MITAMBO YA ANALOJIA DODOMA KUZIMWA JANUARI 31...

Mandhari ya mji wa Dodoma.
Wakazi wa Mkoa wa Dodoma wametakiwa kujiandaa wakati wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikitarajia kuzima mitambo ya kurusha matangazo ya televisheni  ya mfumo wa analojia Januari 31, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Habbi Gunze alisema hayo jana katika Mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema maandalizi ya kuzima mitambo ya utangazaji wa televisheni katika Mkoa wa Dodoma, yamekamilika kwa kushirikisha wadau wa sekta ya utangazaji  Januari 31, mwaka huu saa sita usiku.
Gunze alisema elimu kwa umma kupitia mbinu mbalimbali kuhusu mchakato wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa digitali, imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha  ambapo matangazo ya digitali yanawafikia watu asilimia zaidi ya 20 kati ya watu asilimia 24 wanaopata matangazo ya televisheni ya analojia.
Alisema Serikali iliweka ratiba ya uzimaji mitambo ya analojia,  ambapo  katika Mkoa wa Dar es Salaam  ilizimwa Desemba 31, mwaka jana na Dodoma na Tanga  mitambo itazimwa Januari 31, mwaka huu.
Katika Jiji la Mwanza mitambo hiyo itazimwa Februari 28, Moshi na Arusha mitambo itazimwa Machi 31, mwaka huu na Mkoa wa Mbeya mitambo hiyo itazimwa Aprili 30, mwaka huu.
Alisema mabadiliko hayo hayahusu matangazo kwa njia  ya utangazi wa satelaiti, nyaya na redio.

No comments: