ACHINJWA, KISA KUWAITA KWA MAJINA WEZI WAKE...

Kamanda Dhahiri Kidavashari.
Mkazi wa kitongoji cha Kapepe, tarafa ya Mwese wilayani Mpanda, Saliunga Jinane (43) ameuawa kwa kuchinjwa aliowatambua kwa sura na majina watu waliomvamia na akatishia kuwashtaki Polisi  kama wasingemrudishia fedha walizompora.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari  amethibitisha kutokea mauaji hayo, akisema yalitokea  alfajiri ya siku ya Krismasi, Kapepe.
Akielezea, Kidavashari  alisema  alfajiri ya siku ya tukio  watu watatu  wasiofahamika,  walivamia  nyumba ya  Jinane  akiwa  na mkewe, Leticia Masila (30) na kumlazimisha awape fedha alizokuwa nazo.
Inadaiwa bila ajizi aliwakubalia na kuwapa Sh 50,000 wakazipokea na kuondoka bila kuwadhuru  wanandoa hao.
“Bila shaka watu hao walikuwa na taarifa kuwa Jinane alikuwa na kiasi hicho cha fedha, wakiwa na tochi yenye mwanga mkali walivamia nyumba yake akiwa na mkewe na kumlazimisha awakabidhi fedha zote alizokuwanazo.
“Jinane hakufanya ukaidi aliwakabidhi watu hao Sh 50,000 nao wakaondoka bila kuwadhuru wanandoa hao,“ alisema.
Kwa mujibu wa Kidavashashi, baada ya watu hao kutoka nje, Jinane aliwafuata na kwa sauti akawatamkia kuwa,  anawatambua  na kuwataja kwa majinammoja baada ya mwingine huku akiwafokea na akiwataka wamrudishie fedha  zake  vinginevyo  atawashitaki Polisi.
Inadaiwa kuwa watu hao  waliingiwa na hofu  kutokana na tishio la Jinane, ndipo walirejea  nyumbani kwake wakamkamata  na  kumcharaza  viboko  na kumchinja mbele ya mkewe na kutokomea  kusikojulikama, bila kumdhuru  mkewe.
Kamanda Kidavashari alidai kuwa mke wa marehemu alikiri kumsikia  mumewe  akiwaita  ‘wauaji’ hao  kwa majina  akiwafokea na kuwasihi wamrejeshee fedha walizompora, vinginevyo  angewashitaki  Polisi  kwa kuwa anawafahamu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari  mke wa marehemu  alidai kuwa  hakuweza kukariri  majina ya ‘wauaji’ hao, kwani ilikuwa ni  mara yake ya kwanza kuwaona.
Kamanda alieleza kuwa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na walinzi wa jadi na watendaji wa vijiji, kata  na wananchi kwa ujumla, wameanza kuwasaka watu hao  ambao  wanadaiwa  kujificha  kusikojulikana.

No comments: