Makao Makuu ya Tanesco yaliyoko Ubungo, Dar es Salaam. |
Shirika la Umeme (Tanesco) limetajwa kuzidiwa na mzigo wa kazi, kutokana na kuzalisha, kusambaza umeme na kukusanya mapato peke yake.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesema shirika hilo sasa ni ajenda kuu ya Serikali, ambayo imeanza mchakato wa kukusanya maoni ni nini kifanyike kuliboresha.
“Kwa kweli kwa sasa kama Serikali,Tanesco ndiyo ajenda yetu kuu, tumeanza mchakato wa
kukusanya maoni kwa wadau mbalimbali wakiwemo wasomi juu ya nini kifanyike ili kuboresha shirika hili,” alisema Simbachawene.
Simbachawene alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyeitaka Serikali iangalie uwezekano
wa kuvunja shirika hilo au lipatiwe mtu mwingine wa kuliendesha, akisisitiza kwamba pamoja na kuzalisha umeme mdogo, limeshindwa kukusanya mapato yake.
Pamoja na swali hilo la nyongeza, mbunge huyo alitaka kufahamu pia ni kwa nini agizo la Rais la kutaka wananchi wa Somanga wafungiwe umeme, halijatekelezwa hadi sasa.
Naibu Waziri alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha utendaji wa chombo hicho, unakuwa wa ufanisi bila kujali ni nani analiendesha. “Uamuzi wa suala hili utategemea zaidi maoni haya ya wadau na wataalamu kwa ujumla,” alisema Simbachawene.
Kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Rais ya umeme kwa wananchi wa Somanga, alisema Sh milioni 290 zimekadiriwa kutumika katika kupeleka umeme kwenye vijiji saba vya Kilwa Kaskazini.
Alitaja vijiji hivyo vitakavyopelekewa umeme ni Banduka, Mtandago, Miteja, Sinza, Puyu, Matandu na Njenga.
Simbachawene alisema fedha hizo zitajumuisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 0.4 yenye kilometa 15.5, ufungaji wa transfoma saba zote za kVA 50 na kuunganishia umeme wateja wapatao 225.
Aliwashauri wananchi wa Somanga Fungu kuanza kupeleka maombi Tanesco Kilwa Masoko ya kuwekewa umeme.
Hoja kuhusu utendaji wa Tenesco imekuja huku mchakato wa kufanya mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji ukiendelea kwa lengo la kuboresha huduma kwa wateja.
Shirika kupitia ofisi yake ya Mawasiliano, lilishatoa matangazo kwa wadau wa sekta ya nishati ya umeme, kushiriki katika kutoa maoni ni namna gani wangependa Tanesco mpya iwe ili kusaidia kuleta mabadiliko yatakayoboresha kutekeleza majukumu yake ya kuhudumia wateja.
Licha ya kusambaza anuani za barua pepe, simu na mtandao wa kijamii wa facebook, Tanesco katika matangazo yake, ilisema wafanyakazi wake watapita katika maeneo wakigawa dodoso fupi kama njia ya kukusanya maoni.
No comments:
Post a Comment