WALIOKUFA JENGO LILILOPOROMOKA DAR SASA WAFIKIA 22...

Jengo hilo lililokuwa na ghorofa 16 baada ya kuporomoka juzi.
Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linamshikilia mmiliki wa kampuni ya Lucky inayodaiwa kujenga ghorofa lililoanguka juzi, na kuhofiwa kuua watu zaidi ya 60 wakiwemo watoto wanne, maiti zaidi wameendelea kunasuliwa kutoka kwenye kifusi.

Jengo hilo lililopo katika mtaa wa Indira Gandhi na Barabara ya Morogoro jijini Dar es Saam, liliporomoka juzi saa 2.30 asubuhi.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana ilisema inawashikilia Mmiliki wa Kampuni ya Ujenzi,  Ibrahim Kisoki na Mhandisi mshauri, Zonazea Bushudada baada ya kujisalimisha.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova  alisema jana kuwa watu hao walijisalimisha wenyewe mchana kwa nyakati tofauti katika Kituo Kikuu cha Polisi baada ya Polisi kutoa saa 12 wawe wamejisalimisha.
Kisoki ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi, Kata ya Goba Wilaya ya Kinondoni. Kwa pamoja wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na jengo hilo.
Kamanda Kova alisema zoezi la kutoa watu walioangukiwa na jengo hilo zinaendelea.
Taarifa zilizopatikana hadi jana usiku zimekwishatolewa maiti 22 ambazo zimehifadhiwa katika Hospitali  ya Taifa Muhimbili.
“Maiti wamehifadhiwa Muhimbili na pia majeruhi wanapata matibabu katika hospitali hiyo na  mpaka sasa watu kumi wanaendelea na matibabu, watatu hali zao si nzuri na wengine watano wameruhusiwa baada ya hali zao kuendelea vizuri,” alisema Kamanda Kova.
Viongozi mbalimbali wameendelea kufika katika eneo hilo kuangalia namna kazi hiyo  ya uokoaji inavyoendelea na pia kutoa pole kwa watu ambao wamepoteza jamaa zao katika ajali hiyo, ikiwa ni pamoja na waliofiwa na watoto wao ambao walidondokewa na jengo hilo wakiwa wanacheza.
Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni miongoni mwa viongozi ambao walifika mapema jana,  ambapo Rais alitoa agizo la kukamatwa kwa wahusika wa jengo hilo na hatua kali zichukuliwe dhidi yao. Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema kazi ya uokoaji inayoendelea ili kutoa miili ya watu inaanza kuwa ngumu kutokana na kuzuiliwa na nondo na hivyo wameomba msaada kwa kampuni ya kichina kuja kutoa msaada wa kukata nondo hizo.
“Jambo jingine linalochelewesha hapa na kufanya zoezi hilo kwenda polepole ni kujitahidi kuondoa kifusi kwa ustaarabu ili tusiharibu miili tunayoiokoa kwa sababu uwezekano wa kutoa watu wakiwa hai tena ni mdogo sana, ni vema itoke katika hali nzuri bila kuikata kata,” alisema Sadiki akiendelea kusimamia uokoaji huo.
Alisema kazi hiyo ilifanyika usiku wote na kuna baadhi ya miili ilitolewa usiku, ikiwa ni pamoja na watoto wawili wenye asili ya Kiasia.
Sadiki aliendelea kusisitiza watu wanaoishi pembeni mwa jengo ambalo pia linamilikiwa na mmiliki wa jengo lililoanguka, na pia linajengwa na mkandarasi huyo huyo kujitahidi kuondoka mpaka pale litakapokaguliwa kwa sababu nalo lina viashiria kuwa haliko salama kutokana na nyufa kadhaa zinazoonekana.
Alisema jengo hilo likionekana kuwa halina ubora na wakaguzi wakithibitisha hilo, litaamriwa kubomolewa mara moja kwa ajili ya usalama wa watu.
“Wahandisi na makandarasi wakifanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na weledi, haya hayawezi kutokea, hatuwezi kuendelea kuangalia usanii huu wa Bongoland …. Si kwamba hawajui nini wanafanya hii ni haramu,” alisema kwa hasira Sadiki.
Alisema kampuni zenye vibali zinachukua kazi kwa ajili ya kujipatia fedha tu na baada ya hapo kukabidhi kazi kwa mafundi wasiokuwa na ujuzi unaostahili ambao hujenga bila kufuata sheria, huku akionesha jengo hilo kuwa halikuwa na zege, bali ni mchanga na kiwango kidogo cha saruji.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa pamoja na Kamanda Kova hawakuweza kubainisha zoezi hilo la uokoaji ni lini linatarajiwa kukamilika ingawa Sadiki alisema anafikiri lingeweza kukamilika jana.
Multarali Damji ni miongoni mwa watu ambao wana majonzi baada ya kuondokewa na mjukuu wake, Salman Damji anasema pamoja na kwamba mmiliki wa jengo hilo ni ndugu yake, hatua kali zichukuliwe dhidi yake na kwamba Serikali imuamuru kutoa fidia kwa wafiwa wote.
Mohamed Karim ni mzazi ambaye watoto wake wawili walikuwa wakicheza katika uwanja wa mpira uliokuwa jirani na jengo hilo, kwa bahati mbaya mtoto mmoja amekufa huku mmoja akiokolewa akiwa hai baada ya kuona vumbi linaanza kutimka.
“Watoto walikuwa wakicheza hapo nje wametengeneza timu za watoto wanne wanne, wakati wengine wakicheza, wanne walikaa pembeni wakiwaangalia, jengo lilipoanza kuanguka waliokuwa wakicheza walibahatika kukimbia lakini waliokuwa wamekaa wote wanne wamefia humo akiwepo mtoto wangu,” alisema Karim kwa majonzi.
Alisema eneo hilo walitengeneza uwanja ambao watoto walikuwa wakija kusali asubuhi na baada ya swala hutumia uwanja kucheza kila siku za Sikukuu na siku ambazo walikuwa hawaendi. Mtoto Shuhid Abbas Kanji mwili wake haujapatikana.

No comments: