Msanii Elicabeth Michael 'Lulu'. |
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuachia kwa dhamana msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael 'Lulu' anayekabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Lulu aliwasilisha maombi ya dhamana kupitia kwa jopo la mawakili wake, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika.
Maombi hayo yaliwasilishwa chini ya hati ya dharura, wakitaka yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa madai kuwa mshitakiwa amekaa rumande kwa muda mrefu.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Zainab Mruke alisema kuwa, mahakama imekubali ombi hilo la dhamana kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika na dhamana ni haki yake ya msingi.
Alisema Lulu atakuwa nje kwa dhamana endapo atakuwa na wadhamini wawili, wafanyakazi wa serikali watakaosaini hati ya Sh milioni 20, atatakiwa kuwasilisha hati zake za kusafiria kwa msajili wa mahakama na kutosafiri nje ya Dar es Salaam bila idhini ya Msajili wa Mahakama.
Aidha anatakiwa kuripoti mahakamani kila mwezi hadi kesi yake ya msingi itakapokwisha, pia Jaji Mruke alisema ingawa dhamana ni haki yake kisheria lakini ikumbukwe kuwa kuna roho ya mtu imepotea hivyo lazima sheria zifuatwe.
Alimtaka msajili wa mahakama kuhakikisha masharti yote yanatimizwa na kuongeza kuwa: “Mshitakiwa ataendelea kubaki rumande hadi atakapotimiza masharti hayo.”
Baada ya kuambiwa dhamana yake imekubaliwa Lulu alianza kulia mahakamani, hata hivyo alirudishwa rumande kwa kuwa hakutimiza masharti ya dhamana baada ya kuchelewa kuwasilisha hati yake ya kusafiria kwa msajili wa mahakama.
Awali Wakili Kibatala aliiomba mahakama itoe dhamana kwa mshitakiwa kwa masharti ambayo itaona yanafaa kwa kuwa shitaka linalomkabili Lulu lina dhamana, ambapo upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku Lulu akikabiliwa na mashitaka ya kumuua Kanumba kwa kukusudia hata hivyo baada ya upelelezi kukamilika, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alibadilisha mashitaka dhidi yake na kuwa ya kuua bila kukusudia.
No comments:
Post a Comment