Godbless Lema. |
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa, akituhumiwa kuchochea kutenda kosa na kusababisha uvunjifu wa amani.
Lema alifikishwa mahakamani jana, chini ya ulinzi mkali mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Msofe, na kusomewa mashitaka na Mwanasheria wa Serikali, Eliaine Njiro.
Njiro alidai mahakamani hapo kuwa Aprili 24, Lema alitenda kosa hilo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai sura namba 16 na marejeo ya 2002.
Akisoma maelezo ya mashitaka hayo, Njiro alidai kuwa Aprili 24 katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Lema alitamka maneno yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
Alidai kuwa Lema alisema Mkuu wa Mkoa anakuja kama anakwenda kwenye ‘send off (sherehe ya kuaga bibi harusi)’ na hajui mahali chuo hicho kilipo.
Pia anadaiwa kusema kuwa Mkuu wa Mkoa alishindwa kuwapa pole wanafunzi hao kwa kufiwa na mwenzao na hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu na kuwa hakuwasaidia kutokana na matatizo yao.
Baada ya kusomewa mashitaka, Lema alikana na Mwanasheria huyo kudai kuwa dhamana kwa mshitakiwa iko wazi na wao Serikali hawana pingamizi kwani upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Mawakili wa Lema, Method Kimomogoro na Humphrey Mtui, waliiomba Mahakama imwache mteja wao kwa dhamana, ikiwezekana ajidhamini mwenyewe.
Wakili Kimomogoro katika ombi hilo, alidai kuwa maelezo ya mashitaka yanayomkabili Lema, hayaonekani kama ni kosa na kwa kuwa ni Mbunge na kiongozi mwenye dhamana, hawezi kutoroka.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Msofe alisema dhamana kwa mshitakiwa iko wazi kwa masharti ya kudhaminiwa na mdhamini mmoja kwa Sh milioni moja. Diwani wa Viti Maalumu Chadema, Sabina Francis alimdhamini Lema.
Msofe alisema Mahakama ilimwacha Lema kwa dhamana na shauri hilo litatajwa Mei 29.
Nje ya Mahakama, wafuasi wa chama hicho walikuwa wamejaa kuanzia saa mbili kasorobo asubuhi, wakisubiri hatma ya Mbunge wao, huku polisi wakiimarisha ulinzi mkali mahakamani na maeneo kadhaa ya jiji hilo.
Hatimaye baada ya kupata dhamana, Lema aliondoka katika viwanja vya Mahakama hiyo kwa maandamano na wafuasi wa chama hicho, hadi ofisi za Chadema mjini hapa.
“Niliwaambia nikitoka Polisi lazima nifanye hivi. Nashukuru vyombo vya habari, nawashukuruni sana kwani nilikuwa nikisoma taarifa na hamkuweka chumvi wala kuegemea upande wowote, kuhusu kukamatwa kwangu,” alisema.
No comments:
Post a Comment