Baadhi ya magari yaliyochomwa moto wakati wa vurugu za Mtwara hivi karibuni. |
Serikali leo inatarajiwa kutoa msimamo wake kuhusu vurugu zilizoibuka na hatua zitakazochukuliwa ili kurejesha utulivu mkoani Mtwara.
Hatua hiyo inakuja baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, juzi na jana kwa kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi mkoani humo.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, zilisema leo ndiyo siku Pinda atakayotoa majumuisho ya ziara yake hiyo Mtwara.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kuliibuka vurugu zilizosababisha vifo huku zikihusishwa na mgogoro wa gesi asilia na kusababisha Pinda afanye ziara ya ghafla ya siku mbili.
Katika ziara hiyo iliyoanza juzi na kutarajiwa kumalizika leo, Pinda alikutana na makundi ya kijamii kusikiliza maoni yao kuhusu sakata hilo.
Kabla ya makundi hayo, Pinda alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujadili hali halisi ambapo baadaye alikutana na viongozi wa dini na wazee.
Makundi mengine ambayo alikutana nayo mpaka jana jioni ni madiwani na wabunge wa Mtwara, vyama vya siasa vya upinzani na baada ya chakula cha mchana alitarajiwa kukutana na viongozi wa CCM na wafanyabiashara.
Taarifa za uhakika zilizopatikana jana jioni, zilieleza kuwa vikao hivyo visingeweza kukamilika hadi usiku na hivyo leo anatarajiwa kuzungumza katika kikao cha majumuisho kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara.
Kutokana na mkutano, kuna uwezekano Pinda akachelewa ufunguzi wa shughuli za Bunge zinazotarajiwa kuanza leo.
Wakati Serikali ikichukua hatua za kudhibiti ghasia hizo, taarifa kutoka Masasi zilisema mji huo jana ulikuwa shwari.
Taarifa za vyombo vya habari, zilimnukuu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Dk Harry Mwembe akisema idadi ya vifo vilivyotokana na vurugu hizo, iliongezeka kutoka watu watatu mpaka wanne juzi asubuhi.
Wakati hayo yakijiri Mtwara, Chadema imeweka wazi msimamo wake kuhusu vurugu za Mtwara, ikisema inaunga mkono wananchi na kuitaka Serikali isitishe kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam, hadi itakapozungumza na wananchi kuhusu suala hilo kwa uwazi na kuridhiwa.
Aidha, ilituma ujumbe kwa CCM ikisema ghasia kama hizo zitasambaa sehemu zingine za nchi ikitamba kwamba wakati wa kubembelezana umekwisha huku ikitumia usemi wake wa kawaida kuwa kama ni noma na iwe noma.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisema jana Dar es Salaam katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu kuwa kama CCM inafikiri ina wajibu wa kuzungumzia suala la gesi, ijiandae kutoa majibu ya dhahabu, urani na pembe za ndovu.
Alisema wamekaa siku mbili kujadili suala la gesi Mtwara, na kuona kinachotokea ni kielelezo kuwa Watanzania wamechoka, hawana imani na nchi wala viongozi wao na kuamua kuchukua hatua.
Bila kujali hasara ya mali na maisha ya watu inayotokea Mtwara, Mbowe alisema wananchi wameona rasilimali hiyo inasafirishwa kwa ajili ya kunufaisha wachache walioko CCM ndiyo maana wakachukua sheria mkononi na kwamba wanastahili kupongezwa.
“Hatuwezi kuendelea kufanya kazi za siasa kama dini … amani ya nchi itakuwapo pale rasilimali za nchi zitakaponufaisha wananchi,” alisema Mbowe na kusisitiza kuwa Serikali ikae na wananchi wa Mtwara na kujadili suala hilo kwa uwazi na kuridhiwa kwa faida ya wote.
Kadhalika alisema chama hicho kinaitaka Serikali kuweka mikataba yote 26 ya gesi mezani ili kampuni zilizowekeza zifahamike na kujadiliwa.
Aidha, alisema Chadema haina vita wala haichukii wawekezaji na wasiwe na hofu nao ila wawepo wale ambao wananufaisha pande zote.
Kuhusu Katiba akizungumza kwa jazba, alisema hawatakubali kupandikiziwa isiyo na maslahi na wananchi na kwamba pindi ikitokea hivyo “hapatatosha”.
“Tukiona Katiba Mpya haisimamii maslahi ya Watanzania tutakataa kuiridhia na tutawaamsha Watanzania nchi nzima,” alisema.
Kuhusu Muungano, alisema Chadema inataka Serikali ya Tanganyika na kwamba si Muungano wa kulazimishana kwa kuwa Zanzibar tayari ni nchi kamili yenye jeshi lake, bendera, wimbo na Dola inayojitegemea.
“Chadema tumekuwa tukidai Muungano wa serikali tatu…hatuna ugomvi na Zanzibar ila wao wanatuona sisi mandondocha, kwa kung’ang’ania Muungano ambao hata Katiba yao walishajitoa,” alisema na kuongeza kuwa mwaka 2013 ni wa nguvu ya umma, bila kufafanua umma upi.
Bila kuzingatia kuwa maoni ya Katiba mpya yanatolewa, alitishia kuwa Chadema haitaingia kwenye uchaguzi na Tume ya Uchaguzi iliyopo ambayo alidai ni ya kiinimacho isiyo huru na kwamba suala hilo lisipofanikiwa wataingia barabarani na “kitaeleweka”.
No comments:
Post a Comment