BINTI ANAYETUMIKIA KIFUNGO RUKWA AFAULU DARASA LA SABA...

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya.
Mtoto mwenye umri wa miaka 15 anayekabiliwa na kesi ya mauaji, amefaulu Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi na sasa ameomba kuharakishwa kwa kesi hiyo ili kama ataonekana hana hatia, ajiunge na masomo ya kidato cha kwanza.
Kwa sasa, mtoto huyo wa kike ambaye jina lake linahifadhiwa, yuko katika mahabusu ya kike katika Gereza la Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
Binti huyo mdogo alitoa rai hiyo ya kutaka kuharakishwa kwa kesi yake, kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, ambaye aliwatembelea na kuwapatia heri ya sikukuu ya Krismasi mahabusu wa kike, Jumatatu wiki hii.
Mkuu huyo wa mkoa alibainisha ombi la binti huyo katika mahojiano na gazeti hili baada ya kutembelea  mahabusu hiyo, na kudai kuwa mtoto huyo ambaye amefungwa katika gereza hilo, anatuhumiwa kumuua mtoto mwenzake kwa kumpiga jiwe kichwani wakati wakicheza.
“Baadaye usiku, hali ilizidi kuwa mbaya ndipo mtoto huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa hospitalini, lakini  alifariki dunia muda mfupi baadaye,” alisema mkuu wa mkoa.
Aliongeza kuwa mtoto huyo wakati anatenda kosa hilo Oktoba mwaka huu, tayari alikuwa amefanya mtihani wake wa darasa la saba na kwa mujibu wa matokeo yaliyotoka hivi karibuni, ni miongoni mwa  wanafunzi waliofaulu ambao wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Mtoto huyo alikuwa akisoma katika Shule ya Msingi ya Lusaka katika Wilaya ya Sumbawanga, na kesi yake kwa sasa iko katika Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, bado ikiwa katika hatua za awali.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo ameomba kesi yake iharakishwe kusikilizwa ili iwapo atakuwa na hatia aweze kujiunga na wenzake kwa masomo ya sekondari yanayotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.

1 comment:

Anonymous said...

yule mtoto wa Sumbawanga mambo yake yaliishia wapi, je alihukumiwa au? Maana naona ile haikuwa na makusudi ya kuua may be ugomvi wa watoto na bahati mbaya jiwe likaleta madhara