WANAWAKE WALIOZAA NA BWANA HARUSI WATIBUA NDOA KANISANI...

Altare ya Kanisa Katoliki Parokia ya Familia Takatifu, Sumbawanga ambako ndoa hiyo ilikuwa ifungwe.
Wakati Wakristo wakiungana kusherehekea Sikukuu ya Krismasi usiku wa Desemba 24, Bwana harusi, Crispin Saadani (34) aliyekuwa akisherehekea siku hiyo kwa kufunga ndoa na mchumba wake, alijikuta akizuiwa kuweka ahadi hiyo ya maisha baada ya wanawake wawili alioishi na kuzaa nao, kuingilia kati.
Akiwa ndani ya jengo la Kanisa Katoliki, Jimbo la Sumbawanga, Parokia ya Familia Takatifu na mchumba wake aliyetambulika kwa jina moja la Elizabeth, bwana harusi huyo mtarajiwa alijikuta akizuiwa kupanda madhabahuni na wanawake wawili waliojitokeza huku wakijitambulisha kuwa ni wake zake.
Wakati Padri Boniface Nyama akijiandaa kufunga ndoa hiyo, wanawake hao, Maua Chatakwa na Mwasiti Mbegele (27) walifika kanisani hapo na kumuita mmoja wa wa  wazee wa kanisa hilo.
Akisimulia kisa hicho, Mzee huyo wa Kanisa ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Crispin na mchumba wake, siku hiyo saa sita usiku katika  mkesha  wa Krismasi walikuwa miongoni mwa  maharusi  watarajiwa 32 waliokuwa wameketi  katika  benchi  wakisubiri zamu  zao  ili  wapande madhabahuni kufungishwa ndoa  na Padri Nyama.
Alisema Mwasiti na Maua walitinga kanisani humo, wakamwita  na kumweleza kuwa wamemfuata  bwana wao ambaye wamesikia  anafunga  ndoa na mwanamke mwingine huku wakitoa ishara za kumwonesha.
Mwasiti ambaye ni mkazi  wa Bangwe mjini hapa anayejishughulisha na ufundi  wa kushona nguo za kike, alidai kuishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye mtoto  aitwaye Henry mwenye umri wa mwaka na nusu.
Naye Maua, mkazi wa Jangwani mjini hapa, alidai aliishi kinyumba na Crispin na kuzaa naye watoto wawili.
Akisimulia hali ilivyokuwa, Mwasiti  alidai aliishi kinyumba  na mume huyo na kuzaa naye mtoto wa kiume, Henry,  lakini  walitengana  baada ya  kubaini kuwa  mumewe alikuwa  na wanawake  wengine  wawili  zaidi ambao  ni Maua  na Elizabeth.
“Nilipomtaka aachane nao alikataa  na kusema kuwa  ataishi nao kama wake zake. Alianza kutupangia zamu,  lakini  nilishindwa  pale alipoenda kulala  kwa Maua siku tatu  ya nne nilikusanya  nguo  zake  na kupeleka huko, ukawa mwisho wetu, ” alidai Mwasiti na kuongeza kuwa  kisa hicho kilitokea mwaka  huu. 
Mwasiti alikiri aliposikia Crispin anataka kumuoa Elizabeth, alimshawishi Maua wakamwekee kizuizi ili tu asifunge ndoa na Elizabeth ndipo walipokodi teksi iliyowafikisha  kanisani hapo  saa tano usiku.
Kwa mujibu wa  Mwasiti  baada ya kueleza mkasa  huo  kwa Mzee wa Kanisa, walikaribishwa katika moja ya chumba kanisani  hapo na kukutana na baadhi ya mapadre na wazee wa Kanisa na makatekista.
Alidai baada ya mjadala mrefu ilikubaliwa kuwa shauri hilo  lifikishwe  siku  inayofuata  kwa Paroko wa Kanisa hilo, Padri Leonard Teza, ambaye pia ni Mwanasheria wa Jimbo.
Mzee huyo alikiri kumfuata Crispin ambaye ni mkazi wa Utengule katika Manispaa ya Sumbawanga, alipoketi na mchumba wake akisubiri kupanda madhabahuni na kumuomba atoke nje ya Kanisa kwa dharura na wakaishia kuahirisha ndoa hiyo.   
Mwasiti  ambaye alikuwa muwazi kwa gazeti hili, alidai Crispin aliitwa na kukiri  kuwa  anawafahamu  na amezaa  nao huku wao  wakisisitiza kuwa wapo tayari  afunge ndoa  lakini  awaeleze jinsi atakavyowatunza watoto hao watatu.
“Crispin alikubali kutupatia mtaji wa Sh 100,000 kila mmoja wetu  huku mimi  akidai atanipatia fedha hizi za mtaji Aprili 25, mwaka kesho na mwenzagu Maua aliahidiwa kupewa  kiasi  hicho cha fedha.
“Pia aliahidi kutoa Sh 240,000 na seti ya TV ya inchi 9  aliyochukua kwake (Mwasiti) ifikapo Machi mwaka huu,” alisema  Mwasiti.
Kwa mujibu wa madai ya baadhi ya mashuhuda, wazazi  wa bibi harusi  walisema ndoa hiyo isifungwe tena kwa kuwa bwana harusi amewafedhehesha  huku baadhi ya wakazi  wa  mjini  hapa wakimtuhumu bwana harusi kwa kusababisha hayo yote.
“Kosa hapa  wa kulaumiwa ni huyu bwana harusi, kwa nini  asiwafahamishe  wale wake zake wengine kuwa anatarajia  kufunga  ndoa?” Alihoji mmoja wa mashuhuda.
Akizungumza  kwa njia  ya simu jana, Padri Teza alikiri kutokea  kwa  mkasa huo, lakini  hatimaye alisema baada ya kukutana  na wanawake hao walifikia makubaliano na  hatimaye ndoa hiyo ilifungwa Jumatano asubuhi.

No comments: