WATOTO 140 WAZALIWA MKESHA WA KRISMASI DAR...

Watoto 140 wamezaliwa Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke katika mkesha wa Sikukuu ya Krismasi huku watoto wa kiume wakiongoza kwa idadi ya waliozaliwa katika mkesha huo.
Hospitali ya Amana katika Manispaa ya Ilala, ndiyo inayoongoza kwa idadi ya watoto waliozaliwa katika mkesha huo baada ya watoto 62 kuzaliwa ambapo kati yao, 32 ni wa kiume na 30 wa kike.
Muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo, Upendo Kitaponda alisema watoto hao wote wamezaliwa wakiwa na afya njema pamoja na mama zao ambao wengi walianza kurejea makwao baada ya kutokuwa na matatizo.
Hospitali ya Temeke inafuatia baada ya watoto 53 wakiwemo 29 wa kiume na 24 wa kike kuzaliwa katika mkesha huo na kwa mujibu wa muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo, Asha Kitumbuizi, watoto wote wamezaliwa wakiwa na afya njema pamoja na mama zao. 
Aidha, katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, watoto 25 wamezaliwa katika mkesha huo huku  watoto wa kiume wakiwafunika tena watoto wa kike kwa idadi ya kuzaliwa.
Kwa mujibu wa muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo, Anjela Magesa, kati ya watoto hao, watoto wa 15 ni
kiume na 10 wa kike.
Akizungumza mmoja wa wazazi wa watoto hao waliozaliwa wakati wa mkesha Eliminata Sabinius aliyejifungua pacha, alisema ni furaha kwake na familia yao kwa kufanikiwa kuwapata watoto hao wakiwa wenye afya njema.
Alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa amemjalia kujifungua salama ndani ya mkesha huo huku akiwaasa wazazi wengine kuhakikisha wanawapa watoto hao matunzo mema.

No comments: