EWURA YATEKETEZA SHILINGI BILIONI 14 KWA MWAKA...

Dk Haruna Masebu.
Matumizi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), yameongezeka zaidi ya mara mbili kutoka Sh bilioni sita mwaka 2010/11 hadi Sh bilioni 14 mwaka 2011/12.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wameonesha kushitushwa na matumizi hayo na kuitaka mamlaka hiyo itoe ufafanuzi wa fedha hizo ikiwa ni pamoja na mafanikio iliyopata.
Hata hivyo, katika kutetea matumizi hayo, Mamlaka hiyo imekiri ongezeko la matumizi hayo huku ikitoa sababu za kukua kwa shughuli zake wakiwamo wafanyakazi.
Wakati Mamlaka hiyo ikiwasilisha hesabu zake za mwaka wa fedha 2011/12 mbele ya Kamati hiyo jana Dar es Salaam, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alionesha wasiwasi wake juu ya kupanda kwa matumizi hayo tena katika kipindi kifupi.
“Mwenyekiti matumizi ya Mamlaka hii naona yameongezeka kila sehemu, kwa mfano katika eneo la ukaguzi na kazi za nje, matumizi yamepanda kutoka Sh milioni 433 hadi Sh bilioni 2.7,” alisema Bulaya.
Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM) alionesha eneo lingine katika kitabu cha Mamlaka hiyo la kujenga uwezo ambapo fedha hizo zimepanda kutoka Sh bilioni 1.9 hadi Sh bilioni 2.3.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kangi Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara (CCM), alisema ni vema Mamlaka ikatoa maelezo kuhusu kupanda kwa matumizi yake kwa kuwa hata matumizi yote kwa jumla ya Mamlaka hiyo yanaonekana kupanda.
Alitoa mfano wa eneo la mabaraza ambapo matumizi yake yalipanda kutoka Sh milioni 621 hadi Sh bilioni moja.
Lugola alitaka Mamlaka pia ijieleze ni kwa nini iliingia mkataba na kampuni ya GFI kuingiza vinasaba kwenye mafuta bila kuzingatia suala la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kusababisha Ewura kulipia kodi hiyo badala ya kampuni husika.
“Hii kampuni ilipaswa itozwe kodi tangu awali, lakini ninyi hamkuzingatia hili, sasa Serikali imewabana nyie, ndio mnaolipia kodi hiyo kwa fedha za wananchi, naomba mtuandikie maelezo juu ya hili,” alisema.
Mbali na hatua hiyo Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM),  alitaka kujua Ewura kama mdhibiti, inachukua hatua gani kusaidia wananchi kumudu bei za umeme ambazo kwa sasa ziko juu.
Aidha, alihoji tatizo la kutokuwapo kwa utaratibu wa kueleweka kwa watumiaji wakubwa na wadogo wa umeme hali iliyosababisha kuwepo kwa malalamiko kwa wananchi hasa katika malipo ya umeme kila mwisho wa mwezi.
Akifafanua juu ya hoja ya ongezeko la matumizi ya Ewura, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Saimon Sayore, alitaka wabunge wasishitushwe na kupanda kwa matumizi ya Mamlaka hiyo, kwa kuwa inaweza kujiendesha vizuri na kutoa mgawo wake kwa Serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema kupanda kwa matumizi kunatokana na kukua kwa Mamlaka hiyo ambapo shughuli zake zimeongezeka, ikiwa ni pamoja na kuhudumia kifedha taasisi mbili zilizoanzishwa na Serikali ambazo ni Baraza la Ushauri la Serikali na Baraza la Ushauri la Watumiaji.
Akijibu swali la bei za umeme, Masebu alikiri bei ya umeme kuwa juu lakini kwa mujibu wa sheria ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) haijabagua katika malipo na kubainisha kuwa kila mteja atalipa kulingana na bei iliyopangwa na si mwingine kumbebea mzigo mwenzake.

No comments: