MCHUNGAJI AELEZA ALIVYORUKA UKUTA KANISA LILIPOCHOMWA MBAGALA...

Kanisa liliwaka moto Mbagala, Dar es Salaam wakati wa ghasia hizo.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbagala, Frank  Kimaro (32) ameieleza Mahakama kuwa aliruka uzio na kukimbia ili kuokoa maisha yake baada ya kundi la watu kuvamia katika kanisa hilo na kulichoma moto.
Mchungaji Kimaro alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi ya wizi na uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh milioni 520.
Tukio hilo lilitokea Oktoba mwaka jana baada ya vijana wawili wenye umri wa chini ya miaka 18 waliokuwa wakicheza na kubadilishana mawazo kuhusu dini ndipo mmoja akakojolea Kurani.
Tukio hilo liliripotiwa Polisi ndipo vijana waliojiita Waislamu walipovamia kanisa hilo na kulichoma moto na kuharibu mali zenye thamani ya Sh milioni 520.
Akiongozwa na Wakili Tumaini Kweka, Mchungaji Kimaro alidai kuwa, Oktoba 12 mwaka jana akiwa kanisani alipigiwa simu na kuambiwa awe makini kwa kuwa kuna kundi la watu walivamia kituo cha Polisi cha Mbagala. Alipotoka kwenda kumtaarifu mlinzi alisikia vishindo vya watu nje ya uzio.
Alidai kuwa watu hao walianza kurusha mawe ndipo mlinzi alipopiga risasi hewani ili watawanyike lakini alipotaka kupiga risasi ya pili iligoma na watu hao kuvamia kanisa hilo huku wakirusha mawe, yeye akaamua kukimbia.
“Kwa usalama wangu niliruka ukuta na kukimbia hadi katika benki ya CRDB, ambako Meneja wao aliniruhusu kuingia nikajificha huko hadi jioni nilipopigiwa simu na Mwinjilisti aliyekuwa amejificha kanisani kuwa hali imetulia” alidai.
Alidai aliporudi kanisani alikuta uzio wa Kanisa umevunjwa, altari, ofisi yake na mali zilizokuwemo ndani zimechomwa moto na mali nyingine ziliibwa lakini wakati wa tukio hakumtambua mtu kwa kuwa alikuwa katika harakati za kuokoa maisha yake.
Kwa upande wake mlinzi wa Kanisa hilo Michael Woga (30) alidai kuwa, siku hiyo saa 5 asubuhi aliona kundi la watu asiowajua wakirusha mawe ndipo alipopiga risasi hewani ili kuwatawanya lakini alipopiga ya pili iligoma kwa kuwa awali risasi ilitoka lakini gamba lilibaki.
Alidai alijaribu kutoa gamba lakini alishindwa kwa kuwa yeye siyo mtaalamu wa bunduki, akaamua kukimbia ili kuokoa maisha yake lakini alirudi jioni kuchukua nguo zake  na kukuta wamechoma kanisa na nguo zake hakuziona.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Hamid Senkondo (26), Shego Shego (21), Mashaka Imani (22), Hamza Mohamed (28), Juma Mbegu (20), Issa Abdallah (29), Hamis Kimwaga (19), Ramadhan Mburu (42) na Mohamed Yusuph (28) ambao wanakabiliwa na mashitaka matano.
Hakimu Waliarwande Lema ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 4 mwaka huu watakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.

No comments: