LOWASSA AWEKA SAWA SUALA LAKE LA KUENGULIWA UVCCM...

Edward Lowassa.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema aliomba kutoendelea na uenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya kuona ndoto zake zimetimia kutokana na umoja huo kujitegemea.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Lowassa alisema aliwaambia viongozi wa umoja huo kuwa asingependa kuendelea na wadhifa huo aliodumu nao kwa zaidi ya miaka 10.
Katika kikao chake cha hivi karibuni Dodoma, Baraza Kuu la Umoja  wa Vijana, lilimteua Waziri wa Mambo ya Ndani Dk  Emmanuel Nchimbi kuwa Mwenyekiti wa Baraza kuziba pengo la Lowassa.
Hatua hiyo ilitafsiriwa na kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kama ni kumwengua mwanasiasa huyo aliyepata kuwa Waziri Mkuu.
“Niliwaambia nisingependa kuendelea, baada ya kufanikisha ndoto yangu ya kuona Umoja wa Vijana unajitegemea, nisingependa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini,” alisema Lowassa.
Miongoni mwa mambo anayojivunia kuyafanikisha UVCCM, ni pamoja na ujenzi wa jengo la kitega uchumi la umoja huo lililoko Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam.
“Umoja wa Vijana hivi sasa una mradi mkubwa kabisa, jengo lile pale, la pili kwa urefu nchini, haya ni mafanikio makubwa kabisa, zamani walisema kulikuwa na harufu ya rushwa kwenye mkataba ule, lakini hakuna mkataba bora kama ule,” alisema.
Aliendelea: “Umoja wa Vijana watakuwa wakilipwa dola 50,000 kwa mwezi.” Kwa mujibu wake, fedha hizo zitaufanya umoja kujilipa mishahara na  gharama zingine.
Alisema kutokana na mkataba ambao umoja huo ulisaini na kampuni ya Espirit Developer Limited ya  Dar es Salaam  kujenga jengo hilo, sasa Umoja huo unajitegemea na kuufanya uwe na jengo kubwa kuliko hata CCM yenyewe.
“Najivunia sana mafanikio haya makubwa, hii ndiyo ilikuwa ndoto yangu, nawashukuru sana wajumbe wenzangu, Baraza limefanya kazi nzuri sana, nawashukuru vijana waliotuamini na sasa wanaona mafanikio yale,” alisema.
Miongoni mwa watu waliosema mkataba huo ulikuwa na harufu ya rushwa, ni pamoja na Nape Nnauye ambaye sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.
Lowassa katika mazungumzo aliendelea kusisitiza, “Nimetimiza ndoto yangu ya kuona umoja ule unakuwa mfano kwa jumuiya nyingine,” nawaomba wanielewe, kuwa mimi ni mtumishi nisiye na faida, nimefanya yale tu yaliyonipasa kuyafanya”.
Umoja wa Vijana katika mkataba huo, kwa kuanzia utakuwa ukipata dola  50,000 kwa mwezi, mpaka jengo litakapojaa wapangaji.
Aidha, Lowassa alisema katika mkataba huo, jengo la zamani lililokuwa makao makuu ya umoja  huo litavunjwa na kujengwa jipya.

No comments: