BASI LAPARAMIA GARI ALILOPANDA LOWASSA ...

Edward Lowassa.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amepata ajali baada  ya  gari lake alilokuwa amepanda kugongwa ubavuni na basi la Moro Best lililokuwa likitokea mkoani Morogoro kwenda  Dar es Salaam.
Ajali hiyo imetokea jana katika barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam eneo la Bwawani, mpakani mwa Mkoa wa  Pwani.
Lowassa alikuwa njiani kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Morogoro kuendesha harambee ya kupata fedha za kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Usharika wa Kilakala la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro.
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alikuwa akisafiri na gari lenye namba za usajili T 676 AWW aina ya VX Toyota Land Cruiser na ajali  hiyo ilitokea saa 3:15  asubuhi katika barabara hiyo karibu na  daraja eneo la Bwawani,  mpakani mwa mikoa hiyo miwili.
Hata hivyo namba ya basi la Moro Best haikupatikana mara moja baada ya msaidizi  wa Lowassa kuelezea kuwa aliiwasilisha Polisi Mkoa wa Morogoro lakini amesisitiza basi lililosababisha ajali hiyo ni la Moro Best.
Akizungumza katika hotuba yake mbele ya waumini wa KKKT Dayosisi ya Morogoro pamoja na wageni wengine waalikwa akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, Lowassa aliufahamisha umati huo kuwa amenusurika kifo pamoja na wasaidizi wake kutokana na kugongwa na basi.
“Asubuhi ya leo (jana) tulipofika Bwawani tulipatwa na ajali, kuna mabasi mawili yalikuwa yakifuatana moja nyuma  ya  jingine yakiwa karibu kuvuka daraja na sisi tukiwa tunavuka daraja upande wetu,” alisema Lowassa.
“Ghafla lile basi la nyuma dereva wake aliamua kulipita lile la mbele, hivyo akaja upande wetu akatugonga ubavuni. Kweli mkono wa Mungu ni mkubwa sana, saa hizi tungezungumza lugha nyingine ...bwana ni mwema na muaminifu sana, nimetoka  bila mkwaruzo,” aliwaambia waumini na wananchi walioshiriki harambee hiyo.
Polisi mkoani Morogoro imethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa inafanya uchunguzi.
Kwa upande wa ushiriki wa  kuchangia makanisa na Taasisi nyingine za Dini, aliwapasha kwa kusema  hana utajiri kama wanavyofikiria watu wengine.
“Najua maneno yapo mengi kutoka kwa marafiki zangu, naenda kanisani kufuata nini, nimewaambia kuwa ninapata faraja sana kufanya kazi ya mungu... sina utajiri kama wanavyodai, ila nina watu, “ alisema Lowassa.
Pia alisema anajivunia kuwa na ushawishi mkubwa kwa watu katika kazi ya bwana na siku zote anaifanya kwa upendo na kwa furaha kubwa pamoja na uaminivu wa hali ya juu.
Katika harambee hiyo, Lowassa alifanikisha kuchangia jumla ya Sh milioni 64, kati ya hizo fedha tasilimu ni Sh milioni 18,
ambapo yenye binafsi na marafiki zake walitoa Sh milioni 18.5 na lengo lilikuwa ni kupata Sh milioni 48.6.

No comments: