OMBI LA KUSIKILIZWA UPYA KESI YA JERRY MURO LATUPWA...

Jerry Muro.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali ombi la kusikilizwa upya kwa kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 10, iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji (TBC), Jerry Muro na wenzake.

Jaji Fauz Twaib alitoa uamuzi huo jana, bila kusema sababu za kukataa ombi hilo lililowasilishwa na Upande wa Mashitaka katika rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa washitakiwa hao.
Alisema atatoa sababu za kukataa ombi hilo wakati akisoma uamuzi wa rufaa hiyo baada ya kusikiliza hoja nyingine tatu za upande wa mashitaka. Aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 3 mwaka huu.
Katika maombi, upande wa mashitaka ulitaka Mahakama kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya, kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kisheria kuweka kumbukumbu ya mwenendo wa kesi hiyo.
Walidai kuwa Mahakama haikuandika vizuri kumbukumbu za ushahidi na vielelezo katika mwenendo wa kesi, pia baadhi ya ushahidi haueleweki unamaanisha nini, jambo lililosababisha Hakimu kufikia uamuzi usio wa haki.
Aidha, walidai kuna baadhi ya vielelezo na ushahidi haupo kwenye mwenendo wa kesi, ikiwemo maelezo ya onyo yaliyotolewa na Muro katika kituo cha Polisi na kitabu cha wageni waliofika katika Hoteli ya Sea Cliff, hakuna kumbukumbu za wao kuwasilisha mkanda wa kamera, inayonasa matukio (CCTV) ulioonesha washitakiwa walipokwenda kufanya makubaliano.
Aliongeza kuwa kesi hiyo, awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Gabriel Mirunde, lakini Hakimu Frank Moshi ndiye aliyetoa hukumu hivyo kutokana na kumbukumbu za mwenendo wa kesi kutokuwa vizuri, Hakimu huyo alifikia uamuzi usio sahihi.
Washitakiwa wanadaiwa kuwa waliomba rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage kwa lengo la kuzuia kutangazwa kwenye televisheni, habari za tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma akiwa mhasibu wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi alikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Novemba 30 mwaka juzi na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Frank Moshi ambayo ilimwachilia huru Muro, Deogratius Mgasa na Edmund Kapama.

No comments: