MTOTO ACHOMWA MOTO MBEYA KWA KUIBA SHILINGI 500...

Kamanda Diwani Athumani.
Mtoto aliyefahamika kwa jina la Zidane Mbembela (13) amejeruhiwa vibaya kwa kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili wake akituhumiwa kuiba Sh 500 mali ya familia yao.
Wazazi wa mtoto  huyo akiwemo  baba yake Zawadi Mbembela (33) na mama yake wa kambo Pendo Mwampashi (29) wote wakazi wa kitongoji cha Masele katika  kijiji cha Katete wilayani Momba ndiyo waliotajwa kutenda ukatili huo.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athuman alisema tukio hilo limetokea  Februari 19 saa 10:00 jioni na kueleza kuwa tayari watuhumiwa wamekamatwa na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi.
Alisema wazazi hao baada ya kuhisi kuibiwa shilingi 500 walichukua uamuzi wa kumkamata na kuanza kumchoma kwa moto wa jiko la kuni na kumjeruhi vibaya  mtoto Zidane.
Aliyataja maeneo yaliyopata majeraha makubwa kuwa ni pamoja na kiganja cha mkono wa kulia, kiwiko na vidole vya mkono huo.
Tukio hilo linalokiuka haki za watoto limetokea ikiwa ni siku chache kupita tangu mahakama ya hakimu mkazi mkoani hapa kumhukumu kifungo cha maisha mwanamke mmoja aliyeshitakiwa mahakamani hapo kwa kumnyanyasa mtoto aliyekuwa akimlea ikiwemo kumvunja mkono pasipo kumpeleka hospitali, hali iliyolazimu madaktari kuukata kwa kuwa ulioza.

No comments: