AKAUNTI YA TIRDO YAHIFADHI KINYEMELA FEDHA ZA POLISI...

Muhammad Amour Chombo.
Fedha za baadhi ya viongozi wa wilaya wa Polisi pamoja na taasisi, zimebainika kuingizwa kinyemela katika baadhi ya akaunti za Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), wakati viongozi na taasisi hawana ushirikiano wa kibiashara na shirika hilo.
Pamoja na hayo, pia imebainika kuwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Asifa Nanyaro, aliyemaliza muda wake Machi, mwaka jana, alikuwa akilipwa posho ya nyumba iiliyofikia Sh milioni 22 kwa mwaka mzima wakati anaishi kwenye nyumba ya Serikali.
Hayo yalianikwa wazi Dar es Salaam jana na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo pamoja na mambo mengine, ilikataa kupitisha hesabu za shirika hilo na kuagiza Tirdo ianze kuchukua hatua za kumshitaki Mkurugenzi huyo mstaafu kwa tuhuma za wizi wa fedha za umma.
Akizungumzia msimamo wa kamati hiyo kuhusu matatizo hayo, Kaimu Mwenyekiti wa POAC, Muhammad Amour Chombo, pia alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi upya wa hesabu hizo na kupeleka ripoti yake kwa kamati hiyo kwa hatua zaidi.
“Kamati haijaridhishwa na kilichomo ndani ya hesabu hizi, hesabu zenu zimepata hati chafu, tena chafu kweli ndio maana hatupitishi hesabu zenu, kuna mambo mengi ya wizi na ubadhirifu na hata utetezi wenu hauturidhishi,” alisema Chombo.
Awali mjumbe wa Kamati hiyo na mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), alitaka Menejimenti ya shirika hilo, ijibu hoja za CAG kuhusu tatizo la shirika hilo kuingiza fedha zake kwenye akaunti zake zilizopo benki ya NMB huku kukiwa hakuna hati ya kuweka fedha.
Akijibu swali hilo, Mhasibu wa TIRDO, Dominick Kyaruzi, alibainisha wazi kuwa fedha za shirika hilo zimekuwa zikiingizwa na kutoka kwenye akaunti hizo kwa kufuata taratibu zote za kibenki.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kuna tatizo la fedha kuingizwa fedha katika akaunti za shirika hilo ambao hawana uhusiano wowote na TIRDO.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa muda mrefu sasa kumekuwa na watu wakiwemo polisi na taasisi mbalimbali wamekuwa wakiingiza fedha zao kwenye baadhi ya akaunti zetu na kuziacha bila ufafanuzi wowote wala kuwa na uhusiano wowote kibiashara na shirika,” alifafanua.
Alitaja baadhi ya majina yaliyoonekana kutumika kuingiza fedha hizo ambazo kwa mujibu wa Kyaruzi moja ya akaunti za Tirdo, ilikuwa na zaidi ya Sh milioni 60 za watu hao wasio na uhusiano na shirika hilo wakiwemo Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) mbalimbali.
Kutokana na jibu hilo, wajumbe wa kamati hiyo walikuja juu na kuhoji huenda akaunti za shirika hilo zinatumika kwa ajili ya mchezo wa kutakatisha fedha za wizi ambapo Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) alitaka kujua kama wahusika walitaarifiwa au shirika hilo limeripoti polisi.
“Kwanini siku zote hizo mnaona kuna fedha si zenu zinaingizwa kwenye akaunti zenu mmekaa kimya? Hapa kuna kila dalili ya kuwepo mchezo mchafu CAG hili ikague na ikibainika kuwepo kwa mchezo mchafu wahusika wachukuliwe hatua,” alisema Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM).
Kuhusu posho ya nyumba ya Mkurugenzi Nanyaro, Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, Ludovick Manege, alikiri mkurugenzi huyo kulipwa fedha hizo wakati akiishi kwenye nyumba ya Serikali ambayo baadaye aliuziwa.
Alisema menejimenti ya sasa ya shirika hilo iliwasiliana na Dk Nanyaro kuhusu suala hilo, ambaye alijibu kuwa yeye alichaguliwa na Rais tena akiwa mwanajeshi hivyo, kama malipo hayo hayakustahili basi yakatwe kwenye fedha zake za malipo ya posho ya mkataba.
“Tayari tumechukua hatua kuhusu suala hili, tumewasiliana na Wizara ya Utumishi, ili  kumpatia mkataba Dk Nanyaro utakaomuwezesha kulipwa posho hizo na sisi tukate dai letu hili,” alisema Manege, hoja iliyokataliwa na Chombo ambaye alitaka Mkurugenzi huyo ashitakiwe kwa kosa la wizi na si vingine.

No comments: