KARDINALI PENGO AZUNGUMZIA MABILIONI YALIYOFICHWA NJE...

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Viongozi wa makanisa nchini wametumia ibada ya sikukuu ya Krismasi iliyoadhimishwa jana nchini na duniani kote, kuhubiri amani nchini kati ya Wakristo na wasio waumini wa dini hiyo, lakini wakionya tabia ya baadhi ya vikundi vyenye lengo la kuchezea amani ya nchi na kutaka Watanzania bila kujali itikadi za dini, kabila na siasa kuenzi amani na mshikamano uliopo.
Kadhalika Watanzania wametakiwa kutobweteka na amani iliyopo, bali kuilinda kwani kutoweka kwake ni jambo la muda mfupi, huku pia ikizitaka Idara kama Polisi, Mahakama, Ardhi na Maliasili kutenda haki kwa Watanzania na kuepuka kuwanyanyasa ndani ya nchi yao.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao, akitoa neno la Mungu kwenye ibada ya kitaifa ya Krisimasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu mjini Moshi na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali, alisema: “Siku za karibuni tumekumbushwa kuwa amani inaweza kutoweka… Tunayosikia kule Kenya, Congo, Sudan na kwingineko yanaweza kutokea hapa kwetu, tuliposikia makanisa yamechomwa moto na wenye imani kali, tukajua mambo haya yatapoteza amani yetu tusipokaa imara.”
Alisema Watanzania wanaopenda amani ni wengi na wapo katika madhehebu ya dini tofauti, itikadi za siasa tofauti, wataalamu wa fani mbalimbali na kabila tofauti. Hivyo alionya watu kuepuka roho ya udini, itikadi za kisiasa ama kabila. Kadhalika alikemea ufisadi na manyanyaso ya aina yoyote.
Dk Shao alisema kufanyika kwa mambo hayo kwa namna moja au nyingine kunaweza kuathiri umoja miongoni mwa Watanzania, jambo ambalo ni kiini cha migogoro katika baadhi ya nchi duniani.
Aliiomba Serikali kutoa kauli yake dhidi ya vitendo vya udhalilishwaji na kejeli dhidi ya Wakristo vinavyofanywa na baadhi ya vikundi vya Kiislamu ambavyo vinatishia kuvuruga amani ya nchi na kuzorotesha
mahusiano mema baina ya Waislamu na Wakristo.
Hata hivyo, askofu huyo alisema tayari Jumuiya ya Kikristo Tanzania imetoa kauli dhidi ya vitendo hivyo na kutaka majibu ya Serikali kwani wakati mwingine kukaa kimya ni ishara ya kuunga mkono kauli na vitendo ambavyo havina nia njema na umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, ameonya kuwa iwapo Serikali haitachukua jukumu la kulinda nyumba za ibada dhidi ya makundi yenye nia mbaya amani ya nchi iko hatarini kuvurugika.
“Isije kanisa likachomwa moto halafu Serikali iseme sio jukumu lake kuyalinda... Mimi nasema ni jukumu lake kutoa ulinzi iwe kwa msikiti au kanisa kwani hayo ni makundi ya Watanzania,” alisema Askofu Pengo jana wakati akitoa salamu zake za sikukuu ya Krismasi.
Askofu Pengo alitoa salamu hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa ibada ya Krismasi katika Kanisa la Katoliki Parokia ya Mtakatifu Boniventure, Kinyerezi, Dar es Salaam.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuwa kwa sasa watu wanaishi kwa mashaka na wasiwasi mkubwa kwa sababu ya tofauti za kidini zilizoanza kuwa chanzo cha kuvurugika kwa amani iliyokuwepo kwa miaka mingi.
Alitaka Serikali ilinde mali ya watu binafsi na mali za makundi halali katika nchi. Pengo alisema Serikali haina jukumu la kulinda taasisi yake tu au shule, bali pia na mali za makundi mengine halali kama nyumba za ibada ambayo ni mali za madhehebu mbalimbali ya kidini.
“Leo hii akitokea mtu akaniambia Yesu sio mwana wa Mungu mimi sina ugomvi naye kwani imani yake inamtuma hivyo, ila akianza kutukana kwamba mimi ni mpumbavu ninayeamini kile asichokiamini hapo ndipo ugomvi unapoanzia,” alisema Pengo na kuongeza kwamba Waislamu wanaamini kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) ni mtume wa Mungu, "Mimi Pengo siamini hivyo; lakini imani yao hiyo isinifanye mimi nianze kuwaona wao ni wapumbavu hadi nigombane nao."
Pengo alisema kitendo cha watu kujilimbikizia mali ni kinyume na mpango wa Mungu ambaye anataka mali ya ulimwengu iwafae watu wote na sio mtu mmoja kujilimbikizia mali nyingi wakati wenzake wanakufa kwa njaa.
"Kuna watu wengine wanakufa kwa njaa, wewe una fedha nyingi umejilimbikizia huu ni upotoshaji wa mpango wa Mungu," alisema Pengo aliyetumia maadhimisno ya sikukuu ya mwaka huu kuzindua Parokia ya Mtakatifu Clara ya Mongo la Ndege na ya Mtakatifu Boniventure ya Kinyerezi.
Akizungumzia kuhusu Katiba, Kardinali Pengo alisema Katiba itakayotungwa ni ya Watanzania wote, hivyo ihakikishe tunu za taifa zilizoko ndani ya katiba ya sasa zinalindwa kwa gharama yoyote.
Pengo alisema hategemei taifa kupata katiba yenye kuleta mgawanyiko wa Watanzania bali kuimarisha umoja wa kitaifa uliopo na kulinda uhuru wa kuabudu wa kila mtanzania. Pia alitaka katiba ambayo italinda hadhi ya kila Mtanzania.
Alipendekeza kuwa kama kuna idadi kubwa ya watu watatoa maoni yenye kuvuruga umoja na mshikamano uliopo, ni vyema maoni hayo yasipewe kipaumbele kwani kufanya hivyo ni kuvuruga amani ya nchi.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa akizungumza katika ibada ya Krismasi jijini Dar es Salaam, amesema tabaka lililopo kati ya masikini na matajiri likiachwa liendelee, litaleta hatari ya kutoweka kwa amani hiyo, hivyo ni vyema likaangaliwa.
Alisema mtu asiyenacho ameendelea kuwa chini dhidi ya yule mwenyenacho, jambo ambalo halipaswi kuendelea.
Aidha, aliwataka waumini wa dini hiyo nchini kote kudumisha amani kuanzia katika ngazi za familia zao licha ya kuwa wamekuwa wakichokozwa na baadhi ya watu ambao hata hivyo hakuwataja.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amevitaka vyombo vya dola kuwabaini na kuwachukulia hatua watu wote wanakuwa chanzo cha chokochoko za dini chini.

No comments: