fedha ambazo wanatuhumiwa walijipatia kutokana na nyadhifa zao.
Inadaiwa Simba na Mwaking’inda wakati wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya nafasi zao, wakaharibu hisa milioni 7.8 zisizotumika za UDA, Shirika linalomilikiwa kati ya Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, kesi ya matumizi mabaya ya Ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja imeahirishwa hadi Mei 28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment