NAULI BOTI KWENDA ZANZIBAR SASA HAZIKAMATIKI...

Moja ya boti zinazofanya safari zake kati ya Dar na Unguja ikiwa bandarini tayari kwa kuanza safari.
Tatizo la kupandishiwa nauli lililowapata wananchi wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, limewakuta pia abiria wanaosafiri kwa usafiri wa boti kwenda Unguja na Pemba katika Bandari ya Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa juzi na jana na gazeti hili katika vituo vya kukatia tiketi viliyopo katika maeneo ya bandari hiyo, umebaini kuwepo kwa tatizo hilo huku abiria wakilazimika kulipa nauli mpya ya Sh 30,000 kwa boti ambao hapo awali walikuwa wakikata tiketi hiyo kwa Sh 25,000.
Aidha, kiwango cha nauli pia kimepanda hadi kufikia Sh 20,000 kwa boti ambazo awali ilikuwa ikilipiwa  Sh 15,000 kwa safari hizo, huku ikielezwa kuwa kidogo hali ilianza kurejea taratibu katika siku ya jana
Mmoja wa wakatisha tiketi ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema kupanda kwa nauli kumesababishwa na mahitaji ya usafiri kwa abiria wengi waliojitokeza kituoni hapo kwa ajili ya kwenda kusheherekea sikukuu katika visiwa hivyo.
Huku akitaja majina ya boti zilizohusika katika kutoza nauli hizo, alisema hali kama hiyo imekuwa ikijitokeza kila mwaka inapofika kipindi cha sikukuu mbalimbali zikiwemo  za mwisho wa mwaka.
“Afadhali leo (jana) kidogo bei ya nauli imepungua boti ambayo tiketi yake juzi ilikuwa ikikatwa kwa Sh 30,0000 leo unaweza kuipata hadi kwa Sh 28,000 na ile ya Sh 20,000 imeshuka hadi Sh 18,000 au 17,000,” alisema.
Kwa kipindi cha zaidi ya wiki moja iliyopita, abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali hususani katika kituo cha mabasi cha Ubungo, wamekuwa wakikabiliana na tatizo la kupanda nauli, jambo lililotokana na tabu ya usafiri katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu.
Hata hivyo, ushirikiano unaofanywa na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) pamoja na Jeshi la Polisi wa kuendesha operesheni dhidi ya wahusika wa mabasi yanayobainika kutoza nauli kwa viwango vya juu, umesaidia kudhibiti tatizo hilo.
Alipotafutwa Ofisa mawasiliano wa Sumatra, David Mziray ili kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya wasafirishaji wa boti waliopandisha nauli, hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu.

No comments: