Mambo yamezidi kuibuka ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambapo safari hii wainjilisti 12 wa Usharika wa Lokii Jimbo la Arusha Mashariki katika Dayosisi ya Kaskazini Kati, wameibuka na kudai hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi sita.
Kutokana na adha hiyo, wametoa siku saba wawe wamelipwa malimbikizo ya mishahara yao, la sivyo wametishia wataacha kazi ya kutoa huduma katika sharika mbalimbali ndani ya kanisa hilo.
Wakizungumza na mwandishi kwa nyakati tofauti juzi na jana, wainjilisti hao walisema mshahara wao wa mwisho walilipwa mwezi Mei mwaka jana.
Lakini, taarifa zilisema uongozi wa jimbo chini ya Mkuu wa Jimbo hilo, Mchungaji Isack Kisiri, umeshindwa kutoa taarifa yoyote juu ya wainjilisti hao kucheleweshewa mishahara yao.
Uchunguzi wa mwandishi ulifanikisha kuona nyaraka za malipo ya wainjilisti hao, ambapo ilibainika kuwa kila mmoja hulipwa Sh 60,000 kama kima cha chini na kima cha juu ni Sh 93,000.
Hata hivyo, licha ya kulalamika malipo hayo kuwa ni madogo, pia wanalia kufanya kazi katika mazingira magumu, ikiwa ni pamoja na kukosa usafiri.
“Hebu angalia, tunafanya kazi katika mazingira magumu, hatuna pikipiki wala gari lakini hatukosekani kanisani kuhubiri neno la Mungu na kuhamasisha waumini kujiunga na kanisa… lakini uongozi umekuwa ukitukatisha tamaa kwa kutotujali angalia kwa mshahara.
“Sasa uvumilivu umefika mwisho na tumetoa muda wa siku saba na wakishindwa kutekeleza madai yetu tutagoma,” alisema mmoja wa wainjilisti hao.
Kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, wainjilisti hulipwa mishahara yao na Usharika ukisimamiwa na Jimbo lao na mwenye mamlaka ya kuwalipa ni Mkuu wa Jimbo la Arusha Mashariki, ambaye ni Mchungaji Kisiri.
Mchungaji Kisiri hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini juhudi zinaendelea kumtafuta ili kueleza tatizo la malimbikizo ya mishahara kwa wainjilisti hao 12.
Kuibuka kwa sakata la wainjilisti hao ni mwendelezo wa mambo mengi yanayoendelea kufichuliwa ndani ya kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini Kati iliyo katika hatari ya kufilisiwa mali zake, ikiwa ni pamoja na hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs kutokana na deni la Sh bilioni 11.
Kutokana na deni hilo, uongozi wa Dayosisi ulisambaza waraka kwa waumini wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili kunusuru mali za kanisa, jambo lililoibua mgogoro, kwani wengi walipinga huku wakitaka maelezo ya sababu za mradi huo na mingine ya kanisa kushindwa kuzalisha faida, licha ya kuoneka kufanya vizuri kibiashara.
Miongoni mwa waliopinga alikuwa Mchungaji Philemon Mollel wa Usharika wa Ngateu, aliyetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini akageuziwa kibao yeye na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika kanisa hilo nchini.
Uamuzi huo ulizidi kuvuruga hali ya hewa ndani ya kanisa, huku wengi wakimuunga mkono Mchungaji Mollel na kutishia kuacha kutoa ushirikiano kwa Dayosisi, ikiwa ni pamoja na kutopeleka asilimia 40 ya sadaka kama mchango wa maendeleo ya Dayosisi hadi Mchungaji Mollel atakaporejeshwa kazini na kuendelea na shughuli za kichungaji.
Hadi sasa Mchungaji Mollel hajarudishwa kazini, lakini vikao vya ndani vimeripotiwa kufanyika kwa lengo la kutafuta mwafaka.
No comments:
Post a Comment