BENKI YA DUNIA YATOA BILIONI 120 KUSAIDIA BAJETI TANZANIA...

Ramadhan Khijjah.
Shilingi bilioni 120 zimetolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia Bajeti  ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha itakayosomwa mwezi Juni mwaka huu.

Fedha hizo ambazo ni mkopo zitaelekezwa kwenye uboreshaji wa mifumo ya udhibiti wa fedha za umma  pamoja na uboreshaji wa sekta za uwekezaji katika maeneo ya vipaumbele vya nchini.
Kiasi hicho ni sehemu ya fedha zinazochangwa na wahisani ambao wanachangia katika bajeti ya Serikali (GBS) ambako Benki ya Dunia ni miongoni mwa wahisani 11 wanaosaidia bajeti ya Tanzania.
Fedha hizo katika mwaka ujao wa fedha zitaelekezwa katika utekelezaji wa kupunguza umasikini, Mkukuta II na kusaidia Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (FYDP I).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijjah alisema  "Wahisani kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Tanzania kunadhihirisha kuwa wameridhika na mpango wa ushirikiano uliopo kati ya Serikali na sekta binafsi...Tunaamini kuwa tutafanikiwa kutekeleza mipango yote hii kwani ajenda zetu za maboresho zinakubalika," alisema  Khijjah.
 Fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kuboresha maeneo matano ambayo ni upanuzi na uwazi katika kukusanya mapato ya ndani ya Serikali na uboreshaji wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Pia ni kwa ajili ya kuweka mifumo mizuri katika uandaaji wa bajeti ya Serikali, kuanzisha taasisi ambayo itaratibu shughuli zinazofanywa katika maeneo huru ya kiuchumi na kuboresha maeneo yanayohitaji uwekezaji.
Benki hiyo pia imesisitiza  maeneo hayo ni muhimu kwani yanasaidia juhudi za Serikali katika kuinua uchumi wa jumla na kuweka mifumo sahihi na endelevu ya kifedha  kwa manufaa ya uchumi wa nchi na uendelezaji wa miundombinu.
Aidha benki hiyo inaamini kuwa uboreshaji wa maeneo hayo utasaidia nchi kujenga misingi imara ya kiuchumi na kutumia maeneo ya kijiografia yenye rasilimali hizo kwa manufaa ya nchi nzima.
Mkurugenzi wa Kupunguza Umasikini na Uchumi Kanda ya Afrika, Marcelo Giugale alisema uwazi katika bajeti ni jambo la msingi hasa katika eneo la nishati.
“Upatikanaji wa taarifa sahihi, umma kupata takwimu kwa muda na wakati  iwe ni kipaumbele kwa watunga sera.  Uwazi huo uende pia katika eneo la ukusanyaji wa mapato yanayotokana na gesi asilia na madini," alisema Giugale .
Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekubali mpango wa kuwepo kwa uwazi katika sekta ya ugagaduaji (EITI) na imedhamiria kuweka wazi mapato yote yanayotokana na gesi, madini pamoja na mafuta.
Mpango huo unaamini kuwa kuwepo uwazi katika sekta hiyo katika nchi mbalimbali kutazidisha imani kati ya wananchi na Serikali inayoratibu mapato yanayotokana na rasilimali za asili.
 Utoaji wa fedha hizo katika eneo hilo kunafanya fedha ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia katika kuboresha mapato yanayotokana na rasilimali za asili kufikia Sh bilioni 160.

No comments: