BUNGE LAJITOSA KUSHUGHULIKIA SAKATA LA GESI MTWARA...

Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Makinda akiingia bungeni mjini Dodoma, jana.
Bunge linatarajia kuunda Tume ili kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi wa mkoa huo kuhusu malalamiko ya gesi.
Tume hiyo ambayo muundo na wajumbe wake vitatangazwa baadaye, pia itasikiliza upande wa Serikali ikiwa ni hatua ya kutatua mgogoro huo.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alitoa taarifa hiyo bungeni jana mjini hapa  baada ya kipindi cha Maswali na Majibu, kabla ya kuahirisha kikao cha kwanza cha mkutano huo wa 10 wa Bunge.
Alisema Tume itaundwa rasmi ili kupata ukweli wa jambo hilo ambalo taarifa zake zimekuwa zikitawala vyombo vya habari ndani na nje ya  nchini.
Alisema ingekuwa vema wakapata uhakika kutoka kwa wahusika kabla ya kulijadili katika mkutano huu kutokana na unyeti wake.
Spika aliongeza kuwa Bunge ni chombo muhimu cha kuleta umoja na amani, hivyo ni vema wabunge wakavuta subira, kuwa na busara na wakati huo huo hekima ikitumika katika kujadili suala hilo.
“Nimekuwa nikipokea mapendekezo kutoka kwa wabunge kuhusu kujadili suala hilo kwa hoja ya dharura, lakini nimeona ni busara kuunda Tume kwenda kupata uhakika wa suala hilo,” alisema.
Alitaka wananchi wa Mtwara kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Tume itakapowasili na kuzungumza nao kuhusu malalamiko yao.
Wakati Bunge likichukua uamuzi huo, juzi Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema uamuzi  wa kujenga bomba la gesi na kuisafirisha ulipata baraka za Bunge ambalo wabunge wake bila kujali vyama, walipitisha Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2012/13 ambao miongoni mwake, suala hilo lilikuwamo.
Simbachawene ambaye alikuwa akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV, alieleza wasiwasi wake kwamba upo uwezekano wa ushindani wa kibiashara miongoni mwa kampuni au watu binafsi kujipenyeza katika suala hilo na kuamua kulikuza kwa maslahi binafsi.
“Ridhaa ya Bunge ipo katika suala hili na mpango wa maendeleo wa 2012/13 na kitabu cha Bajeti kina picha ya bomba. Kwenye Bunge tumeridhia kabisa.
“Waliosaidia bajeti hii ikapita na mpango ukapitishwa ni vyama vyote ikiwamo Chadema ... waliunga mkono, sasa leo inaonekana vyama vya upinzani ndivyo vinavyopinga!” Alishangaa.
Kuhusu uwezekano wa kampuni kubwa kuwa nyuma ya mgogoro alisema: “Zina ushindani wa kibiashara, inawezakana hii vita ikawa maslahi ya watu binafsi au ya kampuni. Kweli hoja hii haizungumziki tukaelewana? Inashangaza kukuta aliye Iringa, Mwanza anasema hivyo hivyo” .
Hata hivyo, alisisitiza kwamba madai yote ya wananchi wa Mtwara yana majibu. Alieleza kushangazwa na madai kwamba kiwanda cha kuchakata gesi kitajengwa Dar es Salaam.
“Wanachohoji watu wa Mtwara wana haki... ukisema Mtwara tunanufaika vipi ni haki yao... ukweli ni kwamba mtambo tunajenga katika kijiji cha Madimba na wananchi walishiriki uzinduzi, leo wazee wa Mtwara wanasema mtambo umehamishwa wa kuchakata gesi. Duniani kote lazima mtambo wa kuchakata uwe karibu,” alisema na kusisitiza kwamba kiwanda hicho kinajengwa Mtwara.
“Huwezi kuwa na gesi Mtwara na kiwanda cha kuchakata kikawa Dar es Salaam,” alisisitiza na kutaja viwanda vya usindikaji wa gesi katika maeneo ya Kiswele, Mchinga bay, Lindi, Mikindani na Uwanja wa Ndege kwamba vitatoa ajira kwa wakazi mkoani humo.
Aliendelea kufahamisha umma, kwamba kiwanda cha saruji kitakachojengwa katika kijiji cha Msijute kitaanza kuajiri watu 6,000 na pia kuhusu viwanda vya mbolea, eneo limeshapatikana na michoro kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha Amonia uko tayari.
“Sitaki kubeza wajibu wa vyama vya siasa katika kusaidia jamii kupata uelewa kudai haki kutoka serikalini na wala sitaki kubeza wajibu wa asasi zisizo za serikali katika kuwapa watu elimu. Lakini unapokuwa unapeleka upotoshaji ili waidai serikali huku ukiwa unajua, hutendi haki na huna dhamira ya kweli kwa maendeleo ya nchi,” alisema Simbachawene.
Alisema pamoja na kwamba wananchi wana hoja, tayari zimeshajibiwa hivyo wakubali serikali itekeleze hayo inayofanya na kama ni uongo, wasubiri waihukumu mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema ingawa athari za mgogoro hazijajitokeza sasa, alihadharisha fujo na vurugu kwamba zinaleta picha mbaya katika medani za kiuchumi, kisiasa na heshima kimataifa.
Kwa mujibu wa Simbachawene, mwezi huu mkandarasi alitakiwa awe ameanza kazi ya kulaza mabomba. Alisema vipo vifaa kutoka China vimesimamishwa kuletwa.
Alitaka Watanzania wenye mapenzi mema waendelee kutoa elimu kwa wananchi na wakati huo huo wasomi, vyombo vya habari vichangie suala hilo kwa uzalendo na si kwa ushabiki.

No comments: