WATU 30 WATIWA MBARONI VURUGU ZA MBAGALA...

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwadhibiti watu waliokuwa wakifanya fujo hivi karibuni maeneo ya Mbagala, Dar es Salaam.
Watu zaidi ya 30 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka zaidi ya 20 yakiwamo ya kuharibu na kuiba mali za makanisa katika vurugu zilizotokea Mbagala, Dar es Salaam wiki jana.
Washitakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana ni Masenga Yusuph (28), Hamad Sekondo (26), Shengo Mussa (26), Abdallah Said, Ramadhan Salum, Mashaka Iman (21), Kassim Juma (33) na wenzao 10.
Katika kesi ya kwanza inayoendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka akisaidiana na mawakili wengine Ladislaus Komanya na Joseph Maugo, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa mbalimbali ikiwamo kula njama kuharibu mali na wizi.
Wakili Kweka alidai mbele ya Hakimu Sundi Kifimbo katika mashitaka hayo kuwa kati ya Oktoba 10 na 12 mwaka huu katika eneo la Mbagala, washitakiwa walikula njama na kuharibu mali mbalimbali za Kanisa la Anglikana Tanzania.
Kweka aliendelea kudai kuwa washitakiwa hao pia waliiba vitu tofauti mali ya Kanisa hilo.
Katika kesi nyingine inayohusu vurugu hizo, washitakiwa Mwalimu Said (21), Omari Shabani, Ibrahim Msimbe, Abdallah Said, Paschal Kashiriri, Abdulkadir Haji, Ahmad Juma na Mohamed Chobe walipandishwa kizimbani kwa mashitaka ya kula njama na kufanya uhalifu.
Mbele ya Hakimu Fimbo, Wakili Komanya alidai kuwa kati ya Oktoba 12 Mbagala Kibonde Maji, washitakiwa hao waliharibu madirisha ya vioo, milango, madhabahu na mali nyingine zote zikiwa na thamani ya Sh milioni 80 mali ya Kanisa la Agape Parokia ya Mbagala.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao walichoma moto sehemu inayotumiwa kuabudia mali ya Kanisa hilo.
Katika kesi ya tatu inayohusu vurugu hizo yenye mashitaka 20, Wakili Maugo alidai mbele ya Hakimu Binge Mashabala, kwamba washitakiwa Hashim Ligongo (30), Abbas Said (25), Iddi Selemani (41) Yahya Ndege (53), Daniel Ngambilile (36), Hassan Mohamed (24), Said Mkoba (22) na wenzao watano, walikula njama ya kutenda kosa.
Ilidaiwa katika mashitaka mengine 19 kuwa siku hiyo, Mbagala Kizuiani, washitakiwa walifanya uharibifu wa magari yakiwamo ya Serikali na kuiba katika baadhi ya makanisa.
Katika kesi ya nne, washitakiwa Yusuph, Sekondo, Mussa, Said, Salum, Iman, Juma  na wenzao 13 walidaiwa  kula njama na kuvunja jengo lililokuwa likitumiwa kwa ajili ya ibada mali ya Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT).
Kweka alidai, washitakiwa hao waliharibu samani mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 500 mali ya Kanisa hilo na kutenda kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha ambapo waliiba kompyuta ndogo, kinanda na vifaa vingine vyenye thamani ya Sh milioni 20.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kuiba mali hizo,  walimtishia kwa nondo na matofali mlinzi Michael Samuel. Washitakiwa hao pia wanadaiwa kuchoma sehemu iliyokuwa ikitumiwa kwa ibada.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na kurudishwa rumande. Kwa kuwa makosa mengine kisheria hayana dhamana,  kesi hiyo itatajwa Oktoba 30 kwa ajili ya kutajwa masharti ya dhamana.
Katika hatua nyingine, kijana anayedaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha dini ya kiislamu cha Korani alifikishwa katika mahakama ya watoto.

No comments: