BAJETI WIZARA YA MAJI YAPIGWA JEKI SHILINGI BILIONI 185...

Waziri wa Fedha, William Mgimwa.
Baada ya wabunge kugomea bajeti ya Wizara ya Maji kutokana na ufinyu wake, Serikali imekubali kuiongeza Sh bilioni 184.5.

Kutokana na nyongeza hiyo kwa ajili ya sekta ndogo ya maji vijijini, vijiji 840 nchini kote vitatekeleza miradi yao ya maji.
Jana asubuhi kabla ya majumuisho ya hoja ya Wizara ya Maji, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, alitoa kauli ya Serikali kwa maneno, kwamba imekubali mapendekezo ya Kamati ya Bajeti ya Bunge na kuongeza Sh bilioni 184.5.
Alisema hatua hiyo ya Serikali, ilifikiwa baada ya majadiliano kati ya Kamati ya Bajeti ya Bunge, Wizara ya Maji na Wizara ya Fedha.
Baada ya kauli hiyo ya Serikali, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alisema utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, utafanya idadi ya watu watakaopata maji nchini hadi mwakani, kufikia asilimia 62.
Hata hivyo, baada ya majumuisho, wabunge wa upinzani walisimama na kutaka Bunge lisiketi kama Kamati, mpaka kanuni za uendeshaji Bunge zitakapozingatiwa.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,  Kabwe Zitto (Chadema), alizungumzia haja ya kuwapo kwa waraka rasmi wa Serikali kuhusu nyongeza hiyo.
Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Tundu Lissu (Chadema), aligusia zaidi kanuni huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), akitaka Bunge liahirishwe mpaka taarifa rasmi ya Serikali itakapoletwa pamoja na majedwali ya mabadiliko.
Zitto alisema historia inaonesha, kwamba bila waraka, makubaliano hayatekelezeki akitolea mfano umeme vijijini na bajeti ya nyongeza ya Wizara ya Uchukuzi.
Spika Anne Makinda, alikubaliana na hoja hizo na kutoa nafasi kwa Serikali kufanya mabadiliko yanayotakiwa, kabla ya Bunge kukaa kama Kamati jioni. Alisema kama wabunge wasingehoji kuhusu kanuni, angewashangaa.
Wiki iliyopita, kabla ya Waziri Maghembe kurudishwa kufanya marekebisho ya Bajeti ya Wizara yake,  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Said Mkumba, alisema Kamati hiyo haikuridhishwa na kiasi cha bajeti kilichopendekezwa.
Alishauri Serikali angalau itafute fedha za ziada, kama
Sh bilioni 185, ili zipelekwe kwenye miradi ya maji na kupunguza tatizo la maji hasa vijijini.
Pamoja na Kamati hiyo ya  Bunge kueleza kutoridhishwa na bajeti hiyo, wabunge wengi waliochangia bajeti hiyo, waliigomea na kuitaka Serikali kuongeza fedha, kwani hali haikuwa njema.
Majadiliano makali bungeni bila kujali vyama Jumatano na Alhamisi iliyopita yalimfanya Spika Makinda kuahirisha Bunge na kutaka Kamati ya Bajeti ya Bunge, kukutana na Serikali kuboresha bajeti hiyo.
Awali Serikali katika bajeti hiyo, iliomba iidhinishiwe matumizi ya Sh bilioni 398.39, kati ya hizo, matumizi ya kawaida  Sh bilioni 18.95 na Sh bilioni 13.31 ikiwa ni za mishahara ya
watumishi  na Sh bilioni 5.6 matumizi mengine.
Bajeti ya Maendeleo iliyoombwa ilikuwa Sh bilioni 379.44, kati ya hizo Sh bilioni 138.26, fedha za ndani na Sh bilioni 241.17  za nje.

No comments: