WANAFUNZI WAJINYONGA BAADA YA KUFELI KIDATO CHA NNE...

Matokeo ya kidato cha nne  mwaka huu, yamesababisha maafa katika familia kutokana na wanafunzi waliojinyonga hadi kufa mkoani Dar es Salaam na Tabora, kwa  kutoridhishwa na matokeo.
Mwanafunzi Barnaba Venant (18) aliyehitimu sekondari ya Debrabant iliyoko Temeke, alijinyonga kwa kamba ya manila na kufa kutokana na kutoridhika na kupata daraja la nne kwa alama 27.
Barnaba ambaye alikuwa akiishi Nzasa Temeke, alijinyonga juzi saa 4 asubuhi ndani ya nyumba yao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, kijana huyo alikutwa amejinyonga akitumia kamba ya manila aliyoitundika darini.
Kamanda alisema katika uchunguzi wa awali walibaini kwamba kijana huyo alijinyonga baada ya kutoridhishwa na matokeo yake. Mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Temeke huku polisi wakiendelea na upelelezi.
Kwa upande wa Tabora, mwanafunzi aliyejinyonga alihitimu sekondari ya Kanyenye mjini humo.
Akizungumza na waandishi wahabari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Ruta alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Michael Fidelis (19) ambaye ni mkazi wa  eneo la Skanda katika mtaa wa Mwinyi kata ya Chemchemi katika manispaa ya Tabora.
Alisema mwanafuzi huyo aliyepata daraja la sifuri alikwenda kuangalia matokeo yake saa 11 jioni Februari 18 na kukutwa baadaye amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia kamba ya manila.
Kamanda Ruta alisema aliacha ujumbe uliosomeka: “Nisamehe sana mama, usitafute mchawi, nakupenda sana, uamuzi niliochukua ni sababu ya matokeo mabaya, nakutakia maisha mema.”
Mkuu wa Sekondari ya Kanyenye alipokuwa akisoma mwanafunzi huyo,  Kapufi Patson alisema Michael alikuwa mpole na mtaratibu na walishangazwa na uamuzi aliochukua wa kujinyonga.
Akielezea nafasi ya mwanafunzi huyo kitaaluma,  Mkuu wa Shule alisema katika mtihani wa majaribio mwaka jana, alipata daraja la nne kwa alama 33.
Matokeo ya sekondari hiyo yanaonesha kuwa hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza na pili. Waliopata daraja la tatu ni wawili, daraja la nne ni 14 na wanafunzi 85 walipata sifuri. Wanafuzi 36 matokeo yao hayakutoka kwa sababu walikuwa wanadaiwa ada ya mtihani.
Taarifa kutoka kwa rafiki wa kijana huyo ambaye maziko yake yalifanyika juzi, zilisema awali alipigiwa simu na kaka yake aishiye Mbeya kumwambia kwamba matokeo yametoka.
Walisema wakiwa kwenye intaneti, kijana huyo ambaye ni wa kwanza kuzaliwa kwa mamake, alionekana amenyong’onyea.
“Aliporudi nyumbani alinyong’onyea zaidi. Hakusema chochote. Kumbe alipotoka hapo alikwenda kujinyonga,” alisema mmoja wa watu waliokuwa naye.
Kwa mujibu wa ndugu zake, kijana huyo alikuwa akiishi na ndugu zake nyumba tofauti na mama yake ambaye alishaachana na baba yake mzazi na kuolewa na mume mwingine.
Ilielezwa kuwa alikuwa na kawaida ya kula usiku nyumbani kwa mama yake. Lakini usiku huo hakuonekana na ilipofika saa 3 usiku walikwenda na kukuta amejifungia ndani wakavunja mlango na kukuta amekufa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alitangaza matokeo hayo Jumanne ambapo alibainisha kwamba zaidi ya nusu ya watahiniwa walipata daraja la sifuri.
Kati ya wanafunzi 397,136 waliofanya mtihani huo, 240,903 walipata sifuri. Waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la pili ni 6,453, la tatu ni 15,426 na la nne ni 103,327.

No comments: