ASKOFU KKKT AJIOKOA KWA MLANGO WA NYUMA, AFICHWA...

Vurugu, mabishano na ubabe jana vilitawala katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ngateu, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha baada ya Askofu Msaidizi wa Dayosisi hiyo, Solomon Massangwa na ujumbe wake, kuwasili kujaribu kueleza hali halisi ya mgogoro unaofukuta ndani ya Kanisa hilo.
Lakini tofauti na matarajio yao, walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa waumini waliopinga kikao cha siri baina ya msaidizi wa Askofu na ujumbe wake, uliolenga kukutana na wazee wa Usharika huo.
Akifuatana na Mchungaji mstaafu Gabriel Kimelei na Katibu wa Jimbo la Arusha Magharibi la Dayosisi hiyo, Daniel Medani, Askofu huyo Msaidizi alikutana na umati wa waumini waliokuwa katika makundi kwenye viwanja vya Kanisa hilo, ndipo akaomba kuonana na wazee wa Kanisa.
Hata hivyo, wakati akiomba kukutana na wazee, waumini walicharuka na kutaka kusiwe na kikao cha siri.
Mmoja wa waumini hao ambaye ni kiongozi wa kwaya ya Usharika, Zephania Kwayu, alianzisha sakata hilo, baada ya kupaza sauti akisema: ‘’Hakuna kuzungumza na wazee wakati kila kitu kiko wazi, semeni mbele yetu na mtueleze Mchungaji Mollel (Philemon) anarudi lini kazini na waliosababisha mambo kuharibika wanawajibika vipi?’’
Kauli ya Kwayu iliwapandisha mori waumini wengine ambao nao walipiga kelele kwa sauti za juu kwamba hawataki kusikia chochote zaidi ya Mchungaji Mollel kurudishwa kazini mara moja na bila masharti.
Mollel alifukuzwa kazi Jumatatu na uongozi wa Dayosisi hiyo, akituhumiwa kuwakashifu na kuwakosea adabu viongozi waandamizi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati akiwamo Askofu Thomas Laizer, jambo ambalo linapingwa na washarika wanaoamini ametolewa kafara, kutokana na kujitoa mhanga kuhoji kinachoelezwa kuwa ni ubadhirifu mkubwa katika miradi ya Kanisa.
Wakionekana wazi kukasirika, waumini hao jana walikaribia kuchukua sheria mkononi kwa kutaka kumshambulia Askofu Massangwa ambaye alilazimika kujificha katika ofisi za Usharika huo kupitia mlango wa nyuma wa Kanisa hilo.
Huku waumini wengine wakifunga milango ya Kanisa ili Askofu huyo na ujumbe wake wasitoke, mvua kubwa ilinyesha hali iliyosaidia kuwaokoa na kipigo cha washarika wao.
"Fungeni milango yote asitoke huyo, wamezoea kulinda mafisadi na tunataka Mchungaji wetu arudishwe haraka, la sivyo tuwafundishe adabu hapa hapa kanisani,’’ washarika hao walisikika wakifoka kwa sauti za hasira huku wakiwa tayari kwa lolote.
Jitihada za baadhi ya wazee wa Usharika huo kuwatuliza waumini wao hazikuzaa matunda, huku ujumbe huo ukitoroshwa ili kuokoa maisha yao licha ya mvua kubwa kuwanyeshea.
Baada ya Askofu Msaidizi kufanikiwa kutoroka na ujumbe wake, Kwayu aliwaambia waumini kwamba wametoa hoja kumi za kutekelezwa na viongozi wa Dayosisi ili kurudisha mshikamano kanisani humo.
Moja ya hoja hizo ni pamoja na kurudishwa kazini Mchungaji Mollel, kufukuzwa kazi mara moja kwa Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Israel ole Karyongi na kujiuzulu kwa Askofu wa Dayosisi hiyo,Thomas Laizer.
Mgogoro ndani ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati uliibuka baada ya waumini kupewa waraka wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya hoteli ya Corridor Springs kudaiwa Sh bilioni 11 na benki moja nchini.
Hatua hiyo inapingwa na waumini hao na baadhi ya wachungaji akiwamo Mollel anayetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini ‘aligeuziwa kibao’ na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika Kanisa hilo nchini.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya Kanisa hilo vilieleza kuwa hatua hiyo ilitokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14 na kwenda kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Godwin Lekashu na Karyongi.
Taarifa za ndani zilisema Mchungaji Mollel aliandikiwa barua Desemba 17 na kutakiwa kufanya mambo hayo matatu kabla ya Desemba 23.
Mosi, alitakiwa kumwandikia barua Askofu  Laizer kumwomba radhi na kueleza ni kwa nini alimkashifu na kumdharau.
Pili, atoe tamko katika Mtaa wa Azimio ibadani Desemba 23, akiomba radhi kwa aliyotamka; na tatu ifikapo Desemba 23, awe amemwarifu Katibu Mkuu kwa barua kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo na kwamba yote yafanyike kabla ya Desemba 24.
Vyanzo vya habari vilisema baada ya Mchungaji Mollel kukaidi hayo, kikao cha watu watatu wakiongozwa na Karyongi kiliamua kumfukuza kazi na kumvua uchungaji.
Hata hivyo, habari za uhakika zilisema Mchungaji Mollel hakufanya hivyo kwa madai kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu aliyetukuka kufuata maadili na kamwe hawezi kufanya hivyo, kwani hakumkashifu mtu wala kiongozi yeyote, bali alieleza ukweli juu ya nani wa kuwajibika katika deni la Sh bilioni 11.
Wakati huo huo, habari zilizotufikia baadaye jana zilieleza kuwa, Askofu Laizer amelazwa katika hospitali maarufu ya Kanisa hilo ya Selian, mjini hapa.
Chanzo cha habari kilisema alilazwa tangu juzi. Juhudi za kumwona hospitalini hapo hazikuzaa matunda kutokana na kutanda kwa usiri wa kulazwa kwake. Inadaiwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.

No comments: