MABINTI WATATU WA FAMILIA MOJA WABAKWA NA KUUAWA...

Mabinti watatu kutoka kijiji kimoja kidogo nchini India wamebakwa na kuuawa kabla ya miili yao kutupwa kwenye kisima, imefahamika.
Wasichana hao watatu - wenye umri wa miaka 11, tisa na sita - walitoweka Siku ya Valentine kutoka kijiji chao fukara cha Murmadi mjini Lakhni Tehsil baada ya kutoka shuleni.
Miili yao ilikutwa kwenye kisima siku nne baadaye karibu na mji wao ulioko wilaya ya Bhandara - ambao uko kilomita 65 tu kutoka jiji la Nagpur.
Ilidaiwa kwamba madada hao watatu - ambao walikuwa wakiishi katika lindi la umasikini - walichukuliwa na mgeni kwa ahadi ya kupatiwa chakula.
Mauaji hayo ya kutisha yamekuja baada ya mwanafunzi mwenye miaka 23 kubakwa kikatili ndani ya basi mjini New Delhi na kufariki siku 13 baadaye kutokana na majeraha makubwa.
Mashambulio hayo ya kikatili yamelipua maandamano nchi nzima huku wananchi wakitaka kuimarishwa ulinzi kwa wanawake.
Mauaji hayo 'mabaya' ya hivi karibuni yanaweza kuanzisha kampeni kukomesha mashambulio ya ubakaji wa kutumia nguvu kote katika eneo hilo.
Jamii ya mahali hapo tayari imelaani kuhusu shambulio hilo.
Waziri Mkuu Prithviraj Chavan alisema: "Tukio hilo linasikitisha sana na kuumiza mno. Nawataka watu kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya sheria."
Babu wa wasichana hao - ambaye hawezi kutajwa kwa sababu waathirika wa ubakaji hawatakiwi kutajwa chini ya Sheria ya India - anaamini madada hao walitoroshwa na mtu asiyefahamika kwa ahadi ya chakula, imeripotiwa na NDTV.
Baba wa madada hao alifariki miaka minne iliyopita na familia hiyo imekuwa ikihangaika kupata riziki kutokana na ujira mdogo anaolipwa mama yao kama kibarua.
Wanakijiji tayari wameshutumu polisi kwa jinsi wanavyoshughulikia kesi hiyo - wakidai walijaribu kuthibitisha kwamba vifo hivyo vilitokea kama ajali tu.
Waziri wa Muungano Praful Patel, ambaye anawakilisha Maharashtra katika Bunge, alimtembelea mama wa wasichana hao watatu katika nyumba yake.
Aliileza NDTV: "Kama baba wa wasichana hao watatu, nashitushwa na ukatili uliofanywa kwa wasichana hawa. Nimefikisha suala hili kwa waziri mkuu kuhakikisha msaada wa kifedha kwa mjane huyo, uchunguzi wa kasi na kesi katika mahakama maalumu dhidi ya wahusika."
Patel amemtaka Waziri Mkuu Prithviraj Chavan kutenga msaada maalumu wa kifedha kwa mjane huyo, limeripoti gazeti la the Times of India.
Timu kubwa tano za uchunguzi zimeundwa kuwasaka watuhumiwa na donge nono la Rupia 50,000 limetangazwa kwa taarifa yoyote itakayowezesha kukamatwa - kiasi ambacho kinakaribia Pauni za Uingereza 600.
Baadhi ya wafanyakazi wa ujira wa kawaida nchini India hulipwa kiasi kidogo hadi kufikia Pauni za Uingereza 35 kwa mwezi. Lakini wengi wasio na chochote wanapokea kiasi hicho.

No comments: