ALIYENUSURIKA AJALI GHOROFA LILILOPOROMOKA ASIMULIA MKASA MZIMA...

Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Salma wakimjulia hali Mohammed Ally Bhamji, mmoja wa majeruhi wa ajali ya jengo lililoporomoka Ijumaa iliyopita Barabara ya Morogoro na Indira Ghandhi, Dar es Salaam, walipomtembelea Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) jana. (Picha na Ikulu).
Mmoja wa majeruhi  katika jengo la ghorofa 16 lililodondoka katika Mtaa wa Indira Ghandhi juzi jijini Dar es Salaam,  ameelezea jinsi alivyonusurika kifo katika ajali hiyo akiwa ghorofa ya 15.

Selemani Said (26) ambaye ni miongoni mwa majeruhi wanne waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) anasema wakati akiwa gorofa ya 15 alishuhudia jengo lilivyokuwa likianza kushuka.
Majeruhi huyo ambaye ni fundi ujenzi, alisema wakati ajali hiyo ikitokea asubuhi, alishuka na jengo hilo hadi chini na baada ya hapo, alipoteza fahamu na kushtukia akiwa hospitali.
“Siku ile ilikuwa ni siku ya kumwaga zege. Tulikuwa wengi wakiwemo vibarua ambao jengo linapofikia hatua ya kumwaga zege, huwa linahitaji vibarua wengi, nikiwa najiandaa kuanza ujenzi, mara nilihisi kama jengo linaanguka, nilipoangalia nje niliona ninashuka nalo,” alisema Said.
Alisema anachokumbuka ni kwamba wakati likishuka,  huku kukiwa na kelele za watu wakiomba msaada, alishtukia akirushwa nje kupitia dirishani na baada ya hapo hakujua chochote hadi alipozinduka akiwa hospitalini.
Majeruhi huyo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tiba MOI, Dk Cuthbert Mcharo, amevunjika pingili mbili za uti wa mgongo lakini kwa bahati miguu yake inafanyakazi vizuri kama kawaida.
Aidha Dk Mcharo, alisema pamoja na majeruhi huyo, taasisi hiyo  mara baada ya ajali ilipokea majeruhi sita, wawili kati yao wametibiwa na kuruhusiwa huku wanne wakiendelea na matibabu.
Alisema kati ya majeruhi hao, wapo wawili ambao wana umri chini ya miaka 10 ambao wanadaiwa kuwa walikuwa wakicheza pembeni ya ghorofa hiyo. Mmoja wa watoto hao, amevunjika miguu yote na mwingine amepata matatizo ya mgongo.
Watoto hao waliolazwa katika wodi za Moi,  ni Mohammed Ally na Bakhir Hassan ambao wote hali zao zinaendelea vizuri na wanazungumza.
Aidha daktari huyo, alisema majeruhi mwingine aliyelazwa pamoja na Said katika wodi ya Sewahaji, Yusufu Abdallah  amepata matatizo ya nyonga  na alikuwa anaweweseka.
Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete, walitembelea wagonjwa hao na kuwafariji huku Rais akiwaahidi kuwa watapatiwa matibabu na huduma zote wanazohitaji hadi pale afya zao zitakaporejea kama kawaida.
“Tumekuja kuwafariji na kuwapa pole na matatizo yaliyowapata, poleni sana Mungu awatie nguvu, msijali mtapata huduma bora kabisa mpaka pale hali zenu zikapotengemaa,” aliwahakikishia Rais Kikwete.

No comments: