Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu wawili, akiwemo askari polisi mwenye nambari G 1305 Ladislaus, maarufu kwa jina la Zinja, kwa tuhuma ya kumshambulia, kumpiga na kumsababishia mauti kijana aliyetuhumiwa kuwa ni mwizi wa baiskeli.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alikiri kutokea kwa mkasa huo.
Pia, alithibitisha kuwa watuhumiwa wote wawili, wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea .
Alisema askari huyo ambaye anafanya kazi katika kituo cha polisi mjini hapa, wakati mkasa huo wa mauaji ukitokea, alikuwa likizo.
Mwaruanda alisema aliyeuawa alitambuliwa kuwa ni Ally Thomson “Okocha’ (35), anayetuhumiwa kuiba baiskeli ya David Mwaipopo "Mwaisa" (38) miezi miwili iliyopita na taarifa ya tukio hilo iliripotiwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa.
Inaelezwa kuwa tukio hilo limetokea juzi saa nane na nusu mchana kwenye kitongoji cha Mazwi mjini hapa.
Siku hiyo askari polisi huyo akiwa na Mwaisa, walimkamata mtuhumiwa huyo na kuanza kumshambulia kwa ngumi na mateke huku wakimpeleka kituo cha polisi.
Habari zinadai kuwa wakiwa njiani, Okocha alianza kuishiwa nguvu kwa maumivu makali mwilini. Walipomfikisha kituo cha polisi alipatiwa Fomu ya Matibabu (PF3) na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga kwa matibabu, lakini alifariki dunia baada saa 10 jioni siku hiyo.
Taarifa za awali za kipolisi zinadai kwamba Thomson alikuwa amefunguliwa kesi ya wizi wa baiskeli yenye thamani ya Sh 100,000 miezi miwili iliyopita, lakini alikuwa akijificha. Taarifa nyingine zilidai kwamba mtuhumiwa huyo ametoroka na kukimbilia mkoani Mbeya.
Inadaiwa kwamba baada ya Mwaisa kumuona ‘mwizi’ wake huyo akirandaranda mjini hapa, alimpigia simu askari huyo ambaye tangu awali alikuwa akipeleleza kesi hiyo ili aweze kumkamata na ndipo walipotumia nguvu kubwa katika kukabiliana naye na kumsababishia kifo chake.
Pia tangu juzi kulikuwa na taarifa za ndugu wa marehemu huyo waligoma kuchukua mwili wa marehemu wao huyo, kwa madai ya kushinikiza kukamatwa kwa askari polisi huyo, kwani hadi jana askari huyo alikuwa hajakamatwa huku mtuhumiwa mwenzake (Mwasa), alikuwa tayari amekamatwa mara baada ya kuthibitika kuwa Ally alifariki dunia akiwa anatibiwa.
Kwa mujibu wa mganga aliyeufanyia uchunguzi wa kitabibu mwili huo, kwa masharti ya kutoandikwa jina lake, alidai kuwa hata hivi tunaenda mitamboni bado ndugu wa marehemu hawajafika mochwari kuchukua mwili wao licha ya kuruhusu ufanyiwe uchunguzi .
“Kutokana na utata uliojitokeza jana baada ya ndugu wa marehemu kuususa mwili wa marehemu wao endapo kama utafanyiwa uchunguzi wa kitabibu bila wao kushirikishwa basi hawatakuwa tayari kuuchukua wataachia mamlaka kuuzika .. hivyo tuliwashirikisha na wakaafiki afanyiwe uchunguzi wa kitabibu.
Lakini hadi sasa bado hawajarudi kuuchukua labda ni kutokana na shinikizo walilotoa kuwa lazima na askari aliyehusika naye akamatwe …“ alisema.
Hata hivyo hakuwa tayari kuweka bayana kilichosababisha kifo cha marehemu huyo licha ya kukiri kuwa alikuwa amepigwa kwa madai kuwa taarifa hiyo itatolewa mahakamani wakati atakapotakiwa kutoa ushahidi na si vinginevyo.
Chanzo kingine cha kipolisi kinadai kuwa kutokana na hasira za wananchi wanaomlalamikia askari huyo kusababisha kifo cha raia huyo endapo kama atabainika kuwa hana hatia ni muhimu akapewa uhamisho kwani maisha yake yatakuwa hatarini .
Kwa kile ninachoelezwa kuwa ni shinikizo la wananchi wenye hasira kali pamoja na wanandugu kususa mwili wa marehemu huyo, Jeshi la polisi mkoani hapa limesalimu amri kwa kumkamata askari huyo ambaye sasa pamoja na mtuhumiwa mwenzake (Mwasa) wanahojiwa kuhusiana na mkasa huo.
No comments:
Post a Comment