Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu. |
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ametaka Katiba Mpya iipe taasisi hiyo kinga ili isiingiliwe na wanasiasa katika utendaji wake.
Amesema shughuli za BoT ni nyeti hivyo ni vyema Katiba mpya ikatamka kuwa hairuhusiwi wanasiasa kuingilia utendaji wake. BoT ni taasisi ya Serikali ambayo kiutawala iko chini ya Wizara ya Fedha na Waziri wa Fedha, ndiye msemaji wa taasisi hiyo katika shughuli mbalimbali.
Profesa Ndulu ambaye alikuwa jana anaongoza ujumbe wa BoT uliofika mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yake, alisema Benki Kuu inasimamia uchumi wa nchi na huduma zake ni nyeti.
Pia alisema ndani ya Katiba zitenganishwe mamlaka zinazotumia fedha na zinazotoa fedha kwa kuwa madaraka ya kutoa fedha anayo mwenye kutumia na lazima awe na nidhamu ya kutoa fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni vema suala hilo likatenganishwa katika Katiba mpya, dhamira ikiwa ni kuboresha shughuli za fedha na uchumi.
Gavana huyo pia alisema wamependekeza kinga za BoT ambazo kwa sasa zipo ndani ya sheria zilizotungwa na Bunge; lakini akasema ni vema kwa sasa ziwekwe ndani ya sheria mama yaani Katiba, ili kutambulika kirahisi.
Ndulu alitoa maoni hayo akizingatia huko nyuma wakati wa wizi wa fedha kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), inasemekana baadhi ya wanasiasa ndio waliotoa maagizo ya fedha hizo kutolewa.
Lakini pia kuna wakati kulitokea mgongano kati ya aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Balali na kiongozi (jina linahifadhiwa) hali iliyodhihirisha kuwapo shinikizo la wanasiasa juu ya utendaji wa taasisi hiyo nyeti.
Akizungumzia suala la baadhi ya watu kuficha fedha nje ya nchi, Gavana Ndulu alisema fedha zilizoko nje ya nchi ni ndogo kulinganishwa na zilizoko ndani ya nchi ambazo Watanzania wengi wamekuwa wakizirudisha na kuwekeza nchini.
Alisema fedha zilizoko nje ni dola milioni 180 wakati Watanzania walioko nchini wana dola bilioni 2.2 katika benki za ndani na wamekuwa wakiwekeza ndani ya nchi.
Aliongeza kuwa ni kweli watu walikuwa wanaweka nje lakini baada ya kupatikana fursa za kibenki, watu wamerudisha fedha na kuwekeza nyumbani na ndiyo maana Tanzania ya leo imebadilika.
“Ndiyo maana kuna mabadiliko ndani ya nchi kama ujenzi wa majumba… ni kutokana na fursa zilizopo,” alisema.
Kuhusu fedha chafu alihoji: “Hivi nani anaweza kutafuta fedha chafu akaenda kuziweka benki? Au nje ya nchi kama watu wanavyodai?” Aliongeza kuwa wenye fedha chafu wanazilalia kwenye uchago hawawezi kwenda kuziweka benki.
Alisema ndiyo maana wanapendekeza Katiba iwape mamlaka zaidi BoT ili waweze kufanya kazi kwa uhuru.
No comments:
Post a Comment