MADEREVA WA BODABODA WATOANA ROHO KATIKA AJALI...

Madereva wawili wa pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ wamekufa papo hapo huku abiria wao  watatu  akiwamo mtoto wa miaka saba wakijeruhiwa baada ya pikipiki hizo kugongana uso kwa uso katika  barabara ya Majimoto-Mamba  wilayani Mlele.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo ilihusisha pikipiki  namba T 179 CTZ iliyokuwa ikiendeshwa na Mone Ezene (20), mkazi wa kijiji  cha Majimoto  iliyogongana uso kwa uso na  pikipiki namba T 210 VRV  iliyokuwa ikiendeshwa  na Alex Benezedi, wa kijiji cha Ntaswa, Mlele.
Alitaja  majeruhi  ambao walikuwa  wamebebwa  na  pikipiki  hizo kuwa ni Grace Masawe (24) wa Majimoto  ambaye ameumia usoni  na mwanawe, Shauri Masawe (7)  aliyeumua  kifuani. Abiria hao walikuwa wamepakiwa kama `mshikaki’.
Kwa mujibu  wa Kamanda Kidavashari,  abiria  mwingine aliyejeruhiwa katika ajali  hiyo  ametambuliwa  kuwa ni Geofrey Mkoma (32), wa  kijiji cha Kilida, ambaye amejeruhiwa begani abiria wote hao  walikimbizwa katika kituo cha afya  kwa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa  habari  hizi  kwa njia ya simu, Kamanda Kidavashari  alidai  kuwa ajali  hiyo ilitokea  juzi saa  12.30 jioni  wakati  moja  ya pikipiki  hizo ikitoka  Majimoto na nyingine Mamba.
Kwa mujibu wa Kidavashari, chanzo  cha  ajali hiyo  ni mwendo  mkali   na uzembe wa madereva  wote wawili  kwamba tukio  hilo  bado linaendelea  kuchunguzwa.

No comments: